28.5 C
Dar es Salaam
HomeMahojianoMAHOJIANO MAALUM NA WAZIRI WA KILIMO, HUSSEIN BASHE

MAHOJIANO MAALUM NA WAZIRI WA KILIMO, HUSSEIN BASHE

BASHE:
Tuna ndoto kubwa, tutakigeuza kilimo cha Tanzania

Jesse Kwayu na Neville Meena

SWALI: Wakati mmefanya uzinduzi na ugawaji wa vifaa kwa maofisa ugani ulisema kwamba kuna ardhi inayofaa kwa umwagiliaji kama hekta milioni 29 hivi. Mipango ni ipi katika eneo hili?

BASHE: Kwanza kwa muda mrefu sisi kama nchi tumekuwa tukisema kuwa tuna ardhi inayofaa kwa umwagiliaji (potential) kama hekta milioni 29. Lakini ukweli ni kwamba hatuwezi kula potential. Kwa hiyo ni lazima ardhi hiyo sasa igeuzwe ili izalishe. La pili, tunakwenda kubadili muundo wa Tume ya Umwagiliaji. Skimu za umwagiliaji ziko wilayani.

Tunakwenda kuwa na mfumo wa Tume ya Umwagiliaji ambao unakwenda kuwa na ofisi katika kila wilaya ya uzalishaji katika nchi. Kuwe na wahandisi wa umwagiliaji katika kila wilaya ya uzalishaji katika nchi yetu.

Cha pili tunachokwenda kufanya ni kuzitambua hivi hizi hekta milioni 29 ziko wapi? Ziko kwenye mkaratasi tu au ziko Nzega au sehemu gani hasa katika uhalisia wake. Au zilishageuzwa kuwa ni eneo la makazi? Kwa kufanya hivyo tutakuwa na ramani halisi za ziliko hizo hekta milioni 29, kwa kila wilaya kila kata na kila kijiji. Utambuzi huo wa kina utatupa fursa ya kubuni na kupanga ni aina gani ya tekinolojia inafaa kwenye kila eneo la umwagiliaji.

Hali hii itatusaidia kutambua katika utekelezaji wa umwagiliaji tutalima mazao gani, ili tunapokwenda kwenye kila ya bajeti ya mwaka unaofuata tuwe na uwezo wa kusema tunakwenda kujenga hekta milioni nne, au milioni moja au laki tano, tuwe tumeshakuwa na uelewa wa kina wa kila eneo. Hali hii itatupunguzia kupoteza muda katika utekelezaji wa miradi ambao huanza na upembuzi yakinifu.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.

Jingine ni kwamba miradi mingi ya umwagiliaji imekuwa ghali sana kwa namna inavyobuniwa. Yaani mradi unaanza kubuniwa ofisini kwenye meza. Unakuta wanasema tunakwenda kuangalia hili eneo wakulima wanalima nini. Kwanza wako tayari toka nchi inaanza, kama ni mpunga wanalima na upo, kwa hiyo hapa kuna kupoteza muda. Sasa tunatengeneza ramani za aina ya udongo na tunaendelea kufanya. Hatutaki wakati tunatekeleza mradi aje mtu wa tathimini ya madhara ya mazingira aseme anataka kufanya kazi hiyo.

Tunataka kukamilisha kazi hizo zote za kutathimini hali ya udongo, mazingira na kila kitu halafu tunakuwa na taarifa kamili, wakati tukisubiri utekelezaji wa miradi hii. Kanzi data hizo zitatusaidia kujua ni mradi upi utekelezwe wapi kwa ukubwa upi. Na matayarisho haya ya kuwa na ramani hizo ndiyo inafanyika sasa hivi. Tunataka ifikapo mwakani tujue hizi hekta milioni 29 ziko wapi na zitazalisha mazao gani.

