27.2 C
Dar es Salaam
HomeMahojianoMvinyo: Hazina ya kufuta umasikini wa wakulima

Mvinyo: Hazina ya kufuta umasikini wa wakulima

*Alko Vintages yajikita kuwekeza nguvu kuinua uzalishaji zabibu

Na Mwandishi Wetu, FAMA

WAKATI wakulima wa zabibu wakiendelea kulalama kwa kukosa wataalam wa zao hilo nchini, kampuni ya Alko Vintages iko mbioni kuwafuta machozi kwa kuleta wataalam kutoka Afrika Kusini.

Kwa nini Zabibu

Archard Kato ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Alko Vintages iliyoko jijini Dodoma ambako ni Mji Mkuu wa Tanzania.

Kato amekuwa nyuma ya chapa kubwa na maarufu za Mvinyo za Dompo, For You na nyingine ambazo zimekuwa maarufu ndani na nje ya Tanzania.

Pamoja na kwamba sekta ya kilimo imegawanyika katika maeneo mengi, lakini Kato anatueleza kwa nini aliamua kuchagua eneo la kusindika zabibu ili kupata mvinyo. Zabibu zinastawi kwa wingi mkoani Dodoma, na sio eneo jingine kwa Tanzania.

Kwa maneno yake mwenyewe, Kato anasema kuwa, kilichomsukuma hasa kuwekeza kwenye kilimo cha zabibu ni kutokana na ubobevu kwenye masuala ya mvinyo. Taaluma ambayo anasema kuwa aliipata kutoka katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya Tanzania kwa takribani miaka 11.

“Kwanza kabisa mimi ni Process Engineer (Mhandisi wa Michakato) inayohusiana na usindikaji. Ajira yangu ya kwanza ilikuwa ni katika kituo cha utafiti wa zabibu na mvinyo kilichoko Makutopora Dodoma ‘TARI Makotopora‘ nimefanyakazi hapo kwa miaka 11 nikiongoza idara ya utengenezaji wa mvinyo na ni kupitia eneo hilo ndipo nikawa nimepata ufadhili wa kwenda Ujerumani kwa ajili ya kujifunza zaidi masuala ya mvinyo.

“Baadaye nilikwenda Bangkok, Thailand kujifunza masuala ya kutengeneza mvinyo … kwa hiyo ikawa kwamba kwa miaka 11 najihusisha na masuala ya zabibu na mvinyo.

“Muda mchache baadaye nikaomba kustaafu kazi kwa hiari, nikaja kuajiriwa na kampuni ya kutengeza mvinyo ya Tanganyika Vines Company ambayo ilikuwa ikimilikiwa na Watanzania pamoja na Wajerumani nikaendelea hivyo hivyo,” anasema Kato ambaye kiwanda chake ni cha kipekee nchini kulingana na uwekezaji wa kisasa aliowekeza katika kutengeneza mvinyo.

Anasema licha ya kutumia maarifa yake kwenye kampuni hiyo, lakini hakuwa na matunda mazuri hatua mbayo ilichochea yeye kujiondoa na kuanza safari yake mpya.

“Kutokana na changamoto hiyo nikaona kwa nini na mimi nisiingie mwenyewe moja kwa moja kwa kuwa naifahamu hii kazi vizuri.

“Nikaanza kwa kuanzia nyumbani mwaka 2000 hapo nikitengeneza lita 2,000 za wine kwenye simtank. Changamoto zipo nyingi, lakini kufika mwaka 2007 nikaandikisha rasmi kampuni ya Alko Vintages, tunaendelea hivyo hadi mwaka 2012 ambapo tulipata mkopo wa karibu Sh bilioni 2 kutoka benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) ambao ulinisaidia kuanza kujenga ofisi.

“Hivyo kwanza nishukuru TIB kwani baadaye nilifanikiwa kurejesha mkopo wote na kunisaidia kutanua uwekezaji na sasa tuna vituo vinne vya uzalishaji. Kwa mwaka jana 2021 tuliweza kuzalisha lita milioni 2.4 za mvinyo. Tunaendelea kusaka biashara ya kuziuza japo hatufikirii kama ni changamoto,” anasema Kato.

