26.4 C
Dar es Salaam
HomeMahojianoMtaalamu WetuDUNIA YA SAMAKI: Kifaranga cha kambale ghali, ila sato wameteka soko 

DUNIA YA SAMAKI: Kifaranga cha kambale ghali, ila sato wameteka soko 

Na Mwandishi Wetu, FAMA

Tasnia ya ufugaji wa viumbe hai kwenye maji ni katia ya eneo linalochukua nafasi kubwa kwa sasa nchini Tanzania.Pamoja na kwamba ufugaji wa viumbe aina ya samaki ndio umezoeleka zaidi, lakini ukweli ni kwamba nyanja hiyo ni pana zaidi tofauti na unavyofikiria.

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kilichoko Kaskazini Magharibu wa mji wa Morogoro ni miongoni mwa maeneo ambayo ni kitovu cha ufugaji huo wa viumbe hai kwenye maji.

Lakini kama hiyo haistoshi, kimekuwa ni sehemu ya kutoa maarifa kwa watu mbalimbali wanaohitaji kujikita kwenye fani ya ufugaji wa viumbe hai vya majini ikiwamo samaki bure.

Stella Gengi ambaye ni mtaalamu na mbobezi katika eneo la ukuzaji wa viumbe hai kwenye maji chuoni hapo ambapo anasema sekta hiyo ni pana tofauti na baadhi ya Watanzania wanavyoitafsiri.

Hapa anafafanua kwa upana maana ya ufugaji wa viumbe hai kwenye maji.

“Watu wamekariri kwamba unaposema ufugaji wa viumbe hai kwenye maji basi unamaanisha samaki jambo ambalo siyo kweli, kwani nyanja hii ni pana na unapoizungumzia unahusisha mimea na wanyama wanaoishi kwenye maji wanaoweza kufugika wakiwamo samaki.

“Tunapoongelea mimea inayoishi kwenye maji ipo mingi, lakini ile maarufu ambayo watu wengi wanaijua kuna azola, mwani na mingine,” anasema Stella.

Faida lukuki

Stella anasema kuwa ingawa baadhi ya watu wanaipa kisogo tasnia hiyo, lakini ina fursa nyingi ambazo zinaweza kumfanya mtu kubadilisha maisha yake mara moja.

“Mbali na fedha iliyojificha kwenye ufugaji wa samaki, lakini pia kuna fedha iliyojificha kwenye mwani kwani kilo moja ya mwani ni fedha nyingi sana, pia ukija kwenye kilo ya azola bado ni pesa vilevile, jambo la msingi ni kuhakikisha unafanya kazi hii kama inavyotakiwa,” anasema Stella.

Stella Gengi ambaye ni mtaalamu na mbobezi katika eneo la ukuzaji wa viumbe hai kwenye maji chuoni hapo.

Aidha, katika kuhakikisha kuwa SUA kinatoa ujuzi na kuhamasisha watu wengi kuingia kwenye fani hiyo ikiwamo kutayarisha wataalamu, tayari wamejenga matangi maalumu ambayo yanatumika kwa ajili ya kufanyia mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa fani hiyo.

“Katika matangi yetu tunakuwa na aina tatu ya samaki ambao ni kambale, sato, na samaki wa mapambo, pia tangi jingine ni kwa ajili ya mimea ya azola.

“Pia kuna jengo ambalo ndani yake kuna ofisi, maabara ndogo pamoja na sehemu ya kuzalishia vifaranga vya sato kupitia mtambo wetu wa kisasa,” anasema Stella na kuongeza kuwa hawaishii tu kutoa mafunzo bali chuo pia kinafuga samaki hadi kufikia kiwango kinachohitajika na soko.

Hatua kwa hatua uzalishaji vifaranga

Stella anasema ili kuanza kuzalisha vifaranga vya sato kwanza hutafuta wazazi wazuri wa samaki ambao wana uzito wa kutosha kuanzia gramu 250.

“Pia tunatafuta samaki ambao hawana magonjwa na kiafya wako vizuri, hatua ya kwanza tunawatengenisha kwa siku 14 baada ya hapo tunawakutanisha dume kwa jike na tunawaacha kwa siku tano mpaka saba kwani wanakuwa na hamu ya kukutana.

“Kama unavyojua kwamba sato huwa hawaingiliani na samaki wengine hivyo wanakuwa wako pamoja jike anatoa mayai na dume anatoa mbegu na baada ya urutubishaji samaki jike huyaweka mayai hayo mdomoni.

“Hatua inayofuata hapo ni kumpokonya huyo samaki jike mayai ambayo anakuwa ameyaweka mdomoni. Hivyo hatua inaanzia kwenye mabwawa madogo kisha tunayaangalia kwa muda usiopungua siku saba na inategemea mdomoni yamekaa kwa muda gani,” anasema Stella. 

