27.2 C
Dar es Salaam
HomeKilimo BiasharaReuben: Nguvu ya parachichi na ujasiri wa kutoogopa deni benki

Reuben: Nguvu ya parachichi na ujasiri wa kutoogopa deni benki

…….Safari ya Patrick Mtitu

REUBEN Mtitu anasema kuwa mwanzo wa safari yake ya uwekezaji kwenye kilimo ilikuwa ni upandaji wa miti ya mbao na kuni. “Nilianza kuvuna miti na fedha niliyokuwa naipata nilikuwa nawekeza huku (kwenye parachichi), sababu nilishawahi kupata majanga mengi sana ya moto.

“…..wakati mwingine ukigombana tu na wananchi wanakwambia ‘tutakuchomea ile miti yako’ hivyo hivyo kwa wafanyakazi, kwa hiyo nikaona kabisa hii ni hatari haya majanga lazima niepukane nayo.

“Ikabidi nijiwekeze zaidi kwenye parachichi kwani huku muda mwingi unalazimika kuweka miti yako safi kwa hiyo hata wao kukuchomea inakuwa ngumu tofauti na miti ya kwaida,” anasema Mtitu.

Mtitu anasema jambo jingine ni kwamba kilimo cha miti kwa ujumla kinamwezesha mkulima kuvuna kila baada ya miaka 15 tangu kupanda, lakini parachichi mavuno yake yanapatikana mapema zaidi.

Mtitu ambaye ameanza kilimo hicho mwaka 2012 anasema uwekezaji wake huo unajumhisha ekari 150 zisizopungua miche 15,000. “Kwa mara ya kwanza nilianza kuvuna mwaka 2015 ambapo nashukuru Mungu kwamba mavuno yangu yamekuwa mazuri tofauti na aina nyingine ya kilimo niliyowahi kuifanya.

“Amani ya zao hili ni kwamba kadri siku zinavyozidi kwenda unaendelea kuvuna faida tu kwani uwekezaji unakuwa umeshaufanya tangu mwanzo, hivyo, mti unakupa kipato kikubwa kadri unavyoendelea kuongezeka,” anasema Mtitu.

Mkopo haunikoseshi usingizi 

“Pamoja na juhudi zangu, pia niliingia Benki ya Lilimo nikachukua mkopo wa Sh milioni 350 ambayo nilitumia kuweka miundombinu ya umwagiliaji shambani kwangu. Nilianza kwa kuweka kwenye ekari 50 hivyo bado 100, pia sehemu ya fedha nilinunua vifaa likiwamo trekta.

“Ni mkopo wa miaka 10 na ninaendelea na mazungumzo kwa ajili ya kukopa tena kwa ajili ya kukamilisha miundombinu ya umwagiliaji kwenye ekari 100 zilizobaki kwani hiyo ndiyo siri ya ushindi na ndio maana pamoja na kuwa na mkopo wa Sh milioni 350, lakini sina wasiwasi, nalala usingizi hadi asubuhi, kwani miti yangu inahitaji huduma tu ili izae zaidi kwa hiyo nikiongeza huduma nitapata mafanikio zaidi,” anasema Mtitu na kuongeza:

REUBEN Mtitu.

“Nilianza kuvuna kidogo, lakini sasa hivi nimefikia hatua ya kuvuna zaidi ya tani 10 kwa mwaka za parachichi.

“Tunashukuru kuona kwamba kwa sasa soko la zao hili limekuwa pana na limekuwa likiongezeka kila kukicha huku sisi tukiwa ni sehemu ya wahamasishaji, hivyo kwa maneno machache naweza kusema kuwa kilimo ndio kimeanza sasa hivi, kwani wengi ndio wanaingia zaidi katika sekta hii,” anasema Mtitu.

Unavyoweza kutajirika na parachichi

Kwa mujibu wa Mtitu bei ya kilo moja ya parachichi mwaka 2021 ilikuwa Sh 1,000, lakini mwanzoni mwa mwaka huu 2022 bei ikafika Sh 2,000 na Aprili mwaka huu imeshuka hadi Sh 1,700.

“Mti mmoja wa parachichi kama umezaa vizuri ambao wastani una umri wa miaka 10 unaweza kukupa zaidi ya kilo 300 kwa msimu mmoja, hivyo iwapo utakuwa na miti 10 basi utakuwa na zaidi ya kilo 3,000”, anasema.

Mtitu anasema safari ya kuwa tajiri kwa kupitia kilimo cha parachichi siyo ya kulala na kuamka, badala yake inahitaji uvumilivu. “Kwa mtu ambaye amefanya uwekezaji mkubwa na wa kisasa basi faida anaweza kuanza kuiona kuanzia miaka mitano hadi sita.

“….chini ya hapo tutakuwa tunadanganyana kwani kwa miaka miwili ndio utaanza kuzaa, lakini haliwezi kukulipa kwa kiwango hicho na wala gharama zako zitakuwa hazijarudi, kwani unaweza kukuta mti umezaa matunda nane tu kama siyo 10 jambo ambalo haliwezi kukunufaisha,” anasema Mtitu.

