27.2 C
Dar es Salaam
HomeTahaririAjenda 10/30 ikabadili kilimo cha taifa letu

Ajenda 10/30 ikabadili kilimo cha taifa letu

SERIKALI imezindua ajenda 10/30 inayolenga kukuza kilimo kwa walau asilimia 10 ifikapo mwaka 2030. Mpango huo uliozinduliwa Aprili 04 mwaka huu jijini Dodoma na Rais Samia Suluhu Hassan, ulikwenda sanjari na utoaji wa vifaa vya ugani kwa maafisa ugani nchini kote. Vifaa hivyo vilihusisha takribani pikipiki 7,000, vifaa vya kupima afya ya udongo, simu janja na skana ambavyo vitasaidia wakulima kutambua hali ya udongo shambani kabla ya kupanda mazao.

Hatua hizo ambazo FAMA tunazipigia upatu, tunasema ni juhudi njema za kutaka kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo nchini. Kilimo kwa vyovyote kitakavyoangaliwa ni muhimili mkuu wa uchumi wa taifa letu. Kilimo kinahakikisha Watanzania uhakika wa chakula kwa asilimia 100; mchango kwa pato la taifa kiasi cha asilimia 26.9; ajira kwa nguvu kazi ya taifa kiasi cha asilimia 61.1 na uzalishaji wa mali ghafi ya viwanda nchini kwa wastani wa asilimia 65.

Kama taifa hatuwezi kupanga mpango wowote wa maana wa maendeleo ambao utagusa watu wetu kwa mapana yake kama kilimo kitawekwa kando. Ndio maana sisi tukiwa ni wadau tulioazimia kuwekeza nguvu zetu katika kukuza kilimo kwa kuwa daraja la kuunganisha maarifa, taarifa na kila aina ya nyezo kutoka mdau mmoja kwenda mwingine, tunaona kuwa juhudi hizi za serikali zisitazamwe kwa mazoea tu. Kila mmoja akitimiza wajibu wake kusukuma mbele maendeleo ya kilimo, hakika uchumi wa taifa letu utapiga hatua muhimu na kutokomeza kabisa umasikini.

Katika juhudi za kuleta mapinduzi makubwa ya kilimo, pia wizara imetoa mwongozo muhimu wa uzalishaji wa mazao ambao unazingatia ikolojia ya mazao. Kwa mujibu wa mwongozo huo unaozingatia kanda saba za kijiografia za nchi yetu, kwa maana ya Kaskazini, Mashariki, Kusini, Njanda za Juu Kusini, Kati, Magharibi na Ziwa, zimechambuliwa na wataalam watafiti wa kilimo na kuonyesha kuwa zinaweza kuzaa kanda za ikolojia ya mazao 64. Kwa mujibu wa taarifa za kisayansi za watafiti wa kilimo, ikolojia za mazao zinazingatia hali ya udongo, hali ya hewa na mtawanyiko wa mvua mambo ambayo ndiyo msingi wa kuongeza tija katika kilimo.

Wakati Wizara ya Kilimo ikisukuma kwa nguvu zote mkakati wake wa Ajenda10/30, tunawiwa kukumbushia mambo muhimu ili kwa pamoja taifa letu liondokane na kilimo cha kujikimu. Bado kiwango cha matumizi ya mbinu za kisasa za kilimo kiko chini sana. Mathalani, matumizi ya mbolea kwa hekari yako chini sana, ikikadiriwa kuwa wastani wa kilo nane tu ndizo zinatumika kwa kila hekta kiwango ambacho ni asilimia 10 tu ya kiwango kinachoshauria kimataifa.

Umwagiliaji nao uko chini sana, pamoja na Tanzania kuwa na kiasi cha hekari milioni 29.4 zinazofaa kwa umwagiliaji, ni kiasi kidogo sana cha ardhi hiyo mioundombinu za umwagiliaji kimejengwa, hali inayofanya kilimo chetu kuwa tegemezi zaidi kwa mvua. Hali hii kwa vyovyote haiwezi kuleta mabadiliko kama nguvu kubwa ya uwekezaji wa rasilimali haitaelekezwa kwa kujenga mifumo ya umwagiliaji. Ni rai yetu kuwa sasa Tume ya Uwagiliaji itaimarishwa kwa kuongezewa rasilimali za kufanya kazi ili kujenga mifumo ya uwagiliaji nchini kote.

Katika toleo hili tumezungumza na wakulima wa mazao mengi kama nyanya, zabibu na mazao mengine ya mbogagamboga, kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa takwimu za mazao mengi nchini. Kwa mfano, haijulikani zabibu inayozalishwa nchini ni kiasi gani, hakuna mfumo rasmi wa ufuatiliaji wa zao hilo, mazao ya mbogamboga ambayo ni sekta ndogo ya kilimo inayokuwa kwa kasi kubwa ikikadiriwa kufikia asilimi 11 kwa mwaka, nako hakuna takwimu za maana za kueleweka. Hali hii haiwezi kusaidia kujua mwelekeo halisi wa kilimo chetu na jinsi ya kusaidia kukibadili. 

Hata hivyo, tunaona mwanga mbele ya safari. Hatua ya kugawa vifaa kazi kwa maofisa ugani nchi nzima, tunaziona kama juhudi za kutaka kuondokana na kadhia hii ya kilimo cha kubahatisha. Ndiyo maana tunasema wakati sasa umefika kwa serikali kutambua umuhimu kwa kilimo kwa uzito wake, ni dhahiri kuwa hakuna Mtanzania hata mmoja anaweza kuvusha siku yake ya kuishi bila kupata huduma inayotokana na shughuli ya kilimo. Kwa maana hiyo Ajenda 10/30 iwe mwanzo wa  kutambua umuhimu wa kilimo ili ifikapo mwaka 2030 kilimo chetu kiwe kinakua kwa asilimia 10 hali ambayo itasaidia kupunguza umasikini wa watu wetu kama siyo kuutokomeza kabisa katika taifa hili.

spot_img

latest articles

explore more

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here