Anafafanua zaidi kuwa hatua inayofuata baada ya hapo ni kuanza kuwapa chakula vifaranga hao.

“Baada ya kuwa ameanza kuwa kifaranga kamili hatua inayofuata nikumhamishia kwenye mabwawa kwa ajili ya kumlea, na hapo itategemea iwapo tunataka samaki jike au dume kwani kama tunavyofahamu kwamba samaki aina ya sato wanapokuwa wadogo wanakuwa na jinsi moja ya kike, hivyo tunachokifanya sisi ni kuweka homoni za kusababisha samaki huyo awe na jinsia ya kiume,” anasema Stella.

Kwa nini wanazalisha samaki dume

Stella anasema kuwa shinikizo la kufanya hivyo kwanza linatokana na mahitaji ya wateja ambao wamekuwa wakihitaji zaidi samaki madume kwa kuwa ukuaji wake ni wa haraka.

“Tunazalisha vifaranga wa samaki dume zaidi sababu watu wengi ambao wanahitaji kufanya ufugaji wenye faida wanahitaji zaidi samaki wanaokua kwa haraka, ndio maana utabaini kuwa mahitaji ya vifaranga wa samaki dume yamekuwa ni makubwa zaidi nasi hatuna budi kufanya hivyo.

“Lakini iwapo itafikia kipindi wakahitajika vifaranga vya samaki jike basi wataalamu wetu watajitahidi kuongeza uzalishaji wake,” anasema Stella.

Akizungumzia ufugaji wa samaki aina ya kambale anasema aina hiyo ya samaki wanawazalisha maabara na kwamba uzalishaji wake huwa na msimu.

“Tunachokifanya sisi pindi tunapotaka kumzalisha maabara kwanza lazima tumchome sindano yenye homoni samaki jike ili akomaze mayai kwani kinyume na hivyo mayai yake yanakuwa hayajakomaa.

“Baada ya mayai kuwa yamekomaa tunamchukua samaki dume tunatoa mayai na kuchanganya na yake ya samaki jike kisha tunaanza kuyaangua,” anasema.

Uzalishaji wa kambale sio mchezo

Stella anasema kuwa uzalishaji wa samaki aina ya kambale ni mgumu na kwamba ndio maana hata bei ya vifaranga vyake iko juu Sh 500 ikilinganishwa na bei ya sato ambao ni Sh 100.

“Kambale ni samaki ambao wanajamii ya mmoja kula mwenzake, hivyo ili kuelipuka hilo unapaswa kuwapa chakula cha kutosha mara kwa mara ili kuzuia yule aliyeanza kula akawa mkubwa kumla mdogo, pia katika kuepusha hilo tunajitahidi kuwaondolea mwanga kwani kukiwa na giza inakuwa siyo rahisi sana kuweza kuonana,” anasema Stella.

Sato wanasoko zaidi

Stella anasema kuwa licha ya kuwa na aina tofauti ya vifaranga vya samaki, wateja wa sato ni wengi zaidi.

“Utafiti wetu mdogo unaonyesha kuwa soko la vifaranga vya sato liko juu ikilinganishwa na aina nyingine ya samaki tulionao,” anasema Stella.

Sio kila bwawa ni lakufugia samaki

Mtaalam Stella anasema kuwa siyo kila bwawa ni la kufugia samaki kwani mengine ni kisima na si bwawa.

“Siyo kila bwawa ni la kufugia samaki mengine ni visima vya maji na ndio maana huwa tunawashauri watu kuwaona wataalamu ili kupata ushauri na maelekezo. “Tunapoongelea bwawa la kufugia samaki lina sifa zake. 

Kwanza lazima liwe na sehemu ya kuingizia maji na kutolea maji. Wengi wamekuwa wakikumbuka sehemu moja tu ya kuingizia maji na sio kutoa jambo ambalo ni changamoto hata wakati wa kuvuna samaki wako.

“Sehemu ya kutolea maji inakusaidia kwamba hata kunapokuwa na mafuriko basi ni rahisi kuondosha maji na kuepusha samaki wako kuondoka, pia kuna shauriwa bwawa lako kuwa na overcontrol ya maji ambayo hii inaweza kusaidia kukabiliana na dhoruba yoyote ya maji na bado samaki wako wakabaki salama.

“Pia kwenye eneo la kina cha maji inatakiwa kuwa na urefu wa mita 1.5. Linapokuwa refu sana kunakuwa na athari kwani inapotokea hata mtu katumbukia inakuwa ni changamoto kumtoa.