Anafafanua kuwa kilichomvutia kuingia katika biashara hiyo ni baada ya kuona fursa kubwa iliyojificha kwenye zao la zabibu, huku akiongeza kuwa kusambaratika kwa kiwanda cha Dodoma Wine ilikuwa ni sababu nyingine.

“Niliiona fursa huku sababu zamani kulikuwa na vijiji karibu 93 vilivyokuwa vinalima zabibu mwaka 1980, lakini kufikia mwaka 90 kiwango kilipungua na kutokana na kufa kwa viwanda hivyo hadi mwaka 1995 kilipokuja kiwanda cha Tawico vilikuwa vimebaki vijiji 25 pekee. Hivyo pamoja na mambo mengine lengo langu lilikuwa ni kuwa sehemu ya kuwarejesha wakulima kwenye kilimo cha zabibu,” anasema.

Fursa ya mikopo

Kato anasema kuwa uwepo wa taasisi za kifedha imekuwa ni moja ya chachu inayosaidia kuimarika zaidi kwa uwekezaji wake.

“Mbali na mkopo wa TIB pia tumepata mikopo kwenye benki nyingine kama CRDB na benki nyingine ambazo tumekuwa tukiitumia kwa ajili ya kuboresha biashara nyetu.

“Kwani tunatumia teknolojia ya usindikaji ambazo zinahitaji nguvu kubwa ya kifedha, mfano mwaka jana tumetumia karibu Sh bilioni moja kwa ajili ya kununua mtambo ili kujiimarisha zaidi.

“Kama tunavyofahamu kwamba biashara hii ya uwekezaji wa mvinyo inaushindani mkubwa na karibu asilimia 75 ya wine inayouzwa hapa nchini inatoka Afrika Kusini.

“Sasa nasi tusipowekeza kwenye utaalamu na teknolojia basi itakuwa ngumu kupata soko, mfano sasa hivi tunauza wine China, Marekani na nchi za jirani. Kwa hiyo hatuwezi kufanikiwa kuyashika masoko hayo kama tutakuwa hatujawekeza kwenye teknolojia na kuwa na wafanyakazi wenye ujuzi wa hali ya juu.

“Na katika hilo ndio sababu wafanyakazi wetu wanapata mafunzo Italia na Afrika Kusini,” anasema.

Uhusiano na wakulima

“Ni kweli kwamba bila kuwa na uhusiano mzuri na wakulima ni vigumu kuweza kupata zabibu, kwani uzalishaji wa zababu hapa nchini ni tofauti na sehemu nyingine duniani, sababu utengenezaji mvinyo na ulimaji wa zabibu ni familia.

“Mfano Afrika Kusini peke yake asilimia 70 ya uzalishaji wa mvinyo inazalishwa na wakulima kwa maana ya vyama vya wakulima kama ilivyo pia kwa nchi ya Ujerumani ambako ni asilimia 85 ni vyama vya wakulima.

“Lakini kwa hapa nchini hatuna chama chochote ndiyo sababu kuna uhusiano kati ya mtengeneza mvinyo na mkulima na tunafanya hivyo kwa sababu kuu mbili; kwanza, uwe na uhakika wa kupata zabibu pia kupata zile zilizo bora,” anasema Kato nakuongeza:

“Pia, tumejitahidi kuwa karibu na wakulima kwa ajili ya kuwasaidia mikopo ikiwamo kuwaunganisha na benki moja kwa moja huku sisi tukiwa ni wadhamini wao na hili nina uhakikia linafanywa na sisi tu kwa hapa nchini.

“Matokeo yake ni kwamba mkulima ana uhakika wa kupata mahitaji yake ya kifedha ikiwamo dawa na kuboresha mashamba yao ya zabibu, mfano mwaka juzi msimu haukuwa mzuri na mkopo wameshachukua ikabidi tulipe benki kwa kuamini kwamba msimu ujao mazao yatakuwa mazuri, hivyo ndio namna tunavyoshirikiana.

“Pili tunawasaidia kuimarisha uzalishaji wa zao la zabibu kupitia kuwaunganisha wakulima na kituo cha Makutopora ambapo wamekuwa wakipata ujuzi juu ya namna bora zaidi ya kupruni na kupiga dawa ili waweze kuboresha mashamba yao na kuongeza kiwango cha mazao,” anasema.

