27.2 C
Dar es Salaam
HomeMahojianoMiaka 90 safari ya ushirika: Wakulima wajifunze kwa VICOBA

Miaka 90 safari ya ushirika: Wakulima wajifunze kwa VICOBA

USHIRIKA ni taasisi au chombo cha wanachama walioungana pamoja kwa hiari kwa kusudio la kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii. Hapa nchini kuna aina mbili kuu za vyama vya ushirika; ushirika wa mazao na ule wa kuweka na kukopa. Nje ya hapo, kuanzia miaka ya 2000 kulinzishwa taasisi nyingine ya fedha, inayojulikana kama village community Banks (VICOBA).

Katika makala haya, mwandishi wetu PAUL MABUGA anatupitisha katika mwenendo wa vyama vya ushirika vya mazao ambavyo vilianza kusajiliwa rasmi na serikali ya mkoloni mwaka 1933.

Vyama vya ushirika vya mazao vilifutwa baada ya kuwepo sheria inayovitambua vijiji vya ujamaa mwanzoni mwa miaka ya 1970 na vyama hivyo vikarejeshwa mwaka 1984. Endelea …

Kuna usemi miongoni mwa wakazi wa Shinyanga kwamba “Huyu jamaa nyumbani kwao ni peupe kama shuleni”, ukimaanisha hali ya umaskini ambao kwa mila na desturi za wakazi wa mkoa huu, kipimo chake mara nyingi ilikuwa ni kuwepo kwa mifugo ama nyumba nyingi zilizojaza uwanja.

Hali hiyo kwa sasa ni tofauti. Makazi au nyumbani kwa wakazi wengi siyo peupe kama shuleni. Na hili haliwezi kutenganishwa na kukua kwa ushirika licha ya changamoto kadhaa ambao sekta hii ndogo imezipitia.

“Hiyo kwa sasa hivi hakuna kwa sisi wakulima wa tumbaku na pamba wa Kahama, ilikuwa ni zamani, kwa sasa tuna uhakika wa kipato kutokana na kuwepo kwa ushirika imara,” anasema Robert Mihayo, mkulima na diwani wa Kata ya Nyamilangano katika halmashauri ya wilaya ya Ushetu.

Mihayo ambaye analima pamba na tumbaku anasema chama chao cha ushirika cha Kahama (KACU), kina uwezo wa kutoa bei ya ushindani kwa mazao na wakati mwingine inazidi hata ile elekezi iliyowekwa. Hivyo kuyashinda makampuni binafsi katika huduma.

“Sasa hivi hakuna kukopwa na mizani ya ushirika wetu haipunji na hali hii imepelekea watu kupata fedha na kufanya shughuli za maendeleo, watu wana nyumba za bati, wamenunua mifugo na vyombo vya usafiri kama pikipiki,’’ anasema Mihayo.

Awali anasema kulikuwa na changamoto ya uadilifu miongoni mwa viongozi wa ushirika na hali hiyo ndiyo iliyokuwa ikisababisha wakulima kutofaidika na juhudi zao, lakini kwa sasa anaona kuwa serikali imekuwa makini na ushirika umekuwa na manufaa.

Kauli hiyo ya Mihayo inaashiria kuwapo kwa tumaini kwamba ushirika ukisimamiwa vizuri unaweza kuwa sehemu ya ukombozi kwa mkulima.

Ushirika na Uhuru

Ikumbukwe kwamba ya maendeleo ya ushirika kuonekana kama matubwitubwi kwa wakati huu, lakini pamoja na mambo mengine kama isingekuwa mchango wa sekta hii muhimu pengine uhuru wa Tanganyika ungalipatikana baada ya mwaka 1985.

Yalikuwa maoni ya Tume ya Uangalizi ya Umoja wa Mataifa, Visioning Mission, katika ripoti yake ya Mwaka 1954 kwamba Tanganyika haikuwa na uwezo wa kujitawala hadi baada ya miaka 20 hadi 25.

Haya yanelezwa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Dk. Somo M.L. Seimu, katika kitabu kipya, Agricultural Export Crops and Co-operative Societies in Tanzania,ambacho kinatarajiwa kutoka hivi karibuni.