Kauli hiyo ya Mtitu inaondoa minong’ono ambayo imekuwa ikisambaa kwamba mtu anaweza kutajirika kwa kilimo cha parachichi kwa muda wa miaka miwili pekee.

Pia inaungwa mkono na maelezo ya kitaalamu ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ambayo yanasema parachichi zilizobebeshwa hukomaa baada ya miaka miwili na nusu mpaka mitatu. 

“Vuna kwa wakati, weka kwenye ndoo za plastiki/kreti. Usivune wakati wa mvua/umande kuepuka kuoza. Hakikisha kikonyo kinabaki kwenye tunda,” yanasomeka maelezo ya TARI katika moja ya vipeperushi vyake vya elimu kwa wakulima. 

Gharama za kulima parachichi

Mtitu anasema: “Jambo la muhimu ni kuhakikisha unaupalilia mti wako wa parachichi na kuweka mbolea nzuri ya samadi.

“Mfano mimi nilianza na kidogo kama ekari 20, lakini sasa hivi ninazo 150, ambapo gharama za kutunza shamba kwa mwanzo inaweza kukuchukua hadi Sh milioni 2,” anasema Mtitu.

Aidha, anabainisha kuwa wateja wao wamekuwa wakiwafuata shambani moja kwa moja.

Mtitu anasema kuna wakati anavuna kreti 10 ambazo ni sawa na kilo 20 kwa kreti moja huku kwa msimu uliopita alivuna tani 100 za zao hilo.

“Lakini pamoja na mambo yote juu ya kuweka mbolea na vitu vingine pia kuna changamoto ya palizi ambayo ni muhimu kufyekea miti kila baada ya muda fulani ili kuweka shamba safi.

“Kuna mambo muhimu ambayo tumekuwa tukiyafanya kuhakikisha kuwa shamba linakuwa katika hali nzuri,” anasema Mtitu.

Akifafanya kuhusu mbolea, Mtitu anasema kwa kuwa yeye amekuwa ni mtafiti. Kuna wakati anatumia mbolea ya mabua huku ile ya samadi akilazimika kuifuata Dodoma.

“Kutokana na ukubwa wa shamba langu ambalo ni ekari 150 basi kuna wakati nalazimika kufuata mbolea ya samadi mkoani Dodoma ambayo hadi kuifikisha huku Ludewa inagharimu kama Sh. milioni 2.

“Pamoja na aina hiyo ya mbolea kuna ile ya mabua ambayo niliitafiti nikaona kuwa mabua baada ya kuwa yanachomwa basi inaweza kutumika vema kama mbolea,” anafafanua Mtitu.

Anasema gharama nyingine ni watu wanaomsaidia kuweka mbolea, kufyeka na kuvuna parachichi.

“Mfano kwenye kuvuna kwanza huwa tunawapatia semina kwanza namna ya kufanya kazi yenyewe, utaratibu wetu wa kuvuna tumejiwekea malipo ya Sh 50 kwa kila kilo moja.

“Na hapa huwa nina watu wa aina mbili wa hapa kijijini na wanaotoka mikoa mingine ikiwamo Kigoma ambapo huwa tunawekeana mkataba hata wa miezi 10 ikifika tunafunga hesabu nampa stahiki zake anaondoka,” anasema.

Changamoto ya wataalamu 

Kama ilivyo kwa wakulima wa zao la zabibu mkoani Dodoma wanakolalamikia uhaba wa wataalamu wa zao hilo, upande wa parachichi nako mambo bado si shwari.

Mzee Mtitu anasema kuwa wamekuwa wakishirikishana wao wenywe changamoto zao kupitia vikao vyao huku sehemu ndogo tu ndio wakilazimika kuhitaji wataalamu.

“Muda mwingi tunakaa kwenye vikao vyetu na kushirikishana kwamba majani yamekauka tunafanyaje, kwa hiyo kama kuna namna mwenzio aliwahi kudhibiti anakupa mbinu hiyo na wewe unaijaribu maisha yanasonga, lakini kama itashindikana kabisa basi mnaomba wataalamu wawasaidie,” anasema Mtitu.

Kipo cha kujivunia

Anasema yeye kama mzaliwa wa Ludewa baada ya kuanzisha mradi huo wa parachichi wananchi wamekuwa wakimshukuru kwani amekuwa ni sehemu ya hamasa huku akijivunia mawazo yake.

“Eneo hili halikuwa na miradi mbalimbali ya kuwapatia wananchji kipato cha mara kwa mara, hivyo baada ya mimi kuleta mradi huu wananchi wamenishukuru sana kwani nimewahamasisha kuingia kwenye aina hii ya kilimo kutoka kwenye kilimo cha mahindi ambacho bei zake zimekuwa hazitabiriki.

“Pia hata wanunuzi wangu wamekuwa wakiniambia kuwa natakiwa kuhamasisha wakulima zaidi kulima kilimo cha parachichi ndiyo maana nimekuwa nikigawa miche kwa ajili ya kupanda wanaohamasika wanafanua hivyo na wanaopuuza wanaacha,” anasema Mtitu.

