27.2 C
Dar es Salaam
HomeKilimo BiasharaVijana wasomi wajiunga ‘kushambulia’ kilimo

Vijana wasomi wajiunga ‘kushambulia’ kilimo

Na Mwandishi wa FAMA

MIONGONI mwa kilio kikubwa ambacho taifa hili linakabiliwa nalo ni jinsi ambavyo elimu inayotolewa kwa vijana wetu, kuanzia ngazi ya chini kabisa hadi vyuo vya elimu ya juu, imeshindwa kutumika kuwapa fursa ya kujiajiri.

Maelfu ya vijana wanaomaliza elimu katika ngazi mbalimbali wamejazana mtaani, wengine wanazunguka na barua za kuomba ajira katika maofisi mbalimbali. Kwa bahati mbaya, nafasi za ajira nazo hakuna.

Mathalan, mwaka 2014 Idara ya Uhamiaji nchini ilitangaza nafasi za ajira 70, lakini ilijikuta ikipokea maombi ya watu 10,000 kiasi cha kulazimika kufanyia usaili katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam. Kwa wastani kila ajira zinazotangazwa, waombaji ni wengi mno kuliko uhitaji.

Kwa mfano mwaka 2018 Sekretariati ya Ajira ilitoa ripoti yake ikisema kuwa kati ya Novemba 2015 hadi Desemba 2018 maombi ya ajira yaliyopokewa serikalini yalifikia 594,300, kati ya hizo ni waombaji 6,554 tu walipata ajira. Hii ni sawa na asilimia 1.10. Yale maombi ya Uhamiaji ya nafasi 70 ni sawa na asilimia 0.7 ya waombaji wote.

Ni katika kuzingatia ukweli huu wa ugumu wa ajira na jinsi ya kuunganisha elimu itolewayo kwa vijana wa taifa hili, vijana wanaosoma katika Chuo Kikuu cha Mzumbe wameamua kuunganisha nguvu zao ili kupata jibu la ajira zinazotokana na elimu yao. Wamejiunga na kuanzisha kampuni inayoitwa Shamba Langu Agro Solution Ltd.

Wakizungumza na Jarida la FAMA, Ofisa wa Menejimenti na Usimamizi wa Miradi wa Kampuni hiyo, Nelson Kisanga, anasema katika kutambua changamoto kubwa ambayo inakabili vijana wengi wanaomaliza elimu ya juu, walifanikiwa kutumia fursa waliopewa na Chuo Kikuu cha Mzumbe katika kituo cha malezi ya vijana (Resource and Incubation Centre) kuanzisha kampuni yao ili kutumia fursa ya mapinduzi ya nne ya viwanda na kutengeneza fursa za ajira kwao, lakini pia kutoa huduma kwa jamii.

Kisanga anasema miongoni mwa miradi wanayotekeleza chini ya kampuni yao ni kilimo, ufugaji na kutoa ushauri. Anasema anaendesha shamba darasa katika maeneo ya Morogoro karibu na chuo, lakini kutokana na ufinyu wa nafasi wameamua kuchukua shamba karibu na mto Ruaha Mkuu ambako wanaendesha kilimo cha umwagiliaji.

Ili kupata tija zaidi, wamebuni mradi wa ufugaji wa pamoja wa samaki na kuku (integrated fish and chicken farming). Ufugaji huo unatoa fursa ya mifugo hiyo kutegemeana katika chakula. Kadhalika, wanatengeza funza (maggot) kama chakula muhimu cha samaki na kuku, hali inayopunguza gharama za kukunua vyakula vya mifugo. “Ukuzaji wa maggot unapunguza gharama za chakula kwa ajili ya mifugo. Hii ikichanganywa na integrated agronomic farming inatupa fumbuzi wa maana wa kupunguza gharama na huu umekuwa ni ushauri kwa wakulima wetu,” anasema Kisanga.

Kwa kutambua uwezo wa kiuchumi wa wakulima wengi nchini, mfumo wa Integrated wanashuari utekelezwe kwa kutumia vifaa vingi ambavyo vinapatikana katika mazingira waliyoko wakulima. Kwa mfano, mbali ya maboma ya maji na matangi, wanapendekeza utengenezaji wa mfumo huo utumie vifaa vinavyopatikana bure. Kama makopo na ndoo zilizokwisha kutumika.

Mfumo wa Integrated farming unapambana sana na umasikini katika ngazi ya familia. Kwanza ufugaji wa aina hiyo kwa kutumia vifaa vinavyopatikana katika mazingira bila gharama kubwa unawahakikishia wanafamilia uhakika wa kitoweo, samaki, kuku na mayai. Pia kuna uwezekano wa kuuza ziada na hivyo kumudu gharama nyingine za maisha.