Wataalam kutoka Afrika Kusini

Anasema kwa sasa wako katika mkakati wa kuhakikisha kwamba wanashirikiana na wataalam kutoka Afrika Kusini na kwamba Tanzania kuwa karibu na nchi hiyo ni fursa nyingine kwa wakulima wa zao hilo nchini Tanzania.

“Tunataka kushirikiana na wataalamu kutoka Afrika Kusini kwani kuhusu masuala ya zabibu na mvinyo kuwa karibu na nchi hiyo tunapaswa kuiona kuwa ni fursa na faida kubwa kwetu kama nchi. Inapaswa itusaidie katika kuboresha utengenezaji wa mvinyo pamoja na uboreshaji wa mashamba ya zabibu.

“Mfano wakati sisi wakulima wetu hapa hawazalishi zaidi ya tani tatu kwa ekari, wenzetu Afrika Kunisi wanakwenda kuanzia tani tano, 10 hadi 15 kwa ekari moja,” anasema Kato.

Utekelezaji wake ukoje?

“Tumeshaongea na mtaalamu kutoka Afrika Kusini ambaye atakuwa anakuja kwa kipindi fulani ili afanye mafunzo kwa vikundi vya wakulima kwa ajili ya kusaidia kuziba pengo tunaloliona la ukosefu wa wataalam wa zao la zabibu hapa nchini.

“Asaidie kwanza, waweze kuboresha zabibu zao kwa maana ya ubora wa mazao, vilevile kuongeza kiwango cha mavuno kwani hiyo itatusaidia kuongeza ushindani sisi watengeneza mvinyo na wao wakulima,” anasema Kato.

Mkombozi kwa wakulima

Kato anasema kuwa uwepo wa kampuni yake ndani ya mkoa wa Dodoma imekuwa ni sehemu yenye manufaa kwa wakulima wa zabibu.

“Tunao uhusiano mzuri sana na wakulima, ninachoweza kukwambia ni kwamba isingekuwa uwezo wetu ni mdogo nina hakika kwamba wakulima waliowengi wanapenda kuuza zabibu kwetu.

“Sababu sidhani kama kuna mtu ana uhusiano mzuri nao, hata ukienda vijijini ukaliza wakulima watakwambia kwamba mkombozi wetu ni Alko Vintages iwe ni kuwasaidia changamoto zao, lakini pia wingi wa ununuaji wa zabibu,” anasema.

Wataalam bado

Kato anakubali kuwa bado hakuna wataalam wenye ubora unaotakiwa kwenye zao la zabibu, japo walipo wanasaidia.

“Angalau hawa tuliokuwa nao hawana ubora wa nje, lakini wanatusaidia ikilinganishwa na wale wanaopata uzoefu nje ya nchi.

“Ni kweli kuna pengo la wataalam na ndiyo sababu tumewasiliana na watu wa Afrika Kusini ili waje wasaidie wataalam wetu.

“Japo nafikiria sisi watengeneza mvinyo kujadiliana na kuona ni kwa namna gani tunaweza kusaidia hata mabwana shamba wawili au watatu tukawapeleka Afrika Kusini kwa ajili ya kupata ujuzi kwenye zao la zabibu utakaosaidia kunyanyua zao hili, kwani naamini hili ni jambo linalowezekana.

“Hata kama Serikali haitakuwa na bajeti basi tunaweza kushirikiana na watu wa sekta binafsi,” anasema Kato ambaye amekuwa kwenye sekta ya kilimo cha zabibu kwa zaidi ya miaka 30.

Uwezo wa Alko Vantages

Anasema jambo linalohuzunisha nikuona kwamba hakuna takwimu sahihi kwenye zao la zabibu nchini.

“Bahati mbaya hatuna takwimu sahihi zinazohusiana na kilimo cha zabibu, kwani mimi naweza nikajua kiwango ninachonunua, lakini siwezi kupata takwimu za viwanda vingine.

“Sababu naweza kusema kwamba karibu asilimia 75 ya zabibu zinatumika kwa ajili ya utengenezaji wa mvinyo na kiwango kilichobaki ndio watu wanabeba kupeleka Dar es Salaam na sehemu nyingine ikiwamo Kenya licha ya mwaka huu kutokuwa na Uviko-19.

