26.4 C
Dar es Salaam
HomeMahojianoMaziwa yanavyotoka shamba, kiwandani hadi dukani(l)

Maziwa yanavyotoka shamba, kiwandani hadi dukani(l)

Na Mwandishi Wetu, FAMA

KATIKA makuzi na maisha yetu kokote kule tulikozaliwa na kukulia, matumizi ya maziwa yamekuwa sehemu yetu. Katika maeneo na sehemu nyingi maziwa huwa ni kwa ajili ya watoto (wachanga kwa wadogo) na kwa ajili ya chai asubuhi kwa watu wazima katika familia. Iwe mijini au vijijini, maziwa hupatikana katika uhalisia wake (fresh) au yakiwa yamegandishwa (yoghut).

Kwa mazoea katika jamii ya Kitanzania, maziwa hununuliwa kutoka kwa familia au mtu anayefuga ngómbe au mnyama yoyote anayetoa bidhaa hiyo ambayo nyakati nyingi huonekana kuwa adimu. Maziwa haya hununuliwa kama yalivyo na kwenda kutumika kwa kuchemshwa au kugandishwa. Hii inamaanisha kuwa kiasi kikubwa cha maziwa hutumiwa bila kupitia katika mchakato, mfumo au hatua zozote za kuhakiki usalama wake.

Mtaalamu na mshauri wa uzalishaji wa mifugo katika shamba hilo Dk. Isaya Ketto.

Wataalamu wa maziwa wanasema watumiaji wa bidhaa hiyo, wanaweza kuwa na uhakika kwa kutumia maziwa yaliyopitia katika mchakato wa viwandani kwani huko ndiko kwenye mifumo inayoweza kudhibiti ubora wa maziwa. Nchini Tanzania, viko viwanda kadhaa, lakini kimojawapo ni Kiwanda cha Maziwa cha ASAS (Asas Dairy) kilichopo Iringa.

Asili ya uzalishaji wa maziwa katika kiwanda hiki ni shamba la mifugo la ASAS lililoko eneo la Idingilanyi lililoko mpakani mwa Manispaa ya Iringa na Halmashauri ya Wilaya Iringa. Shamba hili lenye ukubwa wa ekari 4,000 lilianzishwa mwanzo mwa miaka ya 80 likiongeza idadi ya kazi zinazofanywa chini ya Kampuni za ASAS ambazo historia yake inaanzia mwaka 1936.

Mtaalamu na mshauri wa uzalishaji wa mifugo katika shamba hilo Dk. Isaya Ketto, akijibu moja ya mwaswali ya Waandishi wa Jarida la FAMA aliotembelea shamba hilo anasema kuna tofauti kubwa ya kiusalama kati ya maziwa yanayopitia viwandani ikilinganishwa na yale yanayokamuliwa moja kwa moja kutoka kwa wanyama.

“Kuna utofauti mkubwa kwa maziwa ambayo yamepita kwenye mifumo rasmi kama haya ya kwetu, yamepita kwenye mifumo mizuri ya kitabibu yakapelekwa kwenye tengi yakapozwa vizuri yakaenda kiwandani yakapita kwenye vipimo vya ubora, yakaenda kupashwa joto la juu ni maziwa ambayo yanakuwa salama zaidi kuliko ya mitaani,” anasema Dk. Ketto na kuongeza:

“…kwa sababu kwanza ng’ombe wetu wa hapa shambani…. kila mwaka wanapimwa kipimo cha ugonjwa wa TB ili kuhakikisha maziwa yanayoenda kiwandani hayawezi kumuathiri mlaji yeyote”.

Dk. Ketto anasema magonjwa hayo ambayo kitaalamu yanajulikana kama zenosis, zunotic diseases hutoka kwa mnyama kwenda kwa binadamu kwa njia tofauti na kwamba matumizi ya maziwa yasiyohakikiwa wanaweza kuyapata kwa urahisi.

