Na Mwandishi Wetu, FAMA
Kwa muda mrefu nchi nyingi za Kiafrika zimekuwa zikitegemea kilimo kuendeleza uchumi wao. Asilimia 30 ya kipato cha nchi kinatoka kwenye kilimo wakati asilimia 60 za nafasi za kazi zinatoka sekta hiyo pia.
Aidha, kwa mujibu wa Serikali jumla ya wanafunzi 1,956 sawa na asilimia 88.9 ya lengo wamedahiliwa katika vyuo vya kilimo kwa ufadhili wa Serikali. Kati ya hao ngazi ya astashahada ni wanafunzi 1,030 na stashahada ni 926 ambapo watagharimiwa masomo kwa Sh milioni 972.
Matokeo muhimu ya Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya mwaka 2019/20 yaliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) yanaonesha kuwa kati ya kaya 12,007,839 zilizopo Tanzania (11,659,589 Tanzania Bara na 348,250 Tanzania Zanzibar), 7,837,405 (asilimia 65.3) zinajihusisha na shuguli za kilimo.
Kati ya hizo, kaya 5,088,135 (asilimia 64.9) zinajihusisha na kilimo cha mazao tu, ikifuatiwa na kaya 2,589,156 (asilimia 33.0) ambazo zilijikita katika kilimo cha mazao pamoja na ufugaji na idadi ndogo ya kaya (chini ya asilimia moja) zilijihusisha na ufugaji wa samaki na ufugaji wa kuhamahama.
Hii ni sawa na kusema kwamba kilimo bado ni nyezo muhimu ya uchumu katika maisha ya Watanzania.
Aidha, katika nyanja hiyo, kilimo cha mbogamboga ni kati ya vile vinavyoendelea kuchukua umaarufu kwa kuhusisha watu wengi hususan katika maeneo ya mijini pamoja na kile cha matunda hususan embe.
Pamoja na aina hii ya kilimo kuonekana kutokuwa maarufu kama ilivyo kwa mazao mengine ya chakula, lakini ukweli ni kwamba imeendelea kupata wafuasi wengi siku hadi siku.
Kilimo hiki kinafanyikaje
Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA)kilichoko mkoani Morogoro pamoja na taaluma nyingine ambazo zimekuwa zikitolewa, maarifa kuhusu kilimo cha mbogamboga ni miongoni mwa masomo yanayotolewa chuoni hapo kupitia wataalamu waliobobea.
Romani Mfinanga ni Meneja wa Kitengo cha Bustani SUA anabainisha kuwa eneo hilo ni kati ya yale muhimu yanayotazamwa na chuo hicho.
Kwa mujibu wa Mfinanga, pamoja na mambo mengine kitengo hicho pia kinahusika na masuala yote ya uzalishaji pamoja na utafiti wa matunda, viungo vyote, maua pamoja na teknolojia ya kuhifadhi mazingira.
“Kitengo hiki kina wafanyakazi zaidi ya 10 ambao wana jukumu la kuwapokea wanafunzi wa Shahada za uzamivu wanaofika kwa lengo la kujifunza wakitokea katika fani nyingine.
“Upande wa kitengo cha uzalishaji matunda, eneo hili tunazalisha maembe ya muda mfupi, mapera na parachichi ambayo mkulima anaweza kuanza kuvuna matunda hayo miaka mitatu tu baada ya kuwa amepanda.
“Hii inatokana kwamba tumeweza kupunguza ungalishe ambapo mkulima anaweza kuvuma matunda yake ndani ya miaka mitatu na kwa kiwango cha kuridhisha, na ikumbukwe aina hii ya mbegu zilizopo hapa ni ngumu kupata kwenye maeneo mengine,” anasema Mfinanga.
Anasema SUA imekuwa ikitumia mbinu za ubebeshaji miche hatua ambayo inaharakisha uvunaji wa matunda husika ndani ya miaka mitatu tu.
“Mfano sisi tunatumia miche shina ambayo inapandwa kwa ajili ya kuuandaa kuja kubebeshwa aina ya tunda ambalo unalitaka wewe kama mkulima, na hii hustawi sehemu nyingi ambapo mingi inakuwa ni jamii ya sindano nyeusi, sindano nyeupe (embe sindano) pamoja na embe kamba haya ndiyo yanatumika sana sababu yana uwezo wa kustawi maeneo mengi ya Tanzania.