Pia tunakijengea uwezo kitengo cha ubunifu ndani ya wizara. Unajua mwisho wa siku tunawaambia watu wakafanye upembuzi yakinifu, ina majina mazuri mazuri sujui nini na nini, tunatumia fedha nyingi wakati tuna nguvu kazi ndani ya wizara ambayo ingeweza kufanya kazi hizo. Kwa hiyo, sasa tunakwenda kukiimarisha na kuwapatia nyezo zote muhimu.

Tume ya Umwagiliaji nayo ilikuwa haina vitendea kazi. Tunakwenda kununua magari katika mikoa yote. Tunaanza na mikoa 17. Tutakapokwenda kuanzisha ofizi za Tume ya Umwagiliaji kila wilaya, tutahakikisha kila muhandisi wa umwagiliaji wilayani anakuwa na ofisi na hizi zitakuwa ni ofisi kuu za kilimo katika wilaya. Kutakuwa na mtu wa umwagiliaji, mtu wa kilimo (one stop centre). Na tunakwenda kuwekeana malengo (KPI). Hili ni muhimu kwa sababu hatuwezi kuendelea na hali ile ile ya kawaida.

Mwisho tunataka miradi hii kuwa endelevu. Ni kama wewe baba yako anakuja anakupa duka anakupa na mtaji, duka linakuwa mali yako na mtaji ni mali yako, lakini baada ya mwaka mmoja unamfuata baba na kumwambia pale dukani kitasa kimeharibika. Huu umekuwa ni utamaduni kwenye umwagiliaji. Tumewaambia watu wa Wizara ya Fedha, uwekezaji kwenye umwagiliaji siyo matumizi ya kawaida, ni uwekezaji kama tunavyojenga barabara. Tunapojenga hii miradi ya umwagiliaji ni lazima tufikirie fedha hizi zitarudi vipi, na ndiyo maana tumeweka Mfuko wa Maendeleo ya Umwagiliaji. Mfuko huu upo kisheria.

Kwenye skimu kama pale Dakawa ukienda leo kama unataka kulima kuna mchango unalipa. Kuna mambo ya haki za matumizi ya maji na vitu kama hivyo, ni nani hasa anachukua fedha hizo? Kwa hiyo tunachokwenda kufanya kila mahali serikali inawekeza katika mairadi hii ya umwagiliaji, asilimia tano ya pato ghafi inakwenda kuchangia kwenye huu Mfuko wa Maendeleo ya Uwagiliaji.

Kama kuna fedha za umma zimetumika kujenga miradi hii ya maji ni lazima zirudi kama zinavyorudi kwenye ujenzi wa barabara. Kuna kurejesha fedha moja kwa moja au kwa mzunguko kama kupitia tozo kwenye mafuta ambazo huchukuliwa na kuendelea kujenga barabara. Kwa njia hiyo, Mfuko wa Maendeleo Umwagiliaji itachangiwa hivyo ili kuwa na hali endelevu ya kujenga hii miradi.

SWALI: Unafikiri hizo tuzo zinaweza kutosheleza kuendesha huu Mfuko wa Maendeleo ya Umwagiliaji ili uwe endelevu na miradi yake isife?

BASHE: Unajua tumefanya utafiti wetu kwamba kwenye skimu hekta 600,000 tu ambazo serikali imewekeza fedha, tukikusanya tu asilimia tano ya tozo katika pato ghafi la mapato ya skimu hizi, tuna uwezo kukusanya watani wa Sh. Bilioni 40 hadi 50 kwa mwaka. Lakini jingine la umuhimu ni kwamba tukishakuwa na vyanzo endelevu vya mapato, ni rahisi sasa kuzitaka taasisi za fedha zije na kuwaeleza kuwa miradi hii ina uwezo wa kuingiza kiasi hiki cha fedha, na wao sasa wajiunge kwa pamoja kuwekeza kwenye miradi ya umwagiliaji. Taasisi hizi zitawekeza kwa mfumo hata wa kurejesha fedha zao baada ya miaka 10 kwa sababu kuna uhakika wa mapato.