“…ni rahisi kupata magonjwa ya TB kwa maziwa wanayokunywa mtaani ambayo hawajui historia na matibabu ya ng’ombe, maana yake inamuweka mlaji katika hatari lakini maziwa yaliyopitia katika mfumo salama wa kwetu ni maziwa ambayo ni salama kwa mlaji,” anasisitiza na kuongeza:

“Sisi ng’ombe ambaye anatibiwa maziwa yao hatuingizi kwenye tengi na uzuri ni kuwa kiwandani kuna kipimo maalumu cha kudhibiti kiwango cha antibiotic kwenye maziwa, lakini ukinunua maziwa mtaani mtu katibu ng’ombe leo anapeleka sokoni.”

Dk. Ketto anasema pamoja na matibabu mengine, ng’ombe katika shamba hilo la mifugo la mfano huongeshwa kwenye josho kila Jumatatu kwa dawa kiasi cha lita mbili kwa kila ngómbe, tofauti na uogeshaji wa  josho la kudumbukiza ng’ombe ambalo kwa kila lita moja imwagwa kwenye lita 1,000 kuwaogesha ngómbe wengi.

Mfumo wa ukamuaji  

Ufugaji wa kisasa uliojengwa katika mifumo ya kidigitali katika shamba la mifugo la Idingilanyi huwezesha kupatikana kwa maziwa ambayo huunganishwa na maziwa mengine kutoka katika mikoa ya Njombe na Mbeya, kwa ajili ya kusindikwa katika Kiwanda cha ASAS (ASAS Dairy).

Dk. Ketto anasema n’gombe hukamuliwa kwa kutumia mashine katika eneo maalum la kazi hiyo, na kwamba ukamuaji na upatikanaji wa maziwa hufuatiliwa kidigitali katika mfumo wa kompyuta.

“Katika mashine yetu ya kukamulia tuna mifumo miwili; mfumo wa kiutomatiki kwamba ng’ombe anapoingia hapa taarifa zake ziingie kwenye kompyuta kwa siku zote 305. Taazifa zote zinazomhusu zikiwemo za maziwa na matibabu zitasoma kwenye kompyuta,” anasema mtaalamu huyo.

Anasema eneo la kukamulia kitaalamu linaitwa 16 kwa 2 tandempark, likimaanisha kwamba upande mmoja unachukua ng’ombe 16 na wapili 16 hivyo kuwa na uwezo wa kukamua 32 kwa wakati mmoja.

“Huu mfumo ni tofauti na mifumo mingine kwa sababu kuna vifaa vya kung’amua (sensor) ambayo inachukua ishara kutoka sikio la upande wa kulia wa ng’ombe na kupeleka taarifa za ngómbe husika kwenye kompyuta. Taarifa hizo ni jinsi alivyokamuliwa, lita zake alizotoa ni ngapi na taarifa nyingine ikiwemo joto la mwili la upandishaji,” anasema Dk. Ketto na kuongeza:

“Kwa mfano hapa tuna kundi la ng’ombe 16 yule wa kwanza akiingia taarifa zake zikishasoma kwenye hiyo sensor atapelekwa kwenye laini ya kwanza kukamulia na taarifa zake za maziwa zitarekodiwa; wa pili naye hivyo hivyo mpaka wanaingia wote 16. Kwa hiyo huna haja ya kukaa na daftari kurekodi mmoja mmoja, kila kitu kipo moja kwa moja hivyo kufanya usimamizi uwe rahisi.”

Sambamba na mfumo huo, eneo hilo kuna antena ndogo ambayo kazi yake ni kuchukua ishara na hali ya ng’ombe akiwa kwenye joto la kupandishwa (on heat), hatua inayowezesha daktari kutambua idadi ya ngómbe wanaotakiwa kupandishwa kwa wakati huo.

“Hii inawezesha kuwaandaa (hao ngómbe) katika upandishaji. Hiyo tunaongeza ufanisi wa upandishaji kwa sababu unavyopandisha ng’ombe zaidi ya mara tatu ni hasara. Sisi tunataka angalau baada ya upandishaji wa mara mbili, ng’ombe ashike mimba,” anasema.

