27.2 C
Dar es Salaam
HomeMahojianoMahojiano ya Wahariri wa FAMA na Mtaalamu na mshauri wa uzalishaji wa...

Mahojiano ya Wahariri wa FAMA na Mtaalamu na mshauri wa uzalishaji wa mifugo ASAS Dairy Farm-ll

Na Mwandishi Wetu, FAMA

Sehemu ya mahojiano ya Wahariri wa FAMA na Mtaalamu na mshauri wa uzalishaji wa mifugo katika shamba la mifugo la ASAS (ASAS Dairy Farm) lililopo Idingilanyi, Iringa, Dk. Isaya Ketto.

Swali: Bwana Keto hebu tuambie shughuli za hapa

DK. KETTO: Katika mashamba ya ASAS tunafanya shughuli mbalimbali, kubwa ikiwa ni uzalishaji wa malisho na pia tunazalisha mifugo. Pia tuna uhifadhi mkubwa wa chakula ambacho tunazalisha kutoka mashambani kwetu. Kwa hiyo sisi misingi miwili ambayo inatutofautisha na wengine kama ASAS tumejikita kwenye utunzaji wa ndama. Tuna kituo cha kipekee cha utunzaji wa ndama, lakini pia tuna mifumo mizuri ya uzalishaji wa malisho. Kwa mfano tukitaka kuzalisha nyasi za mifugo ni lazima udongo upimwe maabara na baada ya hapo ndio tuchague ni aina gani ya mbolea tutatumia kurutubisha. Hii ni kwa sababu kile mnyama anachokula kutoka kwenye mmea, ndio kinatokana na kirutubisho kilichopo kwenye udongo. Kwa hiyo tumejikita hapo ili kuhakikisha tunapata ndama wazuri, lakini pia lishe inakuwa nzuri kwa lengo la kupata ng’ombe wazuri wanaokamuliwa na kutoa maziwa mengi.

Swali: Umezungumzia utunzaji wa kipekee wa ndama, huu ni utunzaji wa aina gani?

DK. KETTO: Hawa ndama lengo kubwa la utunzaji huu kwa mfumo unaouona hapa ni kuhakikisha kwamba tunampandisha ndama wetu akishakuwa ngómbe mkubwa akiwa na umri wa miezi 13 mpaka 15.  Kwa hiyo mfumo wetu unamfanya ndama aweze kuwa na ongezeko la uzito ambao ni mzuri mpaka anafikia kilo 250 akiwa na mwaka mmoja na hapo ndipo anakuwa tayari kupandishwa. Wapo hawa ndama wanaokaa kwenye hizi fensi kwa miezi miwili na katika muda huo wanapata chakula maalumu kutoka kiwandani ambacho kina protini nyingi na virutubisho vizuri. Pia kunakuwa na maji ya kunywa wakati wote, maana yake hatuna restriction ya chakula kwa ndama kama hawa. Pia wanakunywa maziwa kwa wastani wa lita nne kwa siku kwa kila ndama. Kwa hiyo wakishafikia miezi miwili tutawahamisha kwenda kwenye eneo jingine ili tuweze kuwaandaa kwa ajili ya kumkausha kwenda kwenye kundi lingine la wale ambao wanakua.

SWALI: Sasa unasema wakishatoka hapa wanakuwa wamekaushwa, maana yake nini?

DK. KETTO: Wakitoka hapa wanaingia kwenye makundi mengine katika haya makundi huku ndio wale ambao wanatoka kule wanakuja huku kwa umri na katika kila kundi kuna umri wa miezi mitatu, minne na wale ambao wanatarajia kukaushwa wapo upande wa kule ambao ni wakubwa.

SWALI: Kukaushwa wanakaushwa nini?

DK. KETTO: Maana yake wanategemea chakula chao kwa mfumo wa majani na vyakula vingine si maziwa tena. Hawanyonyi tena. Wananyonya miezi miwili tu. Kwa hiyo wanahamishwa wanaingizwa kwenye makundi ambayo ndio zile kempu za nje kule ambayo ni makundi ambayo tunamuandaa aweze kuwa mtamba ambaye tutampandisha akiwa na kilo 250 kwa mwaka mmoja.

SWALI: Kwa hiyo chakula cha upande huu mwingine ni kipi?

DK. KETTO: Tulichoongezea huku ni PA ambayo tunaita ni fibers diet. Hii hapa siyo kwamba watakula lishe, lakini inasaidia kutengeneza matumbo yao kama mnyama mwenye matumbo manne lile tumbo la taulo linategemea sana namna anavyopata kupata nyasi ngumu kama hizi, maana yake tukishindwa kumpa chakula kama hiki hata tumbo lake haliwezi kuwa vizuri kuwa tumbo la mnyama mwenye matumbo manne.

 SWALI: Ulituambia akifika mwaka mmoja anatakiwa kuwa na kilo 250 unaweza kutuambia makadirio kwamba kasi ama mwenendo wa uzito wake kuongezeka ukoje kwa maana siku hadi siku?