Sehemu ya kitabu hicho inaeleza:“The report established lack of political enthusiasm among the African for independence. This was demonstrated by lack of a political party and political immaturity among the colonised people that undermined opportunity to demand for the independence. The Visiting Mission report argued and concluded that, owing to such political gap the country could attain independence in 20 to 25 years.1 It was in this case forecasted that, such independence could perhaps somewhat before 1975 but not than 1985.”

Katika tafsiri ya Kiswahili isiyo rasmi:

“Ripoti hiyo (ya Visioning Mission) imejiridhisha na kutokuwepo kwa utayari wa Waafrika (Watanganyika) kwa ajili ya uhuru. Hili linathibitishwa na kutokuwepo kwa vyama vya siasa na watawaliwa (chini ya Mkoloni) kutokomaa kisiasa na hivyo kukosa uhalali wa kudai uhuru.

Tume hiyo ya uangalizi ikahitimisha kuwa, kutokana na ombwe hilo la kisiasa nchi (Tanganyika) inaweza kupata uhuru baada ya miaka 20 hadi 25 ijayo. Na kwa maana hiyo uhuru labda ungeweza kupatikana kabla ya mwaka 1975, lakini siyo baada ya 1985.”

Dk. Seimu anaeleza kuwa, changamoto hii ya kuchelewesha uhuru ilikilazimu chama cha Wafanyakazi wa Tanganyika (TAA), hapo tarehe 07.07.1954 kujibadili kuwa chama cha siasa kilichojulikana kama Tanganyika African National Union (TANU), na Julius Kambarage Nyerere akawa Rais wake.

Hii ilikuwa na hatua ya dharura ili kukabiliana na ripoti hiyo ya uangalizi ya Umoja wa Mataifa na hapo harakati zikaanza. TANU kilianza tu, lakini hakikuwa na mtandao mpana na ili kupata wanachama, kwa haraka, iliungana na vyama vya ushirika vya kikabila, mfano Sukuma Union na hii ilikuwa rahisi kutokana na malengo kushabihiana.

Dk. Seimu anaeleza katika kitabu chake kwamba Vyama vya ushirika vilikuwa kama mshirika mkuu katika kupigania uhuru. Mtahalani, TANU ilishirikiana na Sukuma Union kupinga sera mbaya za kilimo za mkoloni wa Kiingereza na hasa ile ya kupunguza mifugo katika eneo la kilimo cha pamba la Usukuma Magharibi.

TANU ilishirikiana na ushirika huo kutetea hoja kwamba wananchi wakipunguza mifugo yao watakuwa maskini, watakosa mbolea ambayo huzalishwa na mifugo yao, na badala yake wakataka bei nzuri ya mifugo na mazao yao.

Kwa hatua kama hizi, TANU ilipigwa marufuku  na serikali ya mkoloni kufanya shughuli zake za siasa  katika maeneo ya Kanda ya Ziwa, ingawa hili halikufanikiwa kwani bado vyama vya ushirika viliendelea kufanya shughuli za siasa kuiunga mkono TANU kwa siri.

Harakati kama hizi ndani ya vyama vya ushirika, vilimpa nguvu Nyerere kupinga ripoti ya Tume ya uangalizi ya Umoja wa Mataifa, akionyesha kuwa kuna chama cha siasa na shughuli za siasa zinaendelea na kwamba kuna watalaam na Watanganyika wapo tayari kwa uhuru.

Unaweza kuona kuwa TANU iliposhiriki uchaguzi wa Baraza la Kutunga Sheria (LEGCO) pamoja na wengine, Paul Bomani kutoka Victoria Federation Cooperative Union na George Kahama wa Bukoba Cooperative Union, walichaguliwa kuwa wajumbe. Ilibidi wachaguliwe kama wagombea binafsi kwa kuwa ushirika ulipigwa marufuku na ingawa likuwa hivyo, lakini ushirika huo ulichangia ushindi wao.

Kitu kingine anachoeleza Dk. Seimu ni kwamba, vyama vya ushirika havikutiliwa shaka sana na serikali ya mkoloni kwa kushiriki katika siasa kwa kuwa wakati TANU inaanzishwa vilikuwa katika kujiunda upya kupigania maslahi ya wakulima.

