26.1 C
Dar es Salaam
HomeMwelekeoProf. Mkenda: Kilimo kitatuvusha tukiongeza tija, ufanisi (ii)

Prof. Mkenda: Kilimo kitatuvusha tukiongeza tija, ufanisi (ii)

Kipaumbele cha nne ni umwagiliaji; tunakwama wakati mwingine kwa sababu tunalima kwa msimu mmoja, hivyo tumeanzisha mfuko wa umwagiliaji ambao watu watakuwa wanachangia ili kuboresha miundombinu ya umwagiliaji na kwenda mbele zaidi kwa kufungua maeneo mapya na mengi zaidi. Lengo letu ni kumwagilia hekta 1,000,000 ifikapo 2025.

Pia kuna suala la masoko, hiki ni kipaumbele cha tano. Ziko changamoto za aina mbili ambazo ni vikwazo vya kuuza na kununua (demand constrains na supply constraints), wakati mkulima analima mazao, lakini hana pa kuuza kutokana na bei imeporomoka. Tatizo lingine ni kwamba soko linahitaji kitu, lakini sisi hatu-supply mfano, tunahitaji mafuta ya kula wote tunatumia na uwezo wa kuzalisha kwenye kilimo chetu tunaweza, lakini hatuzalishi.

“Ziko changamoto za aina mbili ambazo ni vikwazo vya kuuza na kununua (demand constrains na supply constraints).”

Watu tunatumia trilioni ya hela zetu kuagiza kutoka nje. Nusu trilioni tunatoa kuagiza mafuta, hebu fikiria tungezizunguka kwenye uchumi, kwa mfano zikaenda kwenye viwanda, wakalipa wafanyakazi, zikaenda kwa wanaolima alizeti na michikichi. Mfano mwingine ni kwamba watu wengi wanakunywa bia nchini, na kwenye bia kuna kimea kinatumika kinaitwa shayiri, lakini kimea chote kinachotumika katika bia kinatoka nje, lakini mashamba ambayo unaweza kulima ngano au shayiri yapo mengi.

Hata ngano tunaagiza tani 800,000 kwa mwaka kwa aajili ya kutumia na sisi tunazalisha tani 77,000 tu, wataalamu wananiambia tunaweza kuzalisha tani 300,000 au 400,000, huenda hata 500,000 na mahitaji ni mengi. Ukienda yale mashamba yaliyokuwa ya serikali kule West Kilimanjaro utayaona yamekaa hawalimi ngano ya kutosha.

Kipaumbele cha sita ni suala la kupata mitaji kwa ajili ya kuwekeza na kufanyia kazi katika kilimo, ambayo ni changamoto kubwa, fedha za kununulia viatilifu hazipo wakati mwingine kuna watu wanakopa, lakini kurudisha inakuwa ni ngumu sana. Kwa hiyo ni suala kubwa ambalo tunaliwekea mikakati

Mwisho ni Kilimo anga, hii ni kupunguza madhara (risk) kwa sababu tuna kweleakwelea hapa nchini, lakini tulipata nzige hapa majuzi na imetukumbusha tu kwamba unaweza ukapambana sana kulima sana ukijua una uhakika wa kupata chakula na kuongeza tija, lakini wakija wale wadudu wanafuta kila kitu. Sisi hapo zamani tulikuwa na kilimo anga na tuna mpaka maeneo kule Arusha, sasa ni kama kimeachwa. Tulikuwa na bajeti ya kama milioni 500, sasa hivi tumeweka bilioni 3, tunanunua ndege kwa ajili ya kuongeza uwezo wa kupambana na kweleakwelea. Kuna shirika la kupambana na nzige wa jangwani  makao makuu Addis Ababa na lingine la kupambana na nzige wekundu makao makuu yako Lusaka, kwa hiyo ukipata shida mpaka upige simu kuomba msaada kama itatokea shida katika nchi nyingi inakuwa balaa. Wakati wa kupambana na nzige sikutarajia kukaa kule muda mrefu, lakini niliona changamoto

Tulikuwa na bajeti ya kama milioni 500, sasa hivi tumeweka bilioni 3, tunanunua ndege kwa ajili ya kuongeza uwezo wa kupambana na kweleakwelea.

SWALI: Kwa miaka mingi sasa tangu tupate uhuru kilimo cha taifa hii kimekuwa na sura ya kujikimu. Unafikiri nini hasa sababu za hali hii, unafikiri nini kifanyike kuondoa katika mkwamo huu?