“Ukiacha hilo, kisayansi pia inashauriwa kuwa bwawa la mita 1.5 ndio kina kinachopendekezwa hata na wataalamu kwani kimo hicho ndio sahihi kwa viumbe wanaofugwa.

“Sambamba na hilo lazima bwawa lako lifanyiwe urutubishaji wa chakula cha samaki, hivyo hiyo inafanyika kwa kutumia mbolea ya aina yoyote ile na kuweka ndani ya kiroba ambapo baada ya muda maji yanapoingia basi maji yale yanachanganyika na mbolea unayokuwa umeweka kwa kuzingatia ukubwa wa bwawa. 

Mfano kwa mbolea ya samadi unatakiwa kuweka gramu 50 kwa mita moja ya mraba, japo katika hiyo mbolea nzuri ni ile ya kuku kwani anakula vyakula vingi mchanganyiko sambamba na ile ya nguruwe,” anasema Dk. Stella. 

Zipo mbolea za viwandani kama urea na DAP anmbazo pia zinafaa kwa kurutubisha mabwawa.

Anafafanua zaidi kuwa kwa bwawa la mita za mraba 600 wanaweza wakakaa samaki 3,000 kwa wakati mmoja na kuongeza kuwa muda wa uvunaji ni wa kawaida kwa maana ya miezi sita kama ilivyozoeleka.

Aina ya chakula cha samaki

“Katika biashara ya ufugaji samaki gharama kubwa iko katika chakula ambayo huchukua asilimia 60 ya gharama zote za ufugaji. Hapa ndipo wengi wamekuwa wakifanya makosa.

“Ili samaki aweze kukua vizuri anahitaji viwango sahihi vya virutubisho vyote vilivyokamili, swali la kujiuliza kwa mkulima au mfugaji je, samaki wako anapata virutubisho vyote?

“Wengi ukiwauliza wanasema wamemlisha samaki pumba jambo la kujiuliza kwenye pumba kuna virustubisho hivi vyote? lazima mtu atambue kuwa katika kumlisha samaki anapokuwa mdogo anahitaji chakula kiasi gani,” anasema Stella na kuongeza:

“Kwa ukuaji mzuri wa samaki na kupata matokeo mazuri ni bora mtu akanunua chakula cha kiwandani ambacho tayari kimeandaliwa, lakini kutokana na changamoto za gharama unaweza kumuona mtaalamu ili akushauri kiwango sahihi kwa ajili ya samaki wako”.

Kujua kiwango ni muhimu

Stella anasema kuwa ni jambo la muhimu zaidi kwa mkulima au mfugaji kujua samaki wake anakula chakula kiasi gani.

“Lazima ujue samaki wako anakula kiwango gani kwa siku. Mfano kama anakula kilo mbili basi unapaswa kumuwekea kiwango hicho na siyo kusema uweke kilo nne au tano kwa kusema atakula na kesho. Kufanya hivyo unachochea magonjwa kwa samaki na kuongeza uchafu ndani ya bwawa,” anasema na kufafanua kuwa kinachosababisha chakula kuelea ndani ya maji ni kutokana na namna kilivyotengenezwa.

Magonjwa kwa samaki

Anasema pamoja na kwamba siyo jambo la kawaida kuona samaki wanaugua, lakini inatokea kutokana na sababu kadhaa ikiwamo maji kuchafuka na kubeba vimelea vya magonjwa.

“Pili ni kinga ya samaki kushuka kutokana na kukosa utulivu, hivyo kinyume na hivyo basi hawezi kuugua. Na hata inapotokea kuugua ugonjwa wake ni fangasi kwa kiasi kikubwa.

“Ili kujua kuwa samaki wako anafangasi utaona utando mweupe kwenye ngozi yake, na matibabu yake ni pamoja na kupima chumvi gramu tisa ambayo utayachanganya na maji lita moja, kisha unamwagia kwenye bwawa lako.

“Mbinu nyingine la kukabiliana na hali hiyo unaweza pia kubadilisha maji kama nilivyoelezwa huko nyuma, pia unapoona samaki wako anaelea juu basi ujue tayari ana bakteria ambapo unaweza kuitibu kwa iodine,” anasema Stella na kusisitiza kuwa kikubwa ni usafi wa bwawa.

Chuo cha SUA licha ya kuuza mbegu ya vifaranga vya samaki, lakini pia kimekuwa kikitoa elimu ya ufugaji wa viumbe hai kwenye maji bure. Kila mwaka watu mbalimbali wamekuwa wakifika chuoni hapo kwa ajili ya kujifunza.

“Kila mwaka chuo kinatoa mafunzo kwa wakulima na watu mbalimbali bure kuhusu ufugaji wa viumbe hai majini,” anasema.

spot_img

latest articles

explore more

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here