Licha ya sifa hii ya dhahabu na mafanikio mengine, lakini ushirika ambao karibu umri wa miaka 90 tangu ulipowekwa katika mfumo rasmi na serikali ya mkoloni, kwa sasa unaweza kusema umejaa misukosuko inayosababishwa na uendeshaji wake.

Malalamiko ya kutozingatiwa kwa misingi ya ushirika, kutozingatiwa kwa maslahi ya wananchi na ubadhirifu ndani ya vyama vya ushirika vanaedelea kutajwa kuwa baadhi mambo ambayo yanadidimiza sekta hiyo ambayo watalaam wake wanaamini kuwa bado kuna nafasi ya mambo kuwa sawa.

Uzoefu wa ushirika

Naibu Mrajis wa Ushirika Mstaafu, Charles Malunde, katika mahojiano na FAMA anasema wadau wa ushirika wanapaswa kuutumia utashi wa serikali uliopo sasa kusukuma mbele sekta hiyo na kumsaidia mkulima na mwanaushirika wa Tanzania.

“Hadi sasa kuna utashi wa kisiasa katika kuusukuma ushirika japo wakati mwingine unatumika isivyo na wanasiasa, lakini inatosha kuwa sehemu ya kurejea kuhusiana na serikali iliyopo madarakani,” anasema Malunde na kuongeza kuwa:

“Na viongozi waliopo wafanye yale yanayoamuliwa na wanachama wao na kuepuka ubadhirifu wa aina yoyote ile ambao unarudisha maendeleo nyuma.”

Mtazamo wake unaungwa mkono na mkazi wa Nyamalapa katika wilaya ya Itilima, mkoani Simiyu, Emmanuel Masenya, ambaye anasema ushirika uliathiriwa na viongozi wasiokuwa waaminifu, lakini sasa usimamizi wa serikali umesadia kurejesha imani.

 “Zamani kama mwaka 2019 kulikuwa na changamoto kwa viongozi wa AMCOS ambapo kama hujui kucheki mizani vizuri badala ya kulipwa kwa kilo 15 unaweza kulipwa kilo kumi, ulikuwa ni wakati ambao kulikuwa hakuna wanunuzi wengine,” anasema Masenya.

Mkulima huyo anasema hata malipo yalikuwa ya kuzungushwa: ”Kwa mwaka huu hali imekuwa ya kuvutia kwa sababu ushirika umeongezewa washindani baada ya makampuni ya ununuzi kuingia sokoni ambapo tunategemea fedha kuendelea kulipwa mapema na huduma kuboreshwa.”

Katibu wa Chama cha Ushirika cha Msingi cha Mwabuki katika Mkoa wa Simiyu, Pili Maduhu, anasema kuna mabadiliko kuliko hapo mwanzo hasa kutokana na kuwapo kwa ushindani katika ununuzi wa mazao.

“Ushindani uliopo umeleta tija ambapo kwa sasa wanunuzi wanashindana na wakulima kunapata fedha taslim na hakuna kukopwa,” anasema Maduhu.

Anasema katika baadhi ya sehemu, soko moja wanaweza kuwepo wanunuzi hadi watano na hivyo mkulima anachagua. Haya hivyo, ushirika siku zote umekuwa kimbilio kutokana na kuwepo fedha za uhakika kila wakati ambapo wakulima wanapeleka mazao yao kuuza.

Hata hivyo anasema chama chao cha ushirika cha msingi kinafanya huduma kama wakala wa kampuni ya ununuzi, ingawa kinafanya kazi katika misingi ya ushirika na kwamba ni jambo ambalo litaimarika zaidi baada ya kuimarisha chama chao kikuu cha ushirika.

Kufanikiwa na kuanguka kwa ushirika

Naibu Mrajis wa Ushirika Mstaafu, akizungumzia hoja kuwa kama ushirika uliweza kufanikiwa zaidi wakati wa kupigania uhuru dhidi ya mkoloni, lakini kwa nini katika Tanzania huru mambo yanaonekana kuwa kama changamoto na hasa baada ya kurejea kwa ushirika katika miaka ya 1980? Alisema:

“Ni kweli tokea ushirika kurejeshwa miaka ya 1980 changamoto zimekuwa nyingi zaidi kuliko mafanikio. Ule ushirika wa awali uhamasishaji haukutoka katika serikali ya mkoloni, isipokuwa yenyewe iliandaa ya kuufanya ushirika ustawi na uhamasishaji ulifanywa na wanaushirika wenyewe,” anasema Malunde.

