27.2 C
Dar es Salaam
HomeMahojianoPinda atoboa ya moyoni hisia zake kwa kilimo (i)

Pinda atoboa ya moyoni hisia zake kwa kilimo (i)

Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda, anafanya mahojiano na waandishi wetu, Jesse Kwayu na Nelille Meena, juu ya ndoto yake katika kilimo. Anatoboa chimbuko la kukipenda na kukienzi kilimo. Makala haya yanakuletea kwa undani alikoanzia, alipo na na nini matamanio yake katika sekta hii. Soma kwa undani…

SWALI: Mheshimiwa Pinda tunaomba utueleze katika maisha yako ya kustaafu ni kwa nini hasa umeamua kuelekeza maisha yako katika kilimo?

“Nadhani ile background yaani ya malezi na makuzi yangu ya mwanzo ndiyo yaliniingiza na kuzama katika kilimo pengine kuliko jambo jingine.”

JIBU: Kwanza nianze kwa kuwashukuru kwa kutenga muda kuja kunitembelea tangu nimestaafu serikalini. Ninaweza kusema mmefanya jambo zuri la kiuungwana. Lakini hili la kilimo ni mada ambayo ni pana sana. Kwa upande wangu ninachoweza kusema ni kwamba inatokana na historia yangu. Mimi nimezaliwa katika familia ya kawaida kabisa. Ingawa baba alikuwa Mwalimu wa dini, yaani Katekista, lakini ukatekista haukuwa chanzo cha mapato cha kuweza kuishi. Hapana. Kwa hiyo muda mwingi aliutumiwa kwenye kulima. Sasa mimi ni mtoto wa kwanza katika familia ya Marehemu Mzee Pinda. Kama ilivyo kwa mtoto wa kwanza mara nyingi unakuwa ndiyo wasaidizi wa kwanza katika familia.

Sasa nilipokuwa nimekuakua kidogo ikiwa wanaposema wanakwenda shamba, na mimi nikakwenda shamba. Nakwenda shule, lakini Jumamosi ninakwenda shamba. Lakini katika elimu yangu, unajua mimi nimesoma seminari darasa la tano hadi la nane. Sehemu kubwa ya ada yangu ilikuwa inatokana na kilimo. Na kilimo chenyewe ni jitihada za mauzo  ya mahindi haya katika mikoa ya Rukwa na Katavi,  ambako ndiyo zao la msingi. Kulikuwa na changamoto zake nyingi sana.

msimamo wangu na mawazo yangu yote ni kwamba tukiinua kilimo kinaweza kutusaidia kuondoa umasikini wa Watanzania.

Mama Mzazi kwa upande mwingine naye alikuwa ni mjasiliamali mdogo wa aina yake. Kwa sababu alifika mahali akajiongeza akasema anaweza kutengeneza pombe akauza apate hela ya kumsomesha mtoto huyu. Hizi ni pombe za asili iliyotengenezwa kwa kutumia pumba za mahindi.

Sasa ili kuifanya pombe ya pumba iweze kutengenezeka na kunyweka ilikuwa inabidi kutumia kimea cha ulezi. Kwa hiyo mama alikuwa maarufu sana kwa upande huo. Sasa nilivyokuwa mdogo nilikuwa msaidizi wake. Kwa hiyo nimekulia katika mazingira hayo, pamoja na kwamba baadaye nilibahatika nikaingia sekondari nikamaliza, lakini nadhani ile background yaani ya malezi na makuzi yangu ya mwanzo ndiyo yaliniingiza na kuzama katika kilimo pengine kuliko jambo jingine.

Jambo la pili ni muda nilioutumia kufanya kazi na viongozi wa nchi. Pamoja na kwamba nilimaliza chuo kikuu mwaka 1974, mwaka 1975 nikaanza kazi kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama mwanasheria, lakini nilitumikia pale miaka mitatu tu nikawa nimechukuliwa kwenda kutumikia Ikulu katika ofisi binafsi ya Baba wa Taifa kama msaidizi wa Katibu wa Rais. Sasa kuanzia mwaka 1978 ile nimeingia pale Ikulu mpaka nilipokuja kuingia katika siasa mwaka 2000 maisha yangu yote yalikuwa pale Ikulu. Sasa nadhani hili nalo limechangia kwa kiasi kikubwa kwa sababu viongozi kuanzia Mwalimu, baadaye Mzee Mwinyi na baadaye Mzee Mkapa na hata baadaye nilipokuwa nimeingia kwenye siasa utaona kwamba kilimo bado ni sekta ambayo viongozi wote wanaipa nafasi kubwa sana.

Ndiyo maana nilipopata bahati ya kuingia kwenye siasa, nikawa naibu waziri, baadaye waziri wa nchi TAMISEMI kwa hiyo msimamo wangu na mawazo yangu yote ni kwamba tukiinua kilimo kinaweza kutusaidia kuondoa umasikini wa Watanzania. Lakini ni kweli pia kuna mambo mengi inabidi yazingatiwe ili kuweza kuona tunafanyaje. Hatimaye sasa nilipokuja kubahatika kuwa Waziri Mkuu wakati wa awamu ya nne, ndipo sasa yale ambayo nilikuwa kwa muda mrefu nayawaza katika kilimo niliona nimepata fursa ya kuanza kuyatumia.  Ndipo maana hiyo nikiwa na Mheshimiwa Kikwete likaja kuibuka suala la Kilimo Kwanza. Dhana ya Kilimo Kwanza ilikuwa inajaribu kutoa msukumo kwa sekta binafsi kuona ni kwa namna gani nao wanaweza kushiriki katika shughuli za kuendeleza kilimo kwa maslahi mapana ya taifa letu. Sasa ukishakuwa na hali kama hiyo, kweli unapokuja kustaafu unajikuta huna option nyingine. Huna kitu mbadala kichwani mwako. Ndiyo maana nilipokuwa nikiendelea bado serikalini, nikiwa naibu waziri na waziri wa  nchi, wakati ule ule ndiyo nilianza kuwaza kuwa na sehemu ya kilimo kama ya kwenda weekend kupumzika, lakini vile vile kutumia kile kidogo nilichokuwa nakijua katika kuendeleza sekta ya kilimo. Na ndiyo kisa hasa cha kuja kuanza hapa Zuzu au Zinje ambako nilipata kama heka 70 na tukaanza kuzitumia sasa kwa madhumuni ya kilimo.