“Kwa hiyo kwa kutumia shina unaweza ukabebsha embe jingine ambalo unalitaka mfano bolibo, dodo na aina nyingine ndani ya miaka mitatu,” anasema Mfinanga.
Mambo ya kuzingatia
Anasema pamoja na kuwapo kwa urahisi huo wa kuvuna matunda ndani ya miaka mitatu, lakini yapo mambo muhimu ya kuzingatia kwa mtu anayehitaji kufanya hivyo kwa mafanikio zaidi huku akitahadharisha kuwa embe lililobebeshwa linahitaji umakini mkubwa.
“Kiuhakika embe ambalo halijabebeshwa linaweza kukaa miaka 10 hadi 30, japo kadri umri unavyoongezeka uzalishaji wake unakuwa unapungua sawa na kwa hili lililobebeshwa, unachopaswa kukifanya ni kufanya uangalizi wote unaohitajika wa katika kutunza mmeya ikiwamo kuupa maji ya kutosha kupulizia dawa na mambo mengine ili kuusaidia kuwa na afya njema wakati wa uzalishaji.
“Sasa hivi Tanzania tuna changamoto ya wadudu kwenye miti ya maembe na machungwa ambao wanaitwa fitfries ambao kwa sasa wametoka kwenye matunda kwenda kwenye mboga mfano matikiti, sasa mkulima asipochukua tahadhari mapema ya kudhibiti kwa kutumia viuatilifu ambavyo vinashauriwa na wataalamu ambao wanatambulika basi matunda yake sokoni yatakuwa hayana ubora amabao tunapaswa kuwa nayo,” anasema Mfinanga.
Muingiliano ni changamoto
Mtaalamu huyu anasema kuwa muingiliano wa wafanyabiashara wanaosafirisha bidhaa kutoka nchi moja kwenda nyingine umesababisha kuibuka kwa magonjwa na wadudu wanaoshambulia mbogamboga na matunda.
Aidha, anayataja mabadiliko ya tabianchi kama sehemu nyingine ya kusababisha mlipuko wa magonjwa kwenye matunda na mbogamboga.
“Mbinu yakukabiliana na athari hizi za wadudu ni pamoja na kutumia njia za kisasa na zinazopendekezwa na wataalamu na kuacha udhibiti wa mazoea ambao umekuwa haukomeszi tatizo, pia kupata ushauri kutoka wa wataalam, pia anaweza kutumia mimea mingine ili kudhibiti wadudu,” anasema Mfinanga.
Mbali na kuwa na matunda aina ya embe pia SUA ina miche ya matunda ya pasheni tofauti tofauti ambayo unaweza kuvuna ndani ya mwaka mmoja baada ya kupanda huku akisisitiza kuwa udongo ni moja ya nyenzo muhimu pale unapokuwa unalima zao hilo.
“Tumekuwa tukiwashauri wakulima wetu kutumia udongo mzuri ili kupata mazao yaliyo bora, mfano wakati wa kupanda tunashauri mkulima achanganye udongo wenye mbolea ya kuku au ya mifugo yoyote.
“Pia anaweza kutumia udongo wa misitu ambao unaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kupata mazao mazuri, hii ina maana kwamba kama mkulima ameweka toroli nne za udongo wa mbao basi anaweza kuweka nyingine tatu za mbolea ili iweze kuleta mchanganyiko mzuri na rutuba ambayo ni kubwa zaidi.
“Bahati nzuri pasheni haichukui muda mrefu kwani ndani ya siku 14 na 21 inaaza kuchipua,” anasema Mfinanga.
Kilimo cha Nyanya
Kilimo cha nyanya ni moja kati ya mazao ambayo yamekuwa yakiwavutia vijana wengi zaidi kulima nchini Tanzania, kwani wengi wamekuwa wakiwekeza huko kwa kuamini kuwa ni sehemu ambayo wanaweza kutumia muda mfupi na kutengeneza fedha nzuri.
Katika hilo Mfinanga anasema ni kweli, lakini ili ufikie mafanikio hayo basi unatakiwa kuzingatia mambo muhimu yafuatayo. “Kwa hapa SUA kuna aina nyingi ya nyanya na hivyo teknolojia ya kubebesha nyanya kama ilivyo kwenye mazao mengine kama embe na pesheni inafanyika pia.
