*Kwa wengi mkulima ni kama tusi
Katika makala haya, Waandishi Wetu, Jesse Kwayu na Neville Meena wanafanya mahojiano na Mwenyekiti wa Muungano wa Vikundi Wakulima Tanzania (MVIWATA), APPOLO CHAMWELA, ambaye pamoja na mambo mengine anazungumzia safari waliyopitia, wanakopotia na wanakotarajia kwenda katika kumkomboa mkulima mdogo. Soma mahojiano hayo ya kina.
SWALI: MVIWATA mna kauli mbiu inayosema ‘mtetezi wa mkulima ni mkulima mwenyewe’, nini maana ya kauli mbiu hii katika dhana nzima ya utetezi wa mkulima mdogo?
“Hakuna wa kutusemea au kututetea zaidi ya sisi wenyewe, ndiyo chimbuko la kauli kusema kwamba mtetezi wa mkulima ni mkulima mwenyewe.”
JIBU: Taasisi yetu ilianzishwa mwaka 1993 na wakulima 22 waliokuwa wakitoka katika mikoa sita ya Tanzania Bara, kupitia Chuo cha Sokoine cha Kilimo (SUA) waliokuwa wanaratibu shughuli za uanzishwaji wa taasisi yetu hii ya MVIWATA.
Kauli hii ilitokana kwamba ilionekana hakuna chombo ambacho kinatetea maslahi ya wakulima wadogo wa nchi hii. Na wakajaribu kuangalia kwamba wakulima tuko wengi na tunao viongozi wengi wa serikali, tunao wabunge, tunao waheshimiwa madiwani, lakini ni kiasi gani wanavyoweza kubeba matatizo ya mkulima na kuyasimamia.
Kwa kutafakari sana ilionekana pamoja na viongozi hao tunao, lakini changamoto za wakulima bado ni nyingi mno na hakuna wa kuzisemea. Leo tukizungumza kwa mfano hata miundombinu huwezi ukalinganisha miundombinu ya vijijini na miundombinu ya maeneo ya mjini. Tunapozungumzia wakulima tunazungumzia watu wanaoishi vijijini ambao ni waathirika wakubwa huduma za kiumiundombinu, afya na changamoto ya masoko.
Ndipo watu hawa 22 wakaona hapana, wakasema hakuna wa kutusemea au kututetea zaidi ya sisi wenyewe, ndiyo chimbuko la kauli kusema kwamba mtetezi wa mkulima ni mkulima mwenyewe.
zimewezesha kuanzisha vyombo vya kifedha kama kuanzishwa saccos nyingi, na vikoba vingi sana na kupitia wakulima katika kuongeza uzalishaji tunaona kuwa katika maeneo mengi uzalishaji umeongezeka.
SWALI: Mwaka 1993 ilianzishwa MVIWATA na historia yenu inaonyesha kwamba mwaka 1995 MVIWATA ilisajiliwa. Mna chochote cha kujivunia katika miaka takriban 20 ya uwepo wenu?
JIBU: Ya kujivunia yako mengi sana. Kwanza ile tu kutuunganisha sisi wakulima wadogo maana walianza wenzetu, lakini mpaka hivi leo tunavyoongea tunazaidi ya wakulima milioni 5 hadi 6, hadi 8, watu wamejiunga kwenye mtandao huu wa vikundi vya wakulima Tanzania.
Kwa hiyo hayo ni mafanikio makubwa sana, sauti yetu nadhani sasa hivi inasikika. Tunaamini kwamba sauti yetu ikisikika na nikirejea katika swali lako la kwanza kwamba tukiungana na kutumia sauti yetu itatusaidia kutetea changamoto zetu mbalimbali. Hata hivyo changamoto ziko nyingi, lakini mafanikio yapo pia.
Kwa mfano wanachama tukija hapa tuko kwenye ofisi yetu, lakini historia tulianza kwenye majengo ya kupanga. Mpaka sasa hivi tuko kwenye jengo letu, tulianza na watumishi wachache, lakini saa hivi tunao wengi wanafika 38 hadi 40. Hayo yote ni mafanikio.
Lakini pia hata kwa wakulima kupitia shughuli mbalimbali ambazo zinafanywa na taasisi yetu hususan za kuwasaidia wakulima, zimewezesha kuanzisha vyombo vya kifedha kama kuanzishwa saccos nyingi, na vikoba vingi sana na kupitia wakulima katika kuongeza uzalishaji tunaona kuwa katika maeneo mengi uzalishaji umeongezeka.
