*Neema ya kustawi bila umwagiliaji na mvinyo bora
*Wakulima ndo wataalamu, maofisa kilimo
Na Mwandishi wa FAMA
UNAWEZA kusadiki kwamba pamoja na umaarufu mkubwa ambao zao la zabibu limeendelea kujizolea mkoani Dodoma kwa miongo kadhaa sasa, hakuna ofisa ugani aliyebobea katika zao hilo nchini?
Ukweli huu umethibitishwa na Jarida la FAMA kutoka kwa wakulima wenywe wa zabibu, baada ya kuwatembelea mashambani na kujionea juhudi zao ambazo zinawafanya wapenda mvinyo wengi kutabasamu kila wapatapo kinywaji hicho cha heshima.
“Hata wao hatuwalaumu ni kwa sababu tu hawakubobea kwenye zao hili, lakini mazao mengine wako vizuri ila inapokuja hili la zabibu wanakuwa wageni kabisa na hii imesababisha hata wakati fulani watu kuunguza mizabibu kutokana na kutumia pembejeo zisizo sahihi,” anasema Samwel Mombo mbaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Zabibu katika Kata ya Matumburu (CHIWAZAMA).
FAMA kwa nia ya kutaka kufahamu na kujionea juhudi za kukuza kilimo cha zabibu ambalo limekuwa zao la kimkakati nchini, ilifunga safari hadi mkoani Dodoma Mji Mkuu wa Tanzania ambako ndiko kitovu cha zao hilo.
Pamoja na mambo mengine ilipata fursa ya kukutana na wakulima mbalimbali ambao ndio wazalishaji wa zabibu waliobainisha kuwa licha ya umaarufu wa zao hilo, bado hakuna wataalamu kama ilivyo katika mazao mengene ya kimkakati kama korosho na kahawa.
Mombo anasema kuwa kilimo cha zabibu ni kama kilikuwa kigeni hivyo hata maofisa ugani waliopo bado si rahisi kutoa msaada kikamilifu kwa wakulima.
“Ni kweli kwamba maofisa ugani wa kilimo wapo, lakini hawajabobea kwa ajili ya zabibu. Hata yeye ukimuuliza ni kama mnafanana tu kwani na yeye analiona ni zao geni sababu hajafundishwa chuoni na kwamba halipo katika maeneo mengi.
“Kwa hiyo unakuta vyuo vingi havikuwa na mtaala kuhusu zao la zabibu, sasa anakuja ndio ni ofisa kilimo, lakini anajifunza kwako mnakuwa mnasaidiana, wewe ukipata hiki na yeye anabahatisha kile, sasa huwezi kusema huyo ni ofisa kilimo ambaye natarajia nijifunze kwakwe kwa asilimia 100, hapana.
“Hata wao hatuwalaumu ni kwa sababu tu hawakubobea kwenye zao hili, lakini mazao mengine wako vizuri ila linapokuja hili la zabibu na wao wanakuwa wageni,” anasema Mombo.
Naibu Waziri wa Kilimo, Antony Mavunde akizungumza na FAMA anakiri kuwapo kwa upungufu wa wataalamu wa kilimo cha zabibu nchini, lakini anasema suala hilo limewekewa mkakati wa utatuzi katika mwaka wa fedha 2022/23.
Kwa upande wake mkulima mwingine, Justine Kuyaga ambaye ni mwanachama wa kikundi hicho anasema kuwa bado ni mtihani mkubwa kwani hata madawa yenyewe wanayotumia unakutana yemetengenezwa Arusha ambapo hali ya hewa ya Arusha na Dodoma ni tofauti.
“Kwa hiyo unafanya kubahatisha tu kwani hatuna wataalamu kabisa, hata pembejeo zilizopo haziendani na mahitaji yetu watu wa zabibu,” anasema Kuyaga ambaye pia ni Mtunza Hazina wa Chama cha Wakulima wa Zabibu katika Kata ya Matumburu (CHIWAZAMA).
Hatari ya kuunguza mashamba
Kuyaga anabainisha kuwa awali ilikuwa ni changamoto zaidi kwani walifikia hata hatua ya kuunguza mashamba kutokana na kutokuwa na uelewa mzuri wa dawa za kutumia katika zao hilo.