Anasema kupitia maonyesho ya sabasaba na yale ya Chuo Kikuu Mzumbe, wamefanikiwa kujitangaza na kuwafikia wakulima mbalimbali katika mikoa ya Morogoro, Pwani, Tanga, Dar es Salaam na Kilimanjaro kwa kuwapa ushauri wa kuendesha kilimo rahisi kwa gharama nafuu ili kukabiliana na umasikini wa kaya na hata kufikia malengo namba moja na mbili ya Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa 2030.

Kisanga na wenzake wanakiri kwamba jamii imenyanyapa sana kilimo kiasi cha kuona kuwa anayejihusisha nacho amekosa kila kitu, jambo ambalo ni dhana potofu kwani hakuna binadamu asiyehitaji chakula ambacho kwa asilimia kubwa hutokana na kilimo. Ni katika muktadha huo vijana wengi wamekuwa wakikwepa kilimo.

Hata hivyo hali hiyo inaweza kubadilika iwapo serikali itatekeleza mpango wake wa program ya vijana kushiriki kwenye kilimo kama ilivyotangaza bungeni kupitia Bajeti yake ya Wizara ya Kilimo ya mwaka wa fedha 2022/23.

Naibu Waziri wa Kilimo, Antony Mavunde anasema serikali inatambua kwamba vijana nchini Tanzania siyo kwamba hawapendi kilimo bali wanakwazwa na mazingira yalikuwa siyo rafiki kuwafanya wafanye kilimo, changamoto ya maeneo, miundombinu, pembejeo, masoko na mitaj.

“Tumekuja na program maalum ambayo inaitwa Jenga Kesho Bora ya Vijana ambayo lengo lake kubwa ni kuhakikisha tunawapatia vijana maeneo, ambayo tutapima afya ya udongo, pembejeo, kuwatafutia masoko na mwisho wa siku lengo letu ni kuwa na kitu kinaitwa Kijiji cha Vijana cha Kilimo,”anasema Mavunde na kuongeza:

“Tunaamini kabisa hii itakuwa sehemu nzuri ya kuweza kuwavutia vijana wengi kufanya kilimo.  Kwa kuanzia tutaanzia hapa Dodoma ndiyo itakuwa sehemu ya pilot (majaribio) zaidi ya ekari 20,000 zitatengwa kwa ajili ya block farms ambazo vijana wengi watahusishwa kushiriki katika kilimo hicho”.

Katika kukuza kilimo wamekuwa wanakuza mbegu ya viazi lishe vitamu, katika mkakati jumishi wa ufugaji wa kuku, samaki na bustani. Katika kukuza mbegu ya viazi hiyo , anasema ni jawabu la lishe kwa watu wanaosumbuliwa na kisukari na kuimarisha afya ya macho.

Viazi hivyo viko aina tatu, mataya, matalunya na meri anayosema inatoka Israel ikiwa na uwezo mkubwa wa kuhimili maji mengi. Viazi hivyo vinachakatwa, kukaushwa na kutoa unga unaofaa kwa kuoka mikate na maandazi.

Vijana hawa wamejikita pia kustawisha ndizi, wakijikita zaidi katika uzalishaji wa ndizi aina ya Kimalindi ambayo imeboreshwa na kupatikana aina mbili ambazo ni William na Granite zenye sifa ya kuhimili magonjwa na ukame. Lakini kikubwa zaidi, uzalishaji wake ni wa uhakika zaidi kama masharti ya upandaji kwa nafasi utazingatiwa. Mbegu hizi zinaweza kutoa kiasi cha vichane 15 kwa mkungu mmoja.

Ofisa wa Menejimenti na Usimamizi wa Miradi wa Kampuni hiyo, Nelson Kisanga(kulia) akizungumza na Mhariri wa FAMA, Jesse Kwayu(kushoto).

Wamepanua wigo kwa kuanzisha ushirikiano na wanaohitimu Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) pamoja na wataalam wa ardhi kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi ili kujenga nguvu kubwa ya kuendesha kilimo cha kisayansi chenye ufumbuzi ambacho vijana wenye utulivu na uvumilvu wanaweza kujiunga na kuona matokeo chanya.

Vedasto Kessy ambaye ni Ofisa Masoko wa Shamba Langu Agro Solution akizungumzia huduma wanazosukuma kwa wateja wao ni pamoja na ujuzi wa kutengeneza funza wa kulisha mifugo yao. Anasema funza hao wanasaidia kupunguza kwa kiwango cha asilimia 50 gharama za chakula. Wana asilimia kubwa ya kiwango cha protini inayohitajika sana na kuku na samaki.

