Na Hamis Dambaya, Kibaha
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kituo cha Kibaha, Mkoani Pwani kimeuanza mwaka wa Fedha 2022/2023 kwa kutekeleza jukumu la kuzalisha aina sita mbegu mpya za miwa ambazo tayari zimeidhinishwa kutumika baada ya kufanyiwa utafiti.
Mbegu hizo ni ambazo zimeidhinishwa hivi karibuni ni pamoja na TARISCA 1, TARISCA 2, N 47, R 570, R 85/1334 na N36 ambazo kwa mujibu watafiti wake zinategemea mvua, hivyo kuwawezesha wakulima wa kawaida kuzitumia katika maeneo yao kwa ajili ya uzalishaji.
Mkuu wa kitengo cha Uzalishaji wa Mbegu cha TARI Kibaha, Catherine Gwandu, anasema Idara yake inaendelea kufanya utafiti wa uzalishaji mbegu ili kuhakikisha kuwa wakulima wa miwa nchini wanatumia mbegu zilizo bora katika uzalishaji wa miwa.
“Mbegu bora za miwa ndio msingi wa uzalishaji hivyo sisi kama watafiti tuna jukumu la kuhakikisha wakulima wetu wanatumia mbegu ambazo zitawasaidia kukabiliana na changamoto hasa za visumbufu na magonjwa kwani kwa kufanya hivyo zao la miwa litakuwa na tija na uzalishaji utaongezeka,” anasema Gwandu.
Ili kuhakikisha kuwa mbegu hizo za miwa zinawafikia wakulima nchini, kitengo cha Uhaulishaji wa Teknolojia na Mahusiano cha TARI Kibaha kitaanza uzalishaji wa mbegu hizo katika mwaka huu wa fedha wa 2022/2023.
Mkuu wa kitengo hicho, Pili Mauya anasema tayari idara yake imejipanga kuhakikisha mbegu hizo zinazalishwa na kufika kwa wakulima kwa wakati ili waanze kuzitumia na kuboresha kilimo chao.
Kwa mujibu wa Mauya mkakati wa mwaka huu wa fedha ni kuimarisha na kuanzisha mashamba ya mbegu bora katika maeneo ya Mtibwa na Kilombero ambapo uzalishaji wa mbegu za miwa utaendelea kufanyika kwa kiwango cha kutosha kwa lengo la kusambazwa kwa wakulima wengi.
“Tunataka kuona wakulima wanazipata mbegu hizi kwa urahisi na ndio maana zipo kwenye mkakati wetu wa uzalishaji na zitazalishwa katika maeneo ambayo wakulima wenyewe kupitia vijiji vyao watayachagua ili