“Kiukweli tumehangaika sana, hasa kipindi tulipokuwa tukianza. Kuna kipindi tuliunguza mashamba kabisa kwani tulikuwa hatujui ni wakati gani maji yakiwa mengi upige dawa gani, ni wakati gani majani yanaposhambuliwa upige dawa gani ama kwa kipimo gani.
“…lakini baadaye tukaja kugundua kwamba dawa za unga zinaboresha majani na kuyafanya yawe kijani zaidi, lakini dawa za maji zinaingia kutibu ugonjwa ambao unatoka kwenye mizizi. Lakini kuna baadhi ya dawa zinaimarisha maua, kwa hiyo kwa namna tulivyokuwa tunabadilishana mawazo ndio tukajua kipi ni kipi.
“Mfano dawa kama ‘Zantu’ ambayo ni dawa ya maji ukipiga zaidi ya CC 20 una hatari ya kuunguza majani, kwa hiyo unamuuliza mwenzako ‘wewe ulipiga ngapi, anakwambia nilipiga CC 15 ukiona haina madhara basi na wewe unapiga hiyo mnakariri hiyo maisha yanaendelea,” anasema Kuyaga.
Anasema kwamba uwepo wa kikundi chao ndio umekuwa msaada mkubwa wa wao kuendelea kuwa salama kwani imekuwa ni rahisi kushirikishana changamoto na kuzitatua kwa wepesi.
Kauli yake inaungwa mkono na Mwenyekiti wa CHIWAZAMA, Samwel Mombo ambaye anasema: “Lengo la kuanzishwa kwa kikundi hiki pamoja na mambo mengine ni kubadilishana mawazo katika kilimo hasa cha zabibu ili kupata ufumbuzi wa changamoto tunazokumbana nazo wakati wa kupruni pamoja, ziwe za magonjwa kama unavyojua kuwa zao hili lipo kila mwaka.
“Hivyo, inarahisha hata anapokuja mtaalamu akatoa elimu basi inasaidia kutatua changamoto husika kwa pamoja na kwa haraka.
“Pia lengo jingine ni kuhakikisha kuwa tunashauriana kwenye masoko kwani miaka ya karibuni wamejitokeza wasindikaji wengi ambao ni lazima tuhakikishe kuwa tunaweka utaratibu mzuri wa kufanya nao kazi. Ukiacha hilo faida nyingine imeturahisishia kupata uwezeshwaji kwenye taasisi mbalimbali za kifedha ikiwamo benki,” anasema Mombo.
Maandalizi ndio utajiri
Mkulima mwingine ambaye pia anajulikana kwa jina la Julius Mombo anabainisha kuwa ili mkulima wa zao hilo aweze kunufaika zaidi basi anapaswa kuwekeza nguvu na muda kwenye maandalizi kwani kinyume cha hapo atakachovuna huenda ikawa tofauti na matarajio yake.
“Kwa wastani na kitaalamu ekari moja ya zabibu mtu anatakiwa kuvuna tani tano hadi nane ikiwezekana, lakini inategemea zabibu zako umezitunza vipi, zimezaa vipi. Zikizaa vizuri unaweza kufikisha zaidi ya tani tano, lakini hii yote inategemeana na maandalizi yako wakati wa hatua za mwanzo,” anasema Julius.
Anasema katika kijiji hicho wakulima wanalima mazao mbalimbali ikiwamo mahindi, mtama na mazao mengine, lakini hata hivyo wengi wanalima zao la biashara ambalo ni zabibu.
Aidha, Julius anasema kuwa palizi katika shamba la zabibu ni muhimu sana kwani zao hilo halihitaji misukosuko yoyote na wakati mwingine palizi huenda hadi mara tatu kwa msimu mmoja kutegemea na msimu wa mvua.
“Yaani mvua ikiwa imenyesha vizuri palizi huwa ni mara tatu hadi mara nne, lakini ikizidi basi palizi inaongezeka, kwa kifupi zao hili linahitaji mvua ya katikati kwani ikizidi mazao mengi yataungua.
“Mfano msimu wa kiangazi naweza kuvuna tani tano au sita, lakini kipindi cha mvua shamba hilohilo naweza kukuta hata nusu tani nisifike hivyo kwa maneno mafupi naweza kusema kuwa kiangazi ndio neema,” anasema Julius.