DK. KETTO: Sisi tunapima uzito wa ndama kila wiki ili tuweze kupata ongezeko la uzito kwa siku, hii hapa ndio inatupa kielelezo ni kwa namna gani ukuaji wa ndama unakwenda na tunafuatilia kwenye kompyuta. Tuna program maalumu kila baada ya wiki tunakwenda kuangalia ongezeko la uzito wa ndama ukoje, kwa sababu tukishindwa kumpandisha akiwa na mwaka mmoja maana yake tutakuwa tumepunguza muda wa ule mtamba kufanya kazi.

SWALI: Wastani wa uzito wake unakwendaje?

DK. KETTO: Ongezeko ni wastani wa nusu kilo gramu 500 mpaka gramu 600 kwa siku na hii inabadilika sana baada ya kuwa na mfumo wa (pets). Hapa ndama wako vizuri wanakunywa maji muda wote, wanakula chakula kizuri wako mazingira hayana inzi kwa hiyo wako vizuri hata ukuaji wao unakua ni mzuri tofauti na mfumo wa kawaida mbao wangekuwa katika mazingira ambayo siyo rafiki.

SWALI: Baada ya hapo?

DK. KETTO: Baada ya hapa wanakwenda kwenye kundi la mwisho ambako wanaingizwa kwenye makundi ambayo tunawaandaa kuwa mtamba. Katika eneo hili tunawakuza kuwa mitamba ambayo imefikia umri wa kupandishwa. Kwa hiyo wanachanganywa, kuna mitamba iliyopandishwa na mitamba yenye mimba. Mitamba ambayo tunagundua ina mimba tunaiweka nje ambako inapata lishe tofauti. Wale wanaogundulika wana mimba wanapelekwa kwenye kundi lingine la nje na wakishazaa watapelekwa kwingine kwa ajili ya kukamuliwa maziwa. Wakifika miezi saba ya mimba, miezi miwili kabla ya kuzaa wanakaushwa ili waanze kupata chakula maalumu kiweze kumuepusha na magonjwa ambayo yanaweza kutokea.

SWALI: Malisho hayo ni yapi?

DK. KETTO: Hawa ng’ombe wanapata lishe maalumu, hiki chakula cha silage ni maalumu kwa ng’ombe wanaozaliwa. Silage ni mahindi yaliyochachushwa katika mchachusho maalumu. Tunavuna mahindi yakiwa mabichi kabisa, tunayapeleka katika eneo maalum ambako yanahifadhiwa ili kupata tindikali inayotakiwa kuondoa wadudu ambao hawahitajiki. Tunatumia bakteria maalumu wa kuondoa tindikali ili kuepusha athari kwa ng’ombe. Chakula chao kinachanganywa kwenye mashine na ni mlo kamili. Kwa siku moja ng’ombe mmoja anakula kilo 33 ndani ya milo mitatu kwa maana kwamba kwa mlo mmoja hula kilogramu 11. Kwenye milo mitatu kuna chakula wanakikuta asubuhi baada ya kukamuliwa, mchana na jioni baada ya kukamuliwa.

SWALI: Mnajiridhishaje kupata uthibitisho kama ameshika mimba?

DK. KETTO: Kuna kiashiria cha kwanza kama hajashika mimba kwa siku 21 inabidi arudie, ila kama ameshika hatarudia. Baada ya miezi mitatu tunajirisha kupima kuangalia tena, kama hana mimba inabidi turudie kumfuatilia kumpandisha tujue kuna tatizo gani linalomfanya asishike mimba. Hata hivyo, ni mara chache hutokea kwamba mtamba hajapata mimba baada ya kupandishwa.

SWALI: Ikitokea huwa inasababishwa na nini?

DK. KETTO: Inasababishwa pia na mtu ambaye ametambua lile joto, kwa sababu ng’ombe ili umpandishe lazima aingie kwenye joto, labda kachelewa saa kadhaa kawahi kupandisha au kachelewa, ila sasa hivi tuna vifaa maalumu tunatumia mtu kutambua joto moja kwa moja na kutuma taarifa kwenye kompyuta na ng’ombe akapandishwa kwa muda sahihi.

SWALI: Kifaa kinawekwa wapi?
DK. KETTO:
 Kuna hereni maalumu wanazovalishwa ng’ombe kwa ajili ya utambuzi. Kuna programu ya kuangalia taarifa mbalimbali za ngómbe husika ambazo ni uzito wa ng’ombe, kupitia hereni anayovalishwa, taarifa za maziwa na za afya yake kama ni mgonjwa na taarifa zote hizo zinasomeka kwenye mfumo wa kompyuta. Katika mfumo huu, ndiko pia ngómbe wenye matatizo ya kiafya hubaguliwa na kuwekwa kando kwa ajili ya kupata matibabu.

spot_img

latest articles

explore more

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here