Kwa maana hiyo, baada ya hatua hii pamoja na fedha za bajeti tunakwenda kuzialika taasisi za fedha ili kwa pamoja zishirikiane kujenga miundombinu ya umwagiliaji na baada ya miaka mitano au 10 hivi tuwe tumepiga hatua kubwa katika kujenga uwezo mkubwa wa umwagiliaji.

SWALI: Umezungumzia mfumo wa kuwa na ofisi moja ya kilimo (one stop center) itakayokuwa na maofisa ugani, wahandisi wa umwagiliaji na wote wanaohusiana na kilimo katika ngazi ya wilaya; unendeshaji wake kimfumo utakuwaje wakati kuna wizara mbili; TAMISEMI na wizara ya Kilimo?

BASHE: Kwanza mfumo wetu wa utawala katika nchi una serikali kuu na serikali za mitaa. Kwa muda mrefu toka tumekwenda kwenye ugatuzi wa madaraka (decentralization by Devolution – D by D) miaka ya 90 maofisa kilimo, maofisa ugani, wahandisi wa umwagiliaji wa wilaya wote wamekuwa chini ya serikali za mitaa.

Lakini mahitaji yanatusukuma kuamini kwamba kama leo likitokea tatizo la wakulima kutokupata huduma, au uharibifu wa skimu za umwagiliaji haulizwi mtu wa TAMISEMI, anaulizwa Waziri wa Kilimo. Baada kufanyika tathimini ya kina, tukaingalia Tume ya Umwagiliaji tukaikuta ipo ngazi ya taifa. Lakini skimu za umwagiliaji ziko wilayani. Kwa hiyo tunachokwenda kufanya sasa ni kuhakikisha kuwa Tume ya Umwagiliaji inakuwa na ofisi katika wilaya zote zinazoshughulika na umwagiliaji na ambazo zina hazina ya umwagiliaji. Hii inakwenda kuindoa Tume ngazi ya serikali Kuu na kuipeleka ngazi ya Serikali za Mitaa ili kuwa na udhibiti kamili wa eneo hilo. 

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akifanya mahojiano na Mhariri wa FAMA, Neville Meena.

Lakini pia tutakuwa na mfumo mwingine ulioboreshwa zaidi wa usimamizi kwa maana kwamba Wizara ya Kilimo itatoa ofisi katika ngazi ya wilaya, kupeleka vitendea kazi na tunawawekea malengo ya kazi ya kutekelezwa kwani tunapaswa kuwa na udhibiti wa kila siku wa watendaji hawa ngazi ya wilaya. Ile ofisi ya wilaya itakuwa na mhandisi wa umwagiliaji na ofisa kilimo ambao watawasimamia maofisa umwagiliaji na ugani. Ajira zao zitabaki TAMISEMI, lakini utekelezaji wa majukumu na usimamizi zitaangaliwa na kudhibitiwa na Wizara ya Kilimo.

Mathalan, ikitokea leo kuna viwavivijeshi mahali, ofisa ugani wa kijiji anakwenda kumwandikia barua ofisa kilimo wa wilaya, naye atamwandikia Mkurugenzi wa Halmashauri ambaye ataandika barua kwa Ofisa Mtendaji wa Mkoa ambaye atamwandikia Katibu Mkuu TAMISEMI naye atamwandikia Katibu Mkuu Kilimo. Sasa katika mazingira haya uamuzi hauwezi kufanyika haraka katika mchakato mtefu kama huo.

Kilimo kinahitaji uamuzi wa haraka kukabili janga linalotokea, vinginevyo madhara yake yatakuwa ni makubwa mno. Ndiyo maana tunasema tutakuwa na mfumo ‘hybrid’. Kutakuwa na upungufu, lakini tutakwenda huku tukifanya marekebisho wakati tunajenga mfumo imara zaidi wa utendaji na usimamizi. La muhimu ni lazima tuwepo eneo la uzalishaji ili kumpa mkulima huduma anazostahili.