Kwa mujibu wa wataalamu wa zao la zabibu mtu anapohitaji kuwekeza katika kilimo hicho kwanza anapaswa kujiandaa kikamilifu iwapo atalima kisasa.
Soko ni uhakika
Mwenyekiti wa CHIWAZAMA, Samwel Mombo, anasema kutokana na kuwapo kwa masoko kadha wa kadha, wao katika kikundi chao wameingia mkataba na kiwanda cha Aliko Vintage na kwamba hakuna usumbufu wowote kwani wamekuwa wakipata fedha yao miezi miwili tu baada ya kuwasilisha zabibu yao kiwandani.
“Katika hili la soko wala halina usumbufu kwani huwa tunapeleka kiwandani moja kwa moja kwa bei ambayo tumeiridhia, awali tulianza na bei ya Sh. 1,200, lakini kwa sasa tumefika Sh 1,300 kwa kilo moja, hivyo inategemea na msimu, lakini haiwezi kushuka hapo.
“Tumefanya hivyo ili kuwa na mtu wa uhakika jambo ambalo limekuwa halitupi usumbufu mavuno yanapokuwa yameiva basi tunapeleka kiwandani na kupata malipo yetu kwa wakati,” anasema Mombo.
Mkulima marufuku kukata tamaa
Mombo anasema kuwa ni dhambi kwa mkulima hasa wa zabibu kukata tamaa kwani zao hilo linakwenda kuwa la kimkakati.
“Kwa wakulima wa zao letu nawasihi wasikate tamaa kwani tayari Serikali imetutangazia kuwa zabibu linakwenda kuwa zao la kimkakati.
“Hii ni sawa na kusema kwamba baadaye kutakuwa na wigo mpana kwa maana ya kuwa na bodi ya zabibu, bei elekezi na mambo mengine, hivyo tunaamini kuwa tutakwenda vizuri,” anasema Mombo.
Chakujivunia kipo?
“Kwa kweli tunashukuru kwamba katika tasnia hii ya kilimo cha zabibu yapo mengi ya kujivunia kwani kwa sasa tunaona wakulima wakipiga hatua kubwa kimaisha.
“Mfano kwenye kikundi chetu kwa sasa watu wanajenga nyumba nzuri na za kisasa, wamenunua usafiri wa kutembelea, wanasomesha watoto wao vyuo vikuu bila wasiwasi wowote, hivyo ni kupitia zabibu hizi ndio makubwa yote haya yanafanyika hapa Dodoma,” anasema Mwenyekiti Mombo.
Anafafanua zaidi kuwa mafanikio hayo yote pia yamekuwa yakichangiwa na imani ambayo kwa sasa baadhi ya benki zikiwamo NMB na CRDB zimeanza kuwa na imani na wakulima wa zabibu.
“Ngoja nikupe mfano, mwaka juzi tulianza na benki ya NMB ambapo hata wao walikuwa hawaamini kuwa wakimkopesha mkulima wa zabibu ataweza kurejesha hela yao kwani walichukulia zabibu ni kama mtu anayelima mahindi kwamba jua likiwa kali yatanyauka, kumbe sisi tunaona kuwa na mvua kidogo ndio neema.
“Kwa hiyo mwaka wa kwanza mfano kwenye kundi langu tulikopa Sh. milioni 100 tukarudisha vizuri kwa sababu tulikuwa tumeimarisha tuliyoyataka. Mwaka uliofuata tukakopa Sh. milioni 80 nazo tukarudisha vizuri, mwaka huu tumekopa CRDB Sh. milioni 200 ambazo pia tunategemea tutazirudisha vizuri tu,” anasema Mombo.
Fedha ya mkopo inakwenda wapi?
Mombo anasema mbali na mambo mengine fedha wanayokopa inakuwa inawasaidia kununua miti kwa ajili ya kusaidia kuimarisha miche ya zabibu ili iweze kuzaa vizuri. Mti mmoja unauzwa hadi Sh. 2,000.
“Mbali na kununua miti hiyo pia tunatumia fedha hiyo kununua dawa za kutosha ili kunapokuwa na mabadiliko yoyote ya hali ya hewa basi iwe rahisi kukabialiana nayo na fedha nyingine unaweka kwa ajili ya watu kukusaidia kulima pale utakapohitajika kufanya hivyo.