“Lakini naweza kusema kuwa takwimu bado zinakinzana kwani nikichukulia idadi ya wakulima nilio nao na uzoefu wangu wa zaidi ya miaka 30, naweza nikasema kuwa uzalishaji wa zababu hapa nchini haujawahi kuzidi tani 10,000. Bado ni kidogo.

“Najua kuwa takwimu zimekuwa zikionyesha kuwa uzalishaji unafika tani 15,000 unajiuliza zinasindikwa wapi? maana ukienda kwenye viwanda vyetu vilivyopo si ajabu utakuta uwezo wa usindikaji ni Alko Vintages peke yake ambayo inachukua tani 3,000 hizi nyingine zinaenda wapi?,” anahoji Kato nakuongeza:

“Kama sehemu yote ile ni kwa ajili ya kusindika mvinyo ina maana kwamba ni tani 14,000 unajiuliza zinasindikwa kiwanda kipi, maana usindikaji wa mvinyo ni jambo la msimu, mfano mimi kama nina lita milioni 2 siwezi kuja hapa nikawaambia kuwa huwa nasindika lita milioni tano, lazima mtaniuliza kuwa naziweka wapi? Sababu matenki yangu mmeyaona, kwa hiyo tukienda kwenye uwezo hapa Tanzania hakuna kiwango cha lita milioni 5 au 6, kwa hiyo unajiuliza hizi lita ziko wapi?

“Kwa hiyo ninachoweza kusema kwamba hatujaweza kutengeneza lita za mvinyo zinazofika milioni 10, kwani kama ningeweza kubaki kwenye uwezo wangu pekee basi nisingeweza kuzidi tani 2,000. Lakini kwa sababu ya mahitaji ndio maana kuna baadhi ya mvinyo naweka kwenye simtanki ili kuokoa mazao ya wakulima yaliyokuwa yanaharibikia shambani,” anasema Kato.

Anabainisha kuwa jambo analolifanya ni kuhakikisha kuwa anawasaidia wakulima licha ya kwamba mvinyo hiyo ya kwenye matanki haifikii ubora unaohitajika, lakini hawana namna zaidi ya kuwasaidia.

“Ndio maana ukiona kuwa kampuni nyingi ambazo zinatengeneza mvinyo kwa kutumia simtanki isipokuwa chache tu kama Setawico, TBL, kiwanda kimoja kiko Kisutu pamoja na sisi Alko, lakini watu wanakunywa kwani hata sisi kufika hapa tulianzia kwenye simtenki,” anasema Kato.

Bei ya Zabibu

Anasema bei ya soko la zabibu imekuwa ikipanda na kushuka, huku akitolea mfano mwaka 2020 ambao zabibu zilikuwa kidogo na bei ikasimamia Sh 1,600 hadi Sh 1,800 kwa kilo moja.

“Kama unavyojua kwamba bei ya mvinyo wetu haipandi kila wakati, lakini wakulima wetu wanataka bei ipande, mfano mwaka jana tumenunua zabibu kwa Sh 1,400 kwa kilo. Tulichukua tani karibu 3,000 zilizotugharibu zaidi ya Sh bilioni 3,” anasema.

Gharama za Uzalishaji

Kuhusu gharama za uzalishaji, Kato anasema kuwa kwa kiasi kikubwa zinategemea na bei ya uagizaji kwani kwa kiasi kikubwa kila kitu kinatoka nje isipokuwa maboksi na zabibu tu.

“Haihitaji utafiti wa kisayansi kujua gharama hizi zinapandaje kwani zaidi ya asilimia 75 ya gharama za uzalishaji zinategemea kuagiza kutoka nje kuanzia chupa, vizibo, lebo, karatasi za kuchujia karibu kila kitu.

“Wakati mwingine ni ngumu kusema kwamba ni kiasi fulani kwani bei inabadilika badilika, mfano tulikuwa tunasafirisha kontena la chupa kuja nchini. Kontena moja ilikuwa dola 3,800 hadi 4,000, lakini sasa hivi imepanda hadi dola 8,500 na tunashukuru kwamba Shilingi yetu imekuwa imara kwa muda mrefu ikilinganishwa na dola. Hebu fikiria kama dola ingekuwa imefika 2,400 ingekuwaje?

“Jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa tunaongeza uzalishaji zaidi ili kwenda sawia na gharama hizo kwani ukisema ubaki kwenye kiwango chako cha uzalishaji unaweza kushindwa hata kulipa mkopo benki sababu gharama zinaongezaka na na faida inakuwa kidogo,” anasema.

Kipi kifanyike kupunguza gharama?

Anashauri kuwa ili kudhibiti changamoto hizo kodi zinazohusiana na chupa na vitu vingine muhimu zipunguzwe kama siyo kuondolewa kabisa.

“Tatizo hili tungeweza kulidhibiti kwa kuondoa kodi kubwa kwenye vitu vinavyohusiana na uzalishaji wa mvinyo. Hii ingeweza kuwasaidia wakulima wa nchi hii, kwani kilimo cha zabibu kitanyanyua ajira kwa kiasi kikubwa.

“Mimi kinachonipa shida ni kuona zao letu linalotoka hapa linazalisha ajira kwenye nchi nyingine, lakini vijana wetu hapa ndani wanazunguka mtaani bila kuwa na ajira na hakuna mtu anayejali hilo.

“Na niliwahi kuulizwa Afrika Kusini kuhusu mchango wa Serikali kwenye zao hili juu ya kusindika zabibu, lakini nikasema hiyo ni changamoto kubwa ambayo bado inahitaji ufumbuzi ikiwamo kisera. Hata hivyo ninashukuru kusikia kwamba serikali imeomba benki kuweka riba ya asilimia 9, hii itanyanyua kilimo nchini japo ilipaswa kushuka hadi asilimia 5 ili kuweza kusaidia watu kuwa washindani zaidi,” anasema.

Mazingira ya uwekezaji nchini

Kuhusu hilo, Kato anasema Tanzania inapaswa kuchukua mfano wa nchini ya Rwanda ambayo imeweka sehemu moja kwa mtu anayefungua kampuni anapata kila kitu.

“Rwanda wanafanya vizuri, mfano ukiwa unafungua kampuni utakuta TIN namba hapo, na leseni zote jambo ambalo tunapaswa kulichukua. Nimeona hata kwa wenzetu Kenya wao mamlaka za udhibiti wameziita ni mamlaka za kushauri na siyo za kudhibiti kama ilivyo hapa nchini.

“Utakuta mtu aliyeko kwenye mamlaka hii ya udhibiti nao wamejiweka watu wanaotisha sana, kiasi kwamba kufungua kiwanda Uingereza ni rahisi kuliko Tanzania,” anasema.

Akitolea mfano, anasema kuwa amefanikiwa kusajili kampuni yake nchini Uingereza kwa ajili ya kuingia ubia na moja ya kampuni nchini humo ili bidhaa zake ziwe zinapatikana nchini humo.

“Ukiangalia kiwanda ambacho nimeingia nacho ubia nchini Uingereza kwa hapa nchini hakiwezi kupata leseni, jambo la msingi ni Serikali kuangalia mpango wa kuwalea watu wake ili atakapokuwa mkubwa aje azalishe ajira nyingi kwa Watanzania wengi.

“Tuzidi kulelewa, lakini kuna kutishana sana kwa kutoka kwa mamlaka hizi tunazoziita za udhibiti. Ni vema tukaiga mfumo wa wenzetu wa Kenya, sio anakuja mtu kama NEMC hapa anakwambia vitu hadi mwenyewe unabaki unashangaa,” anasema.

Soko la bidhaa

Anasema soko la mvinyo nchini lina ushindani mkubwa likilinganishwa na nchi nyingine na hii nikutokana na kuwapo kwa nchi nyingi ambazo zinauza mvinyo nchini Tanzania.

“Soko letu la ndani hapa liko katika ushindani mkubwa kwani zaidi ya asilimia 75 ya mvinyo inayouzwa hapa nchini inatoka nje ya nchi ikiwamo Afrika Kusini.

“Na Afrika Kusini wanazalisha lita bilioni 1.1 za mvinyo na hawana changamoto ya soko. Ukiangalia mpango wao wa mwaka 2015 walikuwa wanauza asilimia 5 ya uzalishaji wao katika soko la Afrika na mpango wao ni kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.

“Kwa sababu uzalishaji wa mvinyo na zabibu Afrika Kusini umepangiliwa vema na una malengo tofauti na sisi ambao tunafanya holela, hatuna malengo wala mikakati ya kusema kwamba tunawezaje kuingia na sisi kwenye ushindani ikiwamo kulikamata soko la Afrika Kusini kama wao wanavouza hapa kwetu,” anasema.