SWALI: Eneo la kilimo cha mbogamboga linatajwa kuwa linakua kwa kati ya asilimia saba hadi 11 kwa mwaka na changamoto kubwa unayoiona ni jinsi ya kuifadhi mazao ya mbogamboga ili yafike sokoni yakiwa na ubora wake. Umetaja kuwa kuna mpango ya kujenga miundombinu hiyo katika eneo la bandari ya Dar es Salaam, mpango huu umekaaje?

BASHE: Kwanza nirejee kauli yangu ambayo nimekuwa nikiitoa mara kwa mara kwamba kilimo ni biashara.  Sekta ya kilimo ina maeneo mengi. Eneo ambalo linakuwa kwa kasi zaidi ni uzalishaji wa chakula. Hata hivyo, eneo la uzalishaji wa chakula sehemu ya kilimo cha mbogamboga ndiyo inakuwa kwa kasi zaidi. Eneo la mbogamboga linavutia zaidi vijana kuajiriwa. Leo ukienda Instagram hutamkuta mkulima wa tumbaku. Utamkuta wa parachichi, wa matunda nk. Tunatambua kukua kwa kasi kwa uzalishaji wa mbogamboga, na kwa kweli ni mazao ambayo yanaharibika kwa muda mfupi.

Tunakwenda na suluhu mbili kwenye sekta ndogo ya mbogamboga. Moja kusukuma uzalishaji zaidi, lakini pia kusukuma ujenzi miundombinu. Katika bajeti tunakwenda kuibuka na mpango madhubuti wa kuongeza uzalishaji wa parachichi kwa kutoa ruzuku kwenye miche. Sasa hivi mche wa parachichi unauzwa Sh. 6,000. Tunakwenda kuzalisha miche milioni 20 ambayo itasambazwa kwa wakulima. Upanuzi huo utalazimisha sasa kuwe na miundombinu ya hifadhi. Zipo kelele kwamba maparachichi yetu yananunuliwa na Wakenya na kuuzwa Ulaya kama zao la Kenya.

Mimi kama Waziri wa Kilimo siwezi kuwazuia Wakenya kuja kununua parachichi, kwa sababu wanaleta ushindani ambao unasaidia kupandisha bei ya zao hilo. Sasa hivi kilo ya parachichi unauzwa kati ya Sh. 1,500 hadi 2,000. Hii ni bei nzuri. Suluhu ya pili ni ujenzi wa miundombinu. Kwa sasa hatuna miundombinu madhubuti ya kuchambua, kufungasha na kuhifadhi parachichi katika madaraja yake. Kwa hiyo tunakwenda kujenga miundombinu ya pamoja kwa ajili ya kazi hiyo.

Tunakwenda kujenga moja maeneo ya Iringa, nyingine Kilimanjaro na ya tatu Dar es Salaam. Tunaweka Iringa kwa sababu ndiyo ukanda mkubwa zaidi wa uzalishaji katika Nyanda za Juu Kusini, hapa itakuwa ni rahisi kufanya kazi ya kuchambua, kufungasha na kuhifadhi. Dar es Salaam tumezungumza na Mamlaka ya Bandari kuhusu lille eneo lililokuwa la (Export Process Zone Authority – EPZA), watatenga hekari 10 ili kujenga miundombinu ya kilimo.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe(kulia) akifanya mahojiano na Mhariri Mkuu Mtendaji wa FAMA, Jesse Kwayu(kushoto.)

Hapo yatajengwa maghala ya mazao mbalimbali ya kilimo. Yakishajengwa haya tutaweza kujenga ushoroba wa kuingia bandarini kwa ajili ya mazao ya kilimo. Mahali hapo patakuwa ndipo kituo kikuu cha mazao yote ya kilimo, kama ni kodi na kila aina ya taratibu vitafanyika hapo na baadaye kuelekea moja kwa moja kwenye meli bila kuchekeweshwa. Kilimanjaro tutaweka wilaya ya Hai, kwa sababu ya kutumia Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA). Maghala haya pia yanaweza kusaidia kuuza bidhaa zetu kwenda nje ya nchi.