“Katika mikopo hii mfano kama mtu anazalisha Sh. milioni 20 kwenye shamba lake, basi anaruhusiwa kukopa Sh. milioni tano hii inakuwa na faida kwake kurejesha mkopo na kubaki na fedha nzuri yakufanya maendeleo na maandalizi mwengine kwa ajili ya msimu unaofuata,” anasema mwenyekiti huyo.
Wizara ina watu sahihi
Anasema wanaamini kuwa sekta ya kilimo inaongozwa na watu sahihi ambao kwa kiwango kikubwa wana nia ya dhati ya kutaka kuona kilimo kikistawi nchini Tanzania.
“Ukiangalia Mbunge wetu hapa (Dodoma mjini), Anthony Mavunde mbali na kuwa Naibu Waziri wa Kilimo, lakini ni mtu ambaye ana hamasa kubwa na fani hiyo, hivyo tuna uhakika kabisa kwamba changamoto zetu zitafanyiwa kazi.
“Kama hiyo haitoshi, Waziri mwenyewe wa Kilimo, Hussein Bashe anaonekana ana utashi sana na mambo ya kilimo kwa hiyo tunaamini kwamba hiyo sekta baada ya muda watatusaidia na itachanua zaidi, ikumbukwe kuwa tayari Bashe alishafika hapa wakati huo akiwa Naibu Waziri wa Kilimo ambapo alikuja pamoja na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
“Hivyo, kwetu wakulima wizara hii tunaona kabisa kwamba wameipatia jambo la muhimu ni kusubiri matokeo,” anasema Mombo.
Hiyo inamaanisha kwamba wakulima hao wa zabibu kutoka mkoani Dodoma hawana shaka na utendaji wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Serikali na zao mkakati
Mei 15, mwaka huu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa wakati akizindua filamu ya Royal Tour alisisitiza mkoa wa Dodoma kuhakikisha kuwa unalinda kwa nguvu zote zao la zabibu kwa kuwa ndio kivutio na kielelezo cha mkoa huo.
Mombo anasema kuwa tayari walishapata fursa ya kukutana na Waziri Mkuu ambaye alishatembelea kwenye mashamba hayo na kuahidi kusimamia kikamilifu kilimo cha zabibu.
“Jambo la kwanza kama Serikali iliamua kuliweka hili zao la mkakati na siyo hivyo tu kwani alishafika hapa Waziri Mkuu tukamueleza changamoto zetu ambapo binafsi nasema kwa dhati kuwa ni kiongozi anayeishi kauli zake kwani yeye ndio sababu ya sisi kupata mikopo kirahisi kutoka katika taasisi za fedha.
“Ni imani yetu kwamba serikali itaendelea kututazama kwa jicho la karibu licha ya kwamba tayari jitihada zimeanza kuonekana,” anasema Mombo huku akisisitiza kuwa Watanzania nao wana wajibu wa kuwaunga mkono kwa kunywa wine ya zabibu inayozalishwa Dodoma.
Kadhalika akichangia hotuba ya bajeti ya wizara yake bungeni, Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde alisema serikali imejipanga kuendelea kuhamasisha wakulima wa zabibu kulima kwa tija na mwisho wa siku zao hili liwaletee mafanikio wakulima.
Anataja hatua zinazochukuliwa na serikali kuwa ni kukamilisha uanzishwaji wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Zabibu ili kuwawezesha kuwa na sauti moja. Pia kuratibu uanzishwaji wa viwanda vitatu vikubwa vya uchakataji na uhifadhi wa mchuzi wa zabibu ili wakulima waache kuuza zabibu badala yake wauze mchuzi wa zabibu na uwaletee tija kwenye kilimo chao.
“Tumeongeza utafiti kwenye eneo hilo la zabibu na hivi sana ndugu zetu wa pale TARI (Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania) Makutupora wametuongezea mbegu zingine, tunataka wakulima wetu pia waanze kuuza zabibu za mezani,” anasema Mavunde na kuongeza:
“Hivi sasa tumeshagundua mbegu ya Ruby Seedless ambayo itakuwa ni zabibu za mezani. Lakini vile vile na zabibu za viungo kwa maana reisin, hizi zote zitafanyika katika kukuza zao letu hili zabibu.”