Familia

Mtitu anasema amekuwa akihimiza watoto wake kushiriki kwenye kilimo hicho kutokana na changamoto ya ajira iliyopo nchini.

“Pamoja na kwamba sina mtoto ambaye amesomea masomo ya kilimo, lakini kupitia shamba hili wamejifunza na kuwa walimu kwa wengine na hawatamani tena kuajiriwa,” anasema Mtitu.

Kauli ya bwana shamba mwangalizi

Katika shamba la Mzee Mtitu, yupo kijana aitwaye Frank Lucas Mtweve ambaye ana jukumu la kusimamia usalama wa shamba.

“Ninavyoamka asubuhi kwanza kabisa nawahakiki wafanyakazi wa shambani wako wangapi na afya zao kama ziko salama ili wanapoanza majukumu wayafanye kikamalifu,” anasema Mtweve.

Akiwa bwana shamba na mtaalam wa Kilimo, Mtweve anasema licha ya uzuri wa parachichi na mchango wake kwa wakulima, zao hilo lina changamoto zake.

“Changamoto moja wapo ni magonjwa mbalimbali likiwamo la unyaufu ambao unaosababishwa na ukungu kulingana na jografia tuliyonayo. Ugonjwa huu ukikamata mmea hukauka kuanzia majani hadi mche wenyewe, hili huwa tunalidhibiti na dawa mbalimbali za viwandani. Tunachukua kwenye maduka ya pembejeo kwani kulingana na kukua kwa teknolojia basi kila siku dawa zimekuwa zikibadilika.

“Mbali na unyaufu kuna ugonjwa wa kutokubadilika kwa mmea na hii inasababishwa na kutokuchambua mbegu vizuri wakati wa kupanda, kwa hiyo unaweza kukuta kwamba umepanda mmea shambani ukaupa huduma zote na bado usikupe matunda,” anasema Mtweve.

Kwa mujibu wa TARI parachichi hushambuliwa na magonjwa kama mimea mingine hasa kwa upande wa majani na matunda. “Magonjwa hayo husababishwa na fangasi/ukungu, Algae, wadudu pamoja na lishe duni ya mmea,” yanasomeka maelezo ya TARI katika moja ya machapisho yake.  

Mtweve anasema katika kukabiliana na changamoto hiyo kutokubadilika kwa mmea wanajitahidi kwanza kupata elimu ya mche kutoka kwa mzalishaji wa mbegu.

“Kitaalamu huwa tunaamini kitu kimoja kwamba parachichi inakubali kwenye kipimo udongo ambao ni wastani usio na chumvi nyingi wala acid nyingi ili mavuno yake yawe mazuri,” anasema Mtweve.

Anaongeza kuwa wako wadudu wa chini wanaoshambulia mizizi hivyo matokeo yake unayaona juu kwa matunda kunyauka licha ya kuwapo matunda mengi.

“Ili kudhibiti hili tunatumia njia ya kienyeji kwani mbinu za kisasa wakati mwingine zinaweza zisitusaidie, hivyo huwa tunachukua majembe yetu na kuchimba kuzunguka shina umbali wa mita moja na baada ya hapo tunachukua jivu ambalo ni sehemu ya ‘Acidi’ na kulimwaga ndani ya shimo.  

“Pindi mvua inaponyesha majimaji kutoka kwenye majivu yanaenda kukutana na yule mdudu anashindwa kuhimili anakufa na mti wetu unarejea kwenye hali yake, na kama tatizo litakuwa juu basi tunapruni matawi kisha yanazaa mengine,” anasema Mtweve.

Kuhusu uvunaji, Mtweve anasema licha ya kwamba unaweza kuvuna parachichi, lakini yanaweza kukosa soko kutokana na changamoto ya ulemavu wa mazao au uvunaji.

“Unapovuna parachichi ukaacha kikonyo basi ni nzuri kwani inachelewa kuiva kuliko lile lisilo na kikonyo ambalo linaiva haraka na kuharibika upesi.

“Hivyo, kama mnavyojua kwamba parachichi zetu baada ya kuvunwa huwa zinasafirishwa kwa wakati, hivyo mteja anaponunua ambayo haina kikonyo inakuwa changamoto,” anasema Frank.

Malezo ya kitaalamu yaliyotolewa na TARI yanaelekeza kuwa “Uvunaji wa parachichi zilizobebeshwa hukomaa baada ya miaka miwili na nusu mpaka mitatu…”.

Kwa mujibu wa TARI mambo ya kuzingatia wakati wa kuvuna ni pamoja na kuvuna kwa wakati. “Weka kwenye ndoo za plastiki/kreti. Usivune wakati wa mvua/umande kuepuka kuoza. Hakikisha kikonyo kinabaki kwenye tunda,” inasomeka sehemu ya maelezo hayo na kuongeza:

“Mti bora wa parachichi wenye miaka 4-5 huweza kuzaa matunda 300 – 400 kwa mwaka na mti wenye miaka 7 na kuendelea huzaa matunda 800 hadi 1,000 kwa mwaka”.

spot_img

latest articles

explore more

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here