Anaeleza kuwa kinachohitajika ni nzi weusi maarufu kama black fly soldiers ambaye hupatikana porini, lakini habari njema ni kwamba hawaambukizi magonjwa kama hawa nzi wanaotapakaa katika majalala na maeneo machafu.

“Unakusanya takataka za nyumbani zinazooza kama maganda ya viazi, nyanya nk. Kisha unaziweka kwenye ndoo au shimo ulilotengeneza kwa kazi hiyo. Unachukua mayai ya black fly soldier na kuyaweka kwenye hizo taka, baada ya siku 28 unapata hao funza (maggot) ambacho ni chakula bora kabisa cha samaki na kuku,” anafafanua.

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Grayton Ndanze ni miongoni mwa vijana wachache ambao wameona fursa ya kuungana na wenzake katika ndoto yao ya kusuma mbele kampuni yao ili kweli iwe jawabu kwa matatizo ya wakulima. Akiwa chuoni hapo amejiunga na kikundi hicho tayari akiwa amekwisha kujiingiza katika kilimo cha parachichi mkoani Iringa.

Anasema kama ilivyo ada, vijana hawana mitaji, lakini yeye na wenzake watano mwaka 2017 walianzisha kikundi kwa ajili ya kupanda miche ya parachichi ambayo huuza kwa wafanyabiashara wanaotaka kulima zao hilo. Hata hivyo, watatu walijiengua kwa sababu ya uwezo. Hatimaye mwaka 2019 kikundi chao kilikua na kufikia watu 10 wakiwapo vijana na wanawake.

Kikubwa kilichokuwa kinawapa changamoto ni uwezo wa kununua mifuko ya kupanda miche, mbolea ya samadi na mbegu vitu ambavyo vilihitaji gharama kubwa ambazo wengi hawakumudu.

Ndanze anasema katika juhudi hizo, watano katika kikundi chao wamefanikiwa kupata fedha kutokana na kuuza miche nao, wamenunua ardhi na tayari wameshapanda miche ya parachichi katika mashamba ya ekari tatu kila mmoja.

Mkulima huyu anayeibukia katika kilimo cha parachichi anakiri kwamba wenzake ambao hawakuendelea na masomo ya juu baada ya kuhitimu kidato cha nne, kwa sasa wanavuna maparachichi kwa wingi na soko lake ni kubwa kiasi kwamba haoni wakilitosheleza.

“Kwa takwimu zetu tunazojipa tunaona kama tunazalisha sana parachichi aina hii ya Hass, lakini nikuambie yapo makampuni mengi yanakuja kununua mazao yetu yakiwa shambani. Yapo yanayotoka Dubai, Netherlands, India na Kenya ambao kwa kweli wao wamekuwa kama mawakala. Wananunua na kwenda kuyapaki upya kwao kama bidhaa kutoka Kenya,” anasema huku akionyesha matumaini kwamba zao hilo sasa ni mkombozi kwa maeneo ya Nyanda za Juu Kusini au maeneo yote yenye hali ya hewa kama ya huko.

Ndanze pamoja na ukweli kwamba ni mwanafunzi, lakini maisha yake anayamudu mwenyewe akijilipia gharama zote. Baada ya kikundi cha awali kufikia ukomo kwa kila mmoja kujitegemea, mwaka 2020 alianzisha kikundi kingine cha watu watano na kazi kubwa ni kukuza miche ya parachichi.

Lengo ndani ya miaka mitano ni kila mwanakikundi awe amejipatia walau ekari tano za shamba lililopandwa parachichi, kiwango hicho anaamini kinaweza kumpa mkulima walau tani 50 kwa mwaka kiasi ambacho kitamwezesha kumudu gharama za maisha ikiwa ni pamoja na kuhudumia familia yake.

Mkurugenzi Mkuu wa Shamba Langu Agro Solution, Genila Hiel, anasema kuwa wamedhamiria kuwa sehemu ya kutoa majawabu ya matatizo ya wakulima wa nchi hii, lakini pia kutoa mchango wao katika kuyafikia Malengo Endelevu ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa ifikapo mwaka 2030.

Anasisitiza maono na malengo yao kwa pamoja kama kikundi ni kutumia elimu yao kutoa mchango wao katika kwanza kujiajiri wenyewe, lakini pia kuchagiza vijana wengine wajitume kwa kutumia elimu yao almradi tu wawe na dhamira ya kweli ya kufanya kazi kwa pamoja.

spot_img

latest articles

explore more

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here