Anasema hoja siyo wingi wa zabibu bali ni mikakati itakayowezesha Tanzania kushindana kimataifa kwani soko ndio imekuwa changamoto na siyo uzalishaji wa zabibu. Amesisitiza kuwa sekta binafsi ina nguvu ya kulifanikisha soko hilo la nje.

“Tunashuku Mungu kwamba kwa uwekezaji wetu ndio umefanya mvinyo wetu upendwe dunia nzima, kwani tumeshapeleka mvinyo China na bado tuna oda ya kontena nne za mvinyo ambayo inahitajika China na kama tunavyofahamu ukubwa wa soko lao.

“Hivyo na sisi kwa sasa hatuhangaiki sana na soko la ndani bali tunajikita zaidi na soko la nje kwani ndiko fursa kubwa iliko, tayari tumepata soko jingine California, Marekani ambako wamekubali kuchukua kontena moja kwa majaribio ambazo ni Dompo na For You.

“Hivyo, mimi naangalia kwamba tukiongeza kasi ya ubora tunaweza kuwa washindani wazuri kwa wenzetu kwani hatupaswi kuwaogopa sana hawa watu. Pia hatuwezi kuacha soko letu la ndani asilimia 75 litawaliwe na mvinyo wa nchi nyingine, lazima tujitahidi walau tufike asilimia 50,” anasema na kuongeza kuwa licha ya mwaka huu kuwa na kiwango kikubwa cha zabibu ikilinganishwa na uwezo, lakini wanaamini kwa hatua wanazozichukua siku za usoni zabibu zitakuwa hazitoshi.

Mvinyo wa mchuzi

Anasema kuwa kwa sasa kuna mbinu mpya ya soko ambapo nchi kama Afrika Kusini zimekuwa zikiuza mchuzi wa zabibu, hatua iliyosaidia kuziteka nchi ambazo hazilimi zabibu.

“Tunataka kufanya masoko mawili likiwemo lile la mvinyo wa mchuzi kwani ukiangalia asilimia 50 ya soko la Afrika Kusini ni mchuzi ambao unauzwa kwenye nchi kama Canada, Uholanzi, Ujerumani na kwingine ambazo hazilimi zabibu.

“Hivyo na sisi tunataka kulifanya kwa nchini za Afrika Mashariki kwani Uganda, Burundi na Rwanda wote hawalimi zabibu, hata kwenye mikoa kama Mbeya hii biashara inaweza kufanyika unachotakiwa kuwa nacho ni mashine tu kisha unakuja kununua mchuzi hapa kwetu,” anasema.

Kwa kuhitimisha Kato anasema kuwa roho za Watanzania hususan wakulima zinahitaji neno moja tu la Serikali na wala sio fedha, hivyo anashauri kama inahitaji kuona kilimo kinapiga hatua basi lazima iweke kivutio kwenye sekta hiyo.

“Mfano mimi nalipa kodi zaidi ya Sh bilioni 1, lakini tusione kwamba umaana wa mtu ni ukubwa wa kodi anayoilipa peke yake bali ni mguso wake kwenye jamii kuona ana gusa wangapi, ana wakulima wangapi na anatusaidia kuondoa umaskini kwa kiasi gani.

“Kwa hiyo ambacho ningeweza kusema ni kwamba kila mara serikali iwe inahuisha sera zake kwa ajili ya kunyanyua na kuwavutia wakulima kwani itaondoa umaskini na kutengeneza ajira nyingi kwa vijana.

“Kwani kama tunavyojua kuwa zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wako kwenye sekta hiyo, hivyo kwa kuweka uvutiaji huko kutasaidia kutokomeza umaskini na ajira kwa taifa letu,” anasema Kato na kusisitiza kuwa jambo la msingi ni kuwafuatilia wakulima wanaochukua mikopo ili kujua mwendelezo wao.

Kato pia analipongeza Jarida la FAMA kwa kuwamulika wakulima kwani itawasaidia wakulima kupata ujuzi na maarifa kupitia makala zinazochapishwa kupitia wakulima na wataalamu mbalimbali.

spot_img

latest articles

explore more

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here