SWALI: Mheshimiwa Waziri kwa miaka mingi kilimo chetu hakivutii vijana. Ni nini mipango ya Wizara kuvutia vijana wengi zaidi katika kilimo hasa?

BASHE: Tumekuwa na kauli nyingi hapa nchini hasa kutoka kwa viongozi tukiwataka vijana wajiajiri. Lakini sidhani kama kuna kijana yeyote ambaye hataki kujiajiri. Sababu za vijana kushindwa kuchangamkia kilimo ni nyingi. Nitataja tano, moja hawana ardhi. Milki ya ardhi kwa vijana ni changamoto kubwa.

Pili, hata kama angepata ardhi hawawezi kupata mikopo ya kugharimia kilimo, tatu soko la mazao ya kilimo ni gumu sana kwao, nne tekinolojia ya kuwasaidia wamudu kilimo ni changamoto kubwa kwao na tano kilimo kimebezwa sana kiasi kwamba wapo watu wanaoamini kujihusisha nacho ni kujifedhehesha na kushindwa kimaisha.

Tumeanzisha mradi unaotwa ‘bulding a better tomorrow’ yaani kujenga kesho yako iliyobora zaidi. Kama wizara tutatoa ardhi kubwa, tutalipa fidia kokote tunakoichukua kama ni ya halmashari au wapi, kisha tunaipima na kupata hati miliki. Tutaisafisha, tunapima afya ya udongo, tutajua mazao gani yanafaa kulimwa na tekinolojia gani inahitajika. Tutawekeza sisi kama Serikali katika gharama zote hizo. Baada ya hapo tunatengeneza bloku na tutawapa vijana waliko palepale kijijini ambao wanajihusisha na kilimo.

Tunawapa vijana hawa hati za kukodishiwa ama ya miaka 33 au 66 ili taasisi za fedha ziweze kuja kuwakopesa. Hapo tutakuwa tumetatua tatizo la vijana kupata ardhi, kupata mikopo ya fedha na la tatu kwa kuwa tunajua nini kinastawi katika eneo husika baada ya kupima afya ya udongo, tutawaunganisha na masoko. Hii ndiyo itasaidia kuwavuta vijana katika kilimo. Ni mpango wa muda mrefu, utahitaji uwekezaji mkubwa, lakini sisi kama wizara tunaanza na fedha zitakazoingia pale mwoshowe zitakuwa ni za mzunguko (revolving funds).

SWALI: Siku ya uzinduzi wa Ajenda 30/10 kuna benki ilitangaza kwamba imeshusha riba kwa mikopo ya kilimo hadi asilimia tisa. Ni kwa kiwango gani Wizara mmnefanya utafiti wa kina wa kujiridhisha (due diligence) kubaini iwapo hakuna gharama nyingine zilizofichika katika mikopo, ili mkulima asije kujikuta amekopa na gharama ni zaidi hizo asilimia zilizotajwa?  

BASHE: Benki ya kwanza kuanza kutoa riba ya asilimia tisa kwa miradi ya kilimo ni Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB). Hawa walianza 2021/2022 kwenye korosho na pamba kama mradi wa majaribio. Katika kuchakata mazao ya kilimo TADB wakawapa vyama vya ushirika mkopo kwa riba ya asilimia tisa tofauti na aslimia 11 za awali. Baadaye akafuata NMB nayo ikafika asilimia 10. CRDB nao wamekuja na asilimia tisa.

Sisi tulikwenda kufanya uchambuzi wa kina ni kwamba kiwango cha riba halisi (effective rate of interest) kwa mwaka wala haifiki asilimia tisa, ni chini yake kwa sababu mazao haya ni ya misimu, na kuna mikopo ya aina nyingi. Kwa mfano mikopo ya uzalishaji ni ya msimu, kwa hiyo ukilipa hiyo riba wala haifiki asilimia tisa kwa mwaka. Kadhalika tumechambua kama wameweka gharama za utawala, gharama za bima na kila aina ya gharama zinazotozwa na benki, sisi tunachokiangalia ni gharama zote za ujumla wake kiwango cha riba kiwe ni tarakimu moja.