PROF. MKENDA: Kumekuwa na utaratibu wa kutofautisha mazao ya chakula na mazao ya biashara, na mazao ya chakula tunayachukulia tunazalisha ili tule tu, ndo maana wakati mwingine kumekuwa na kupiga marufuku mazao ya chakula mtu anataka kuuza nje ananyimwa kuuza. Wakati wa njaa serikali ina haki ya kuchukua hatua kali. Lakini katika mazingira ya kawaida mtu unajiuliza unalima shamba lako la mahindi halafu huruhusiwi kuuza mahindi mabichi, kuchoma unapigwa marufuku maana tuliona kama tuna mazao ya chakula na mazao ya biashara. Na mazao ya chakula kukawa na tabia kwamba ni kwa ajili ya kula tu.

Sasa hivi tunasema mazao yote ni ya biashara, na ni vizuri watu walime kwa ajili ya kupata fedha, kwa hiyo ni chakula chako, lakini unapata fedha kwa ajili ya kujiendeleza. Kwa maana hiyo sasa mahindi, maharagwe, mbaazi, korosho ni mazao ya biashara. Huu ndo mwelekeo mkubwa ambao tunauchukua sasa hivi. Tunasema hiyo biashara lazima iwe ushindani, na ushindani kwenye masoko ni ubora na wingi. Na wingi wenyewe iwe ni gharama ndogo, kwa hiyo hapo ni ubora na bei kwamba unalima kitu kizuri na uuze kwa bei ndogo, na ili uuze bei ndogo lazima uwe na tija kubwa.

Nizungumzie tena tija kitu kimoja mbacho sijui kama watu watanielewa. Ni kwamba mazao yote tunayotumia ndani ya nchi bei yake ishuke. Na ishuke sana, lakini wakulima wote wanaolima mazao hayo kipato chao kipande, kipande sana. Unawezaje kufanya hivyo? Ni kwamba lazima wazalishe kwa wingi zaidi katika eneo moja, kiasi kwamba kama unaongeza uzalishaji mara kumi, bei ikishuka mara sita bado kipato chake kinaongezeka. Lakini bei inaposhuka, maja kwa moja bei ya chakula inashuka, na mishahara ya wafanyakazi nayo inaongezeka.

Sasa hivi kama asilimia 50 ya watu wa kawaida kipato chao kinatumika katika chakula, lakini kama bei ya kile unachonunua ikishuka mara mbili, inamaana utajikuta unatumia robo tu ya kipato chako kweye chakula na umekwisha kushiba. Unakuwa unapata hela nyingi zaidi za kufanya shughuli nyingine. Kwa hiyo kipato halisi (Real Wage) chetu kinategemea sana bei ya chakula. Hata maendeleo ya viwanda yanategemea kupata mali ghafi katika bei ambayo inawafanya waweze kuwa washindani wazuri. Na ili waweze kupata mali ghafi kwa bei ndogo inabidi uzalishaji uwe na tija kubwa. Pamba kwa mfano kama tunaweza kuongeza mara nne uzalishaji kama ambavyo tuna-target, ina maana hata bei ingepungua mara mbili bado kipato halisi cha mkulima kitaongezeka. Atakayetaka kuweka kiwanda cha nguo atagundua kwamba ndiyo napata pamba, lakini bei yake ni ndogo. Hivyo naweza kushindana na wale wanaotumia pamba kutoka Afrika Magharibi.

Sisi tunakwenda kwa mtizamo kuwa kila zao ni la biashara kwa sababu uzoefu ndiyo inafundisha zaidi. Sasa hivi ukisikiliza sehemu zote utasikia bei ya mahindi imeshuka, serikali inafanya nini, wakati tukichukulia mahindi kama zao la chakula usingesikia watu wakipiga kelele kwamba serikali inafanya nini kututafutia masoko ya mahindi. Zamani wakati tunachukulia kwamba mahindi ni zao la chakula usingesikia watu wakipiga kelele, kwa hiyo ukisikia hivyo unajua kwamba huyu mkulima anatambua kwamba hili ni zao la biashara.