Tukija kwenye maeneo ya upande wa masoko, kidogo imetusaidia kwa sababu kupitia taasisi yetu hii imejenga zaidi ya masoko 13 nchi nzima na ni makubwa. Unapojenga masoko ya mazao ya wakulima moja kwa moja unamsaidia huyo mzalishaji ambaye ni mkulima.
Wameanzisha soko Kibaigwa, Kasanga la samaki, Mbarali kwa ajili ya mchele, Kinole Morogoro na Tawa. Kwa hiyo tunajivunia kwa kweli yapo mengi ambayo nikisema niyaleze yote naweza kuchukua hata siku nzima.
SWALI: Unaweza kueleza mabadiliko ya kukua kwa wakulima wadogo na kuingia katika kundi la juu zaidi, mathalani tukizungumzia zana za kilimo kwamba hapo awali walikuwa wanatumia jembe la mkono na sasa wanatumia labda matrekta madogo, power tiller?
kuna mafanikio makubwa ambayo nisingekuwa hapa, nafikiri hata nisingeyapata. Kipato changu mimi kwa mwaka nilikuwa napata wastani wa gunia 18 ya mahindi.
JIBU: Wapo wengi waliofanikiwa na hata nikijitolea mfano mimi mwenyewe ningekuwa na kitu cha kurudisha nyuma kabla na baada ya kuwa Mviwata na hata ukifika kijijini kwangu, kuna mafanikio makubwa ambayo nisingekuwa hapa, nafikiri hata nisingeyapata. Kipato changu mimi kwa mwaka nilikuwa napata wastani wa gunia 18 ya mahindi na hayo ni kwa ajili ya chakula cha Watoto, mahitaji ya matibabu na vitu vingine. Nilikuwa siwezi kumudu gharama za kuendesha maisha yangu.
Lakini baada ya kujiunga na mafunzo mbalimbali niliyopatiwa yamenisaidia kipato changu kimeongezeka. Ingawa bado sijanunua trekta langu, lakini naona kuna mwanga baada ya muda kadhaa nitanunua. Kwa sasa kipato changu kwa mwaka napata magunia zaidi ya 100, lakini nina kibanda ambacho kwa kweli kina hadhi kama binadamu ukilinganisha na siku za nyuma.
Kwa hiyo najichukulia mimi kama mfano wa kufanikiwa, lakini kuna wanachama wengine wengi nadhani ambao kwa kweli mafanikio ni makubwa pia, na wengine wana power tiller. Unajua maendeleo yanatokana na wewe mwenyewe inaweza ikawa kuna fursa zinakuzunguka, lakini usiyahitaji hayo maendeleo. Kwa hiyo wapo ambao wamefikia kwenye hayo maendeleo ambayo tunayategemea.
watu wameanzisha ushirika wao, lakini wanaongozwa na sheria. Sasa hiyo kitu sisi kwetu tunaona kama ni changamoto, kwa sababu inaathiri na wasiojipanga vizuri kiukweli imeweza hata kuua vile vyama.
SWALI: Unazungumziaje uhusiano uliopo kati ya vikundi vya Mviwata na Ushirika?
JIBU: Kwanza, mfumo wetu wa vikundi hauwezi ukatofautisha sana na ushirika kwa sababu ni kwa nini watu wanaungana? Wanaungana ili kusaidiana katika mambo mbalimbali.
Sasa changamoto iliyopo ya ushirika wa sasa umekuwa sio unaomilikiwa na wanaushirika. Mfano sisi tumeanzisha Saccos na tuliianzisha mwaka 2018 ambayo kwa sehemu kubwa inasapotiwa na taasisi yetu hii ya MVIWATA.
MVIWATA baada ya kuanzisha ile Saccos mwaka 2019 ikaja sheria mpya ya kusimamia ambayo sasa inahitaji vigezo kwamba taasisi yoyote ile ambayo inatoa huduma za kifedha lazima wawe na mtaji tete usiopungua milioni 10, wawe na vifaa kompyuta mpakato, wanatakiwa wawe na wasomi kwa ajili ya kusaidia.
Kwa hiyo ikaja hiyo sheria, sasa unaona kwamba pamoja na kwamba watu wameanzisha ushirika wao, lakini wanaongozwa na sheria. Sasa hiyo kitu sisi kwetu tunaona kama ni changamoto, kwa sababu inaathiri na wasiojipanga vizuri kiukweli imeweza hata kuua vile vyama.