SWALI: Matumizi ya mbolea katika kilimo chetu ni ya chini sana na tunaelezwa kwamba tunatumia wastani wa kilo nane tu kwa hekari ikilinaganishwa na kiwango kinachokubalika kimataifa ambacho ni kilo 80 kwa hekari. Azimio la Abuja la Matifa ya Afrika la 2006 katika kukuza kilimo lililenga hadi ifikapo mwaka 2015 tuwe walau tumefikia kilo 50. Tunaondokaje hapa kwenye kilo nane hadi walau 50?

BASHE: Kuna mambo mengi ambayo yanasababisha wakulima wasitumie mbolea. Moja ni kama tamaduni au jadi na lingine ni maarifa. Hili tunapambana nalo. Wizara tunapambana walau tufike matumizi ya kilo 30 hadi 50 kwa hekari tutakuwa pazuri kidogo. Saa hivi tunahamasisha na kutoa elimu juu ya matumizi ya mbolea.

Suala la pili ni gharama za pembejeo, ni kwa kiwango gani wakulima wa nchi hii wanamudu gharama hizi ni jambo nyeti sana. Duniani kote hata kwa mataifa yaliyoendelea yanatoa ruzuku kwenye pembejeo. Huu ni mchezo wa dunia. Ukitoa ruzuku kwa pembejeo maana yake viwanda vitapata malighafi kwa bei nzuri na wakulima watauza mazao yao kwa urahisi zaidi. Matokeo ya utoaji ruzuku ni makubwa kwenye uchumi, mbali ya viwanda kupata malighafi na kuzalisha bidhaa nyingi, pia mfumuko wa bei utakuwa chini kwa sababu bei za wakulima zitakuwa hazipandi mara kwa mara.

Ukweli mmoja uliowazi ni kwamba bei za mbolea ziko juu mno. Utakuwa mwehu au mwendawazimu kama utaziba masikio kuhusu suala la bei ya mbolea. Tunamshukuru sana Rais amekubali ombi letu la Sh. 150 bilioni fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo ambazo tutazitumia kama fedha ya mzunguko. Kuna watu hawatuelewi wanasema unatoaje ruzuku kama fedha ya mzunguko. Nafikiri suala hapa ni jinsi ya kuitengeneza mfumo wake. Tukipata hiyo Sh. 150 bilioni, tutakaa na taasisi ya fedha itakayokubali kufanya kazi na sisi, tutaiweka kama dhamana. Tutakubaliana na kiwango cha amana hata kama ni asilimia tatu au nne au tano hakuna shida.

Tukishakubaliana hivyo na kuweka fedha hapo, tutatangaza makampuni yatakayoshiriki katika ununuzi wa mbolea. Hatutachagua aina ya mazao, kila mbolea itakayoingia katika nchi hii itakuwa na ruzuku. Wakati wa kuingia bandarini pale tutaipiga ruzuku na tutaweka barcode kwenye mbolea yote inayoingia nchini. Wauzaji wote wa mbolea watasajiliwa. Tutataka kuwe na mfumo wa POS (Point of Sale).

Kwa hiyo tunaanza udhibiti kuanzia mbolea inapoingia nchini, inarekodiwa na wakati wa kwenda kuiuza ukiskani (scan) inajulikana kwenye mfumo kwamba imeuzwa. Wale wote wanaoingiza mbolea nchini watakuwa na dhamana (guarantee) ya benki kwamba wakishauza mbolea yao wanakwenda kwenye taasisi za fedha na kupata asilimia 30 ya mauzo ambayo ndiyo ruzuku ya serikali kwenye mbolea. Watakuwa na kitu kama Letter of Credit na baada ya miezi 12 watalipwa fedha yao baada ya kuuza mbolea kila inapofika Juni kila mwaka. Hali ni hiyo hiyo kwa wazalishaji wa mbolea wa ndani.