Lakini hapa baadhi ya watalaam, waliamini kuwa vyama hivyo baada ya kurejea na kupewa mtaji na serikali visingefika mbali maana wanachama na hata viongozi wao wasingekuwa na uchungu na mali za ushirika huo kutokana na dhana ya kutozimiliki. Na hapo ndipo ufisadi ndani ya vyama ulipoanza kumea.

Kabla ya kurejea tena kwa ushirika huo, vyama vya ushirika vilikuwa vimefutwa kwa sheria ya vijijji vya ujamaa katika miaka ya 1970. Vijiji hivyo ndivyo vilivyopewa jukumu la kununua mazao ya wakulima.

Mtaalam huyu wa ushirika anasema: “Hali ilikuja kuwa tofauti serikali ilipourejesha kama inavyotaka na siyo wanaushirika wanavyotaka. Mfano, mara baada ya kuurejesha, kila mwanakijiji alilazimika kuwa mwanaushirika katika kijiji husika. Hali hii iliondoa moyo kwa wale waliokuwa na mapenzi na ushirika.”

Anasema hatua ya kila kijiji cha ujamaa kuwa chama cha ushirika na kila mwanakijiji anakuwa mwanaushirika iliifanya Tanzania kuondelewa katika uanachama wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika duniani.

Na anaona hatua ya kuziruhusu serikali za vijiji kununua mazao pia ilisababisha  changamoto ya kimaslahi na vyama vya ushirika vya msingi ambavyo ndivyo vina jukumu la kununua mazao na kutetea maslahi ya wanachama wake na hasa kwa sababu uanachama ni wa hiari.

Hata hivyo, kutokana na mabadiliko kadhaa ya kijamii na kimaadili, ushirika unaonekana kama ni dhana ambayo pengine imepitwa na wakati na kama sivyo basi ibadilishwe kimtazamo na kujengwa upya ili kwenda na wakati na kumudu mahitaji mapya yanayohitajika.

Kwa hili Malunde anasema dhana ya ushirika haiwezi kubadilishwa na mabadiliko yanayotokea duniani ingawa anakiri kuwa mifumo yake ya kiundeshaji inapaswa kubadilika ili kumudu mabadiliko hayo.

Mathalani, mienendo ya watu na hasa kiutamaduni imebadilika, watu hawana tena hofu na mali za ushirika, baadhi ya viongozi hawaoni tabu kufisadi na kwake anasema inabidi serikali iendelee kutoa elimu juu ya misingi ya ushirika wenyewe.

Katika hili la dhana ya ushiriki, tunaona akina mama katika VICOBA, kama aina ya ushirika wakiendesha mambo yao kwa nafanikio huko kila mmoja akiwajibishwa na wanachama wenzake, lakini imekuwa vigumu katika ushirika wa mazao ambapo wanachama hawana sauti.

Kwa hili Malunde anaona umuhimu wa serikali kuingilia kati baadhi ya matukio hasa pale inapoonekana wanachama wasio na sauti wanaonewa na mali zao kufisadiwa. Katika hali kama hii Serikali inangilia ili kulinda mali za ushirika.

Anasema bado kuna uwezekano wa vyama vya ushirika kufanya vyema katika kumsaidia mkulima na hasa pale walanguzi wanapo nyimwa nafasi. Na anatoa mfano wa chama kikuu Ushirika cha Kahama (KACU).

“Katika misimu miwili iliyopita, makampuni ya ununuzi wa pamba yalidai bei ya zao hilo katika soko la dunia ipo chini na kwamba wao hawaezi kununua kwa zaidi ya Sh. 840 kwa kilo, lakini KACU ilipolipa Sh. 900 na wao katika maeneo ambako chama hicho cha ushirika kipo wakapandisha na kulipa bei hiyo,” anasema.

spot_img

latest articles

explore more

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here