Kwa hiyo hapa tuna heka 70, lakini 10 ndiyo zabibu, heka kama 30 hivi au 40 tumeziingiza katika kilimo cha miembe na baadaye tukaamua tuongeze mambo mengine kama mabwawa ya samaki ambayo tunayo saba, tuaona tujenge na vitalu nyumba (green houses) ziko kama 12. Baadaye tuaamua kufuga ng’ombe wa maziwa kidogo, kuku, bata, bata mzinga, bata bukini na mabata ya aina nyingine ya asili. Kwa hiyo tukawa tumejiongeza ongeza kwa namna hiyo. Kwa sehemu kubwa ukiangalia kilimo kama mimi unaona kilimo ni mahali kama vile pa kukuliwaza. Umetoka bungeni huko umeulizwa maswali magumu ukipata mwanya huku ukakuta ng’ombe kanona kidogo unasahau mengine. Ni jambo mbadala katika maisha, lakini kwangu mimi lilikuwa na nguvu nyingine ya ziada. Mahali pa kuja kupoza akili baada ya kurupushani za hapa na pale.  Ndiyo maana ukinona sasa mimi ninastarehe zaidi katika mazingira ya shamba kuliko mjini. Mjini naona tabu kidogo. Nikiwa huku nikitembea hata nikiona miti tu basi naridhika sana.

Kwa sehemu kubwa ukiangalia kilimo kama mimi unaona kilimo ni mahali kama vile pa kukuliwaza. Umetoka bungeni huko umeulizwa maswali magumu ukipata mwanya huku ukakuta ng’ombe kanona kidogo unasahau mengine.

SWALI: Mheshimiwa Pinda ulipokuwa madarakani uliamini katika kauli mbiu “Kilimo Kwanza”. Leo hii ukiwa nje ya madaraka bado unaamini kuwa Taifa hili linapaswa kuwa Kilimo Kwanza? Na kama kuna mambo yamebadilika, ni nini hasa?

JIBU: Mimi ni muumini wa dhati kabisa katika hilo. Lakini pengine nisema haraka haraka kwamba mtazamo huo umeimarika zaidi baada ya kupata nafasi ya kuwa kiongozi serikalini. Nilifanya ziara nyingi sana nje ya nchi. Nimekwenda India, nimekwenda Vietnam, nimekwenda China, nimekwenda katika nchi karibu zote zilizokuwa zinaitwa The Big Tigers (Singapore, South Korea, Hong Kong na Taiwan) Nimetembelea zote zile. Nikaona karibu nchi zote zinazoendelea ukisema option ya mbadala wa kilimo ni finyu sana. Tanzania kama sisi hivi ambayo asilimia kubwa karibu 70 hivi wako vijijini, na vijijini maisha yao yanategemea kilimo, sasa wakati huo huo mnakaa kuzungumza namna ya kuondoa umasikini. Sasa unauondoa je umasikini kwa mwanakijiji aliyeko kijijini ambaye tegemeo lake ni kilimo. Ndiyo maana eneo hili naendelea kuliamini kwamba ni eneo muhimu sana.

Ndiyo maana bado naamini safari ya mwelekeo huo bado, itakuja kubadilika badaye, lakini nguvu kubwa naamini inatakiwa kuwekezwa katika sekta ya kilimo.

Ili tuweze kupambana kuondoa umasikini ni lazima sera za nchi kwa kiasi kikubwa ziendelea kuleta mabadiliko ya maisha ya wananchi kule vijijini. Ni kweli serikali zote zimajaribu sana maana kuleta mabadiliko hayo ni pamoja na kuimarisha miundombinu kule vijijini. Hilo halina shaka. Lakini kuondoa umasikini kule ni kuhakikisha tuna huduma nyingine za kijamii kule kama za afya, ili mkulima huyu aweze kufanya vizuri. Sasa ukiangalia tulipokuja na sera hizi kama za kupeleka umeme vijijini, unaona nayo imechangia sana katika kasi ya kuleta mabadiliko.

Ni jambo moja unaliona ni la neema, lakini umeme ule hautolewi bure. Inabidi mkulima huyu atumie fedha kununua ule umeme ili aweze kupata huduma hiyo. Sasa uwezo huo anaupata je? Ndiyo maana nasema utarudi tena kwenye kilimo. Ndiyo maana bado naamini safari ya mwelekeo huo bado, itakuja kubadilika badaye, lakini nguvu kubwa naamini inatakiwa kuwekezwa katika sekta ya kilimo.

Kwa hiyo ukiangalia kuona ni nini mbadala wa kilimo ni finyu sana. Unapokuwa na asilimia kubwa nchi kama Tanzania wako vijijini, hakuna mbadala wa kilimo.

spot_img

latest articles

explore more

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here