Tutaweka lebo za mbolea ya ruzuku kupitia kwa wenye viwanda. Kazi yetu kubwa ni kuhakikisha mbolea hii ya ruzuku haitoroshwi kwenda nje ya nchi. Sasa fedha nyingine ya kutunisha mfuko huu tutapata kwenye zile tozo mbalimbali zilizokuwa zinatozwa kwenye mazao, na kila mwaka tutatenga bajeti kwa ajili ya mfuko huo ili kulinda dhamana yetu isiliwe.

SWALI: Wizara inakusudia kuja na mpango wa kongani katika kuratibu maeneo ya mazao kikanda. Suala hili limekaaje maana tumesikia mkisema ni lazima kuwe na mpangilio bora wa ulimaji wa mazao ili kusaidia tija kwa wakulima wetu?

BASHE: Bado utafiti juu ya idadi ya kongani unaendelea.  Hata hivyo, tunaweza kuwa na kongani kati ya tano mpaka saba kulingana na ikolojia. Kuna kongani kutokana na mazao. Na hapa tutaangalia faidi za ushindani kwa kila eneo. Uzuri wa kuwa na kongani unapata faida kubwa zaidi za kiuchumi katika kuzalisha zaidi eneo moja.

Tutapanga maeneo haya kulingana na orodha ya mazao yanayostawi eneo husika, hali hii itasaida serikali kuwekeza katika miundombinu itakayosaidia kupunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima, lakini pia kuongeza tija. Nikupe mfano; fikiria mkulima wa korosho mkoa wa Pwani au Mtwara anaweza kupata bei ya Sh. 3,000 kwa kilo moja, lakini kama amepanda korosho hiyo hiyo Kasulu, Kigoma hawezi kupata bei hiyo. Sababu kubwa ni suala la usafirishaji, uhifadhi na gharama nyingine za kufikisha korosho sokoni. Inawezekana kabisa angelima michikichi katika eneo lake angepata zaidi. Sasa hivi ndivyo vitu tunataka kuangalia ili kufanya vitu hivi vifanye kazi sawasawa. Tunafanya utafiti wa kutosha ili matokeo yake yatusaidie kubadili kilimo chetu.

SWALI: Ardhi yetu ni ile ile haikui. Matumizi ya ardhi ndiyo yanaongezeka kwa mahitaji mbalimbali. Ni nini mpango wa wizara katika kulinda ardhi ya kilimo?

BASHE: Tunatunga sheria ya ardhi ya kilimo. Nchi hii haina sheria ya kilimo. Tunatunga sheria ambayo itatoa mfumo wa kisheria wa kulinda ardhi ya kilimo. Itazungumzia jinsi ya kulinda kilimo kikubwa cha biashara, kilimo cha mikataba, uwezeshaji fedha kwenye kilimo na ruzuku. Hii ni sheria itakayozungumzia kila kitu kuhusu ardhi ya kilimo. Sheria hii itatupa mfumo wa kisheria wa kulinda ardhi ya kilimo. Bila kuwa na sheria hii inawezekana kila mkurugenzi wa wilaya akajenga nyumba kwenye ardhi ya kilimo na inawezekana kama hali ikiachwa hivi kuna siku tutabomoa nyumba ili tulime.

Hussein Bashe- Waziri wa kILIMO.

SWALI: Je, una jambo jingine lolote ungelipenda kulizungumzia kama hatujaligusia?