Anasema mfumo wa ukamuaji uliowekwa una uwezo wa kukamua ngómbe 400, lakini kwa sasa unafanya kazi nusu ya uwezo wake kwani ngómbe wanaokamuliwa ni 200 tu ndani ya saa moja.

Sehemu ya ng’ombe wa maziwa.

Kuhusu hatua za ukamuaji, Ketto anasema ng’ombe akishaingia kwenye eneo la kukamuliwa kabla ya klasta kuingia kwenye chuchu (kuanza ukamuaji), kuna hatua zinafanyika kuhakikisha maziwa ni safi na salama.

“Lengo ni kudhibiti ugonjwa vipele kwa sababu ni rahisi kuambukiza iwapo labda wanaingia ng’ombe kumi katika hii klasta moja kwa wakati mmoja hasa kama hatuna udhibiti mzuri.

“Kabla ya kukamua tunaangalia ubora wa maziwa kupitia kikombe, unachukua maziwa kwenye kila chuchu kama maziwa yatakuwa yanaganda maana yake yule ng’ombe atakuwa na ugonjwa wa upele maana yake ng’ombe inabidi akamuliwe maziwa yake yaende pembeni yasiende kwenye tengi, unafunga pampu unaunganisha maziwa yanaingia kwenye ndoo ukishindwa kufanya maana yake yale maziwa yataenda kwenye tengi,” anasema Dk. Ketto.

Anasema baada ya kujiridhisha kuwa maziwa ni safi na salama, husafisha chuchu za ngómbe kwa kutumia dawa isiyokuwa na madhara kwa mlaji na akishamaliza kukamuliwa chuchu huchovyeshwa tena kwenye dawa ili chuchu zake ziwe safi hata akienda kulala kwenye matope zisipatwe na madhara.

“Kila kitu hapa kinafanyika kwa teknolijia, yaani kidigitali katika suala la kukamua maziwa na kusafisha chuchu. Huwa kuna mifumo ya mashine ya kukamulia ambayo inatumia roboti ambayo hakuna mtu, kwani ng’ombe akitaka kukamuliwa anaingia sehemu yake.

“Ila kwa mfumo wa mashine hii lazima kuwe na mtu ambaye atasimamia kwahiyo katika hili zoezi la kukagua ubora wa maziwa ni muhimu kwasababu ukishindwa hapa kunaweza kuwa na maambukizi na tatizo la ubora wa maziwa,”anasema.

Anasema katika sehemu ya kukamulia ipo sehemu maalumu ya kumbagua ng’ombe mwenye tatizo la kiafya kuelekea sehemu ya kupatiwa matibabu, baada ya kutambuliwa katika mfumo wa ukaguzi kidigitali.

Dk. Ketto anasema baada ya ngómbe kukamuliwa wale waliokuwa na matatizo lazima wapitishwe kwenye dawa maalumu kwa ajili ya kukinga kwato zao zisioze kwani sifa ya kwanza ng’ombe anayekamuliwa lazima atembee vizuri.

“Kila siku anapokamuliwa lazima apite kwenye dawa wengine wanavyoogeshwa ndio watapita kwenye dawa hiyo mara moja kwa wiki. Kwenye eneo hili pia ng’ombe wanaopita hapa ambao wana hereni (sensor ya kuwasilisha ripoti) upande wa kulia wale wenye shida huonekana moja kwa moja, hivyo hutengwa kwa ajili ya kwenda kufanyiwa matibabu na geti litafunga moja kwa moja mara baada ya kutengwa,” aliongeza.

Kuhusu matumizi ya kompyuta katika shamba la mifugo, daktari wa mifugo wa ASAS Dairy Farm, Dk. Sikili Julio Kibiki anasema inasaidia kutunza kumbukumbu ikiwa ni pamoja na majina ya ngómbe kwani kila mmoja anatambulika kwa jina lake.