“Kuna mbogamboga kama nyanya hasa nyanya chungu au bilinganya ambazo hizi zimekuwa ni rahisi zaidi kwani inatumia muda mfupi hasa pale mkulima anapobebesha mcheshina, kwani mboga zote hizi licha ya kuwa ni kati ya zile zinazoshambuliwa sana na magonjwa kwa kutumia mbinu ya kubebesha siyo rahisi kushambuliwa na magonjwa wala ukame tofati na kama mkulima angeamua kupanda moja kwa moja,” anasema Mfinanga na kuongeza kuwa sasa hivi kuna kampuni ambazo zinajaribu kutengeneza mbengu za nyanya na bilinganya zenye uwezo mkubwa wa kupambana na magonjwa huku SUA ikiwa pia na mpango huo.
Uzingatie nini unapotumia mcheshina?
Mfinanga anasema kutokana kwamba unapokuwa unataka kupanda kwa njia ya mcheshina unalazimika kuhamisha mche kutoka kwenye udongo wake, basi unapaswa zaidi kuzingatia sehemu yenye kivuli.
“Ili upate matokeo baada ya kuhamisha mche na kuupandikiza sehemu nyingine basi unashauriwa uiweke sehemu ambayo kuna kivuli kwani unakuwa unaipeleka kwenye eneo jipya, kinyume na hivyo basi mmea husika utanyauka,” anasema Mfinanga.
Kilimo cha pilipili
Kama inavyofahamika kwamba kwa sasa kilimo cha pilipili nacho imekuwa ni sehemu ya vile vinavyofanya vizuri kwa kuwanufaisha wakulima, SUA pia haiko nyuma katika kutoa mafunzo kwa wakulima huku pia ikitumia mwanya huo kuandaa wataalamu.
“Mkulima anapohitaji kupanda pilipili basi tunamshauri kuchagua kulingana na eneo lake la ardhi, lakini pia mbegu ya varati 1 inaonekana kuwa bora zaidi, ukiacha hiyo kuna pilipili mbuzi ambazo hazishambuliwi sana na wadudu zaidi ya ndege,” anasema Mfinanga.
Eneo la mbogamboga pamoja na matunda yanachukua sehemu kubwa SUA kwani pamoja na kufanya tafiti kwenye mazao mengine pia kimekuwa kikiendesha kwenye mazao jamii ya matikiti na matango.
“Tuna bustani nyingi ikiwamo ya tikiti maji, tango na mboga nyingine ambazo hazitumii dawa za viwandani katika kudhiti wadudu, hivyo hapa tunatumia mbinu za asili katika kukabiliana na wadudu.
“Hii imekuwa ni moja ya sehemu ambayo wakulima wamekuwa wakiitumia kujifunza mambo mbalimbali ikizingatiwa kuwa wakati mwingine kumekuwa na changamoto ya mvua.
“Hivyo kutokana na wananchi wengi kutokutegemea sana mvua, ndio maana baadhi wamekuwa wakilazimika kuchimba visima kwa kuammini kwamba bila maji basi hakuna kilimo, hivyo nasi kama chuo tunaona kuna haja ya kuja na utafiti wa kulima mazao haya bila kuhitaji maji ili tuone ni kwa namna gani tutaweza kuwasaidia wakulima kupitia aina hii ya mbegu,” anasema Mfinanga.
Bidhaa wanazozalisha zinaenda wapi?
Mfinanga anasema kuwa pamoja na kwamba wamekuwa wakitumia muda mwingi katika kufanya utafiti kwa kuzalisha mbogamboga, matunda na bidhaa nyingine, hiyo pia imekuwa ni sehemu ya wao kupata kipato.
“Ni kweli kwamba tumekuwa tukizalisha bidhaa mbalimbali ambazo ni mbogamboga na matunda ila mwisho wa siku tumekuwa tukivuna na kupeleka kwenye maduka ya chuo na huko walimu na wanafunzi wamekuwa wakinunua kwa ajili ya mahitaji yao ya kujenga mwili, hiyo inakuwa ni faida kwetu pia licha ya kutoa elimu,” anasema Mfinanga.