BASHE: Kama nilivyosema Tanzania tuna ardhi inayofaa kwa kilimo hekari 44 milioni kati ya hizo hekari 29 milioni zinafaa kwa umwagiliaji, lakini ifikapo 2050 dunia itakuwa na idadi ya watu bilioni tisa. Kati ya hao watu bilioni mbili watakuwa Afrika na ifikapo 2030 biashara ya kilimo inatarajiwa kuwa na thamani ya Dola za Marekani trilioni moja. Tanzania kilimo kinakua kwa asilimia tatu. Kwa bahati nzuri Rais Samia ameonyesha kuwa na shauku kubwa na kilimo. Ni lazima tujipange kunufaika na ukuaji huo wa kilimo.

Tumejiwekea lengo la kukuza kilimo kwa asilimia 10 ifikapo 2030. Hii itafanikiwa kama tutaongeza umwagiliaji kwa asilimia 50, wakati sasa ni chini ya asilimia 10 tu katika kilimo chetu chote. Tunataka kusukuma uuzaji wa bidhaa zinazotokana na kilimo zifikie pato la Dola za Marekani bilioni tano kutoka pato la Dola miloni 1.2 kwa sasa.

Mikopo kutoka taasisi za fedha zinazokwenda kwenye uchumi kwa ujumla wake ni kati Sh. Trilioni 19 hadi 20 kwa mwaka, lakini sekta ya kilimo inaambulia chini ya Sh. Trilioni 2 wakati ndiyo imeajiri nguvu kazi kubwa zaidi ya nchi zaidi ya asilimia 65 na mchango wake kwa pato la taifa ni asilimia 26. Ni lazima hali hii ibadilike.

Kila tukitafakari shauku aliyokuwa nayo Mwalimu Nyerere kuhusu kilimo mara baada ya uhuru na chini ya utawala wake wote, kisera na malengo leo miaka karibu 40 tunaona alikuwa sahihi sana wakati ule kama ilivyo sahihi leo. Mwalimu alianzisha vituo vya utafiti vya kilimo na ndivyo bado tunavitumia na tunakwenda kuviimarisha, alianzisha mashamba ya mbegu, ushirika uliokuwa umeunganishwa na wakulima, kila kitu alichofanya Mwalimu wakati ule leo kinasimama kwa umuhimu wa kipekee na sahihi katika kukuza kilimo cha taifa letu.

Rais Ali Hassan Mwinyi alifungua masoko katika kurekebisha uchumi, wakati Rais Benjamin Mkapa alijenga sana taasisi na kuendeleza marekebisho ya uchumi. Wakati wa Rais Jakaya Kikwete alianza kuwekeza katika kilimo na alikuja na suala la Kilimo Kwanza na ndiyo kwa mara ya kwanza ikaanza The Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT) na sasa tunapanua hiyo dhana ya ushoroba za kilimo kwa sababu imethibitisha kuwa na mafanikio makubwa hasa kwenye uwekezaji. Rais John Magufuli aliwekeza sana katika kujenga miundombinu. Barabara, madaraja, akaanzisha taasisi za kusukuma wananchi kupata umeme kama REA, na ujenzi wa barabara vijijini kama TARURA.

Haya yote Rais Samia ameyaona na anayaendeleza, lakini naye amekuja na kitu kinachogusa wengi, anawekeza kwenye kilimo. Ana shauku ya kilimo. Anataka sasa mashamba ya mbegu yawekewe mifumo ya umwagiliaji. Yamefunguliwa mashamba matatu mapya, ameongeza nguvu ya serikali kuwezesha katika utafiti na huduma za ugani. Kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi huduma za ugani inakuwa ndiyo kitovu cha kusukuma mabadiliko na maendeleo ya kilimo. Serikali sasa inasukuma mbele juhudi za kuachana na dhana kwamba kilimo ni shughuli ya kujikimu kwa ajili ya kula tu, na badala yake iwe ni biashara kama biashara nyingine.

Tumeona sasa taasisi za fedha zinatoa mikopo ya kilimo kwenye riba ya tarakimu moja, na niseme kuwa sisi na wenzangu hapa wizarani tunaamini kabisa kwamba tunakwenda kufikia malengo tuliyojiwekea.

spot_img

latest articles

explore more

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here