Ndizi kwa mfano nayo ni kitu cha ajabu sana kwa sababu bei ya ndizi nayo inashuka sana kule migombani, lakini mjini bei ya ndizi inapanda. Kwa hiyo tunaweza tukalima ndizi kibiashara, ndizi inaweza kuwa biashara ya mabilioni ya dola. Tukiganya ndizi kuwa kilimo cha kibiashara tukaanza kuuza Saudi Arabia, tukaanza kuuza Ulaya nakadhalika. Wale watu wanaokaa katika maeneo ya ndizi hatakwambia tena mambo ya maparachichi. Hata hivyo, ndizi utakula na utauza. Lakini uzalishaji wake lazima uwe wa kisasa sana. Tunaandika mradi wa ndizi kuangalia ambavyo tunaweza tukageuza ndizo kuwa kilimo cha kibiashara, inahitaji mambo mengi. Kuangalia ndizi moja moja kwamba inaanza lini kufungua ua, unavuna lini kiwango kilichovunwa wakati mmoja ndicho kinakusanywa kipelekwe na kisafirishwe na kinachukua muda gani ili kifike kule, maana wezetu kule wanakula zaidi ndizi mbivu zaidi.

unasema hiyo biashara lazima iwe ushindani, na ushindani kwenye masoko ni ubora na wingi. Na wingi wenyewe iwe ni gharama ndogo, kwa hiyo hapo ni ubora na bei kwamba unalima kitu kizuri na uuze kwa bei ndogo, na ili uuze bei ndogo lazima uwe na tija kubwa.

Kwa hiyo asilimia kubwa ya ndizi ambazo zitatengenezwa lazima ziwe ni ndizi mbivu, unauza nje, lakini nyingine zinabaki kwa ajili ya kula nyumbani. Ninachosema ni kwamba dhana hiyo kweli ijengwe kwa wakulima, lakini iende chini kwenye mitaala. Sasa hivi watu wanalima pilipili, ni biashara na wanauza nje na wana mikataba kabisa na wanatengeneza hela nzuri tu. Zamani ilikuwa mtu ana kabustani kako ka pilipili hapo basi, na ikizidi kidogo mtu anapeleka sokoni anauza halafu basi, kakini sasa watu wanalima kama biashara.

SWALI:

Wataalamu wa uchumi wanasema kuwa ili kilimo kiwe na tija ni lazima mambo mawili makubwa yatokee. Moja kufanya kilimo kikubwa cha kisasa (mechanized), mbili kujielekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji. Unafikiri Tanzania ya leo inahitaji miaka minagapi kufikia mapinduzi hayo? Je, tunao utaishi wa kweli wa kisiasa kufika huko?

PROF. MKENDA: Na sio mambo hayo mawili tu, it is not only about mechanization na umwagiliaji tu, lakini pia kuwa na mbegu bora. Kuongeza tija, tunahitaji kupeleka utafiti kwa wakulima, kuweka umwagiliaji pamoja na masoko ambayo yanatoa motisha Zaidi.

watanie unavyotaka, lakini Msukuma ni mchapa kazi, unaona hata ngoma zao wanacheza kwa majembe wakati wengine wanacheza kwa kushikana mikono.

Tunachofanya kwenye pamba sasa hivi, tumefanya utafiti kugundua, moja ukiotesha kwa nafasi (spacing) tofauti, ukitumia mbolea ya samadi au mbolea aina fulani kutoka Minjingu tutaondoka kuzalisha katika ekari moja kilo 200 hadi 250 tutaenda kilo 1,000 mpaka 1,400. Na baada ya kujaribu katika maeneo mbalimbali na kugundua kweli inafanya kazi, Bodi ya Pamba imemchukua aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri kuwa balozi wa pamba. Anapita vijijini akihamasisha. Kwa nini wamemchukua, kwa sababu alionekana akihamasisha kilimo hicho vizuri mno akiwa Tabora.

Kwa hiyo kampeni inafanyika sasa hivi na nilienda kuzindua Busega maana msimu wa kuotesha ulikuwa bado, ni muda mzuri wa kuwaandaa wakulima. Wasukuma ni watu wanaochapa kazi, watanie unavyotaka, lakini Msukuma ni mchapa kazi, unaona hata ngoma zao wanacheza kwa majembe wakati wengine wanacheza kwa kushikana mikono. Sasa hiyo kampeni inafanyika na kwa kuonyesha kwamba kuna utashi wa kisiasa nilienda kuzindua hiyo kapeni Busega (Mkoani Simiyu), it is going very well. Na kama tukifanikiwa kilimo cha pamba mwaka huu huenda tukawa na mavuno bora na tukiendelea vizuri tutafika mbali zaidi kwenye pamba na tutakuwa tumegusa watu wengi. Hapo unaweza ukamwambia mtu kwamba tuko uchumi wa kati maana mifuko yao itakuwa imeguswa, kwa sababu uchumi wa kati unasikiliziwa kwenye mifuko na siyo kwenye mdomo na microphone.

spot_img

latest articles

explore more

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here