“Kuna majina yote ya ng’ombe kila mmoja ana alama inayoonyesha namba yake ukileta tu namba unaona kumbukumbu zote,” anasema Dk. Kibiki na kuongeza:

“Inatusaidia kutunza takwimu mbalimbali ikiwemo maziwa, rekodi zote za maziwa zinarekodiwa hapa na ng’ombe wote wanaopita hapo inasaidia kujua taarifa za ng’ombe ana joto anatakiwa kupandishwa, pia alizaa lini alipandishwa lini alitakiwa kukamuliwa lini utaziona hapa.”

Usindikaji wa maziwa kiwandani

Baanda ya maziwa kukamuliwa na kuhifadhiwa kwenye matangi maalum, husafirishwa kwenda katika kiwanda cha kusindikaji cha Asas Dairy kilichopo eneo la Ipogolo, barabara kuu ya Iringa Mbeya. Maziwa hayo husindikwa kwa katika mfumo wa biadhaa tofauti.

Mratibu wa uzalishaji katika kiwanda hicho, Lipita Mtimila anasema kiwandani hapo zinatengenezwa bidhaa mbalimbali za maziwa ambazo zina uwezo wa kudumu kwa vipindi vya siku saba, wiki sita, miezi sita na hata miezi tisa.

Mtaalamu na mshauri wa uzalishaji wa mifugo katika shamba hilo Dk. Isaya Ketto.

Lipita anasema biadhaa zinazodumu kwa wiki moja (siku saba) ni maziwa ‘freshi’ ya pact wakati yale ya boksi aina ya UHT yanadumu kwa muda wa hadi miezi tisa. Kwa upande wa bidhaa za mgando kwa maana ya mtindi na yogati zina uwezo wa kudumu muda wa miezi sita bila kuharibika.

“Hizi bidhaa mnazoziona zote leo za ASAS hazikuanza siku moja, sasa tuko hatua ya mwisho ya kuingiza sokoni karibu bidhaa tano za maziwa,” anasema Mtimila na kuongeza kuwa kabla ya maziwa kuingizwa kiwandani lazima yapimwe ubora wake.

“Tuna maabara hapa ya kupima vitu mbalimbali ndani ya maziwa, lakini kikubwa ni ubora wake na pia kubaini kama kuna baktria wanaoweza kusababisha magonjwa kwa mtumiaji, tukibaini tatizo lolote hayo hayaingizwi kiwandani,” anasisitiza.

Anasema maziwa yanayosindikwa kiwandani hapo huchukuliwa kutoka shamba la mifumo la ASAS Dairy Farm lililopo Idingilanyi ambalo huzalisha lita mpaka 40,000 kwa siku na kwamba maziwa mengine hupatikana kutoka Rungwe mkoani Mbeya na mkoani Njombe.

“Sisi ASAS huwa tuna-wasupport wafugaji katika maeneo hayo ambako Rungwe tuna wafugaji kati ya 4,500 na 5,000 hivi ambao huzalisha lita kati ya 20,000 na 22,000 hivi, wakati Njombe wako wafugaji wanaofikia 1,200 ambao wanatupa lita kati 500 na 700 kwa siku,” anasema Mtimila na kuongeza:

“Kwa wastani tunakusanya lita kuazia 50,000 kwa siku ambazo zote husindikwa kwani uwezo wa kiwanda chetu ni kusindika lita 150,000 kwa siku kwa hiyo tunazalisha chini ya uwezo. Tunazalisha asilimia kama 33 tu ya uwezo maana changamoto ni kupata maziwa yenye viwango vya ubora unaotakiwa”.

Anasema ili kuwawezesha wafugaji hao wanaleta maziwa bora, wamewaajiri vijana ambao husimamia ukusanyaji wake kwa kukagua mifumo ya ukamuaji na kupima ubora wake kabla ya kufikishwa kiwandani.

“Pamoja na kwamba yanapimwa na kukaguliwa huko huko kabla ya kuletwa hapa, yakifikishwa lazima yafanyiwe tena vipimo ili kuhakikisha yanakidhi viwango stahili na hayaleti shida kwa warumiaji,” anasisitiza Mtimila.

ITAENDELEA…

spot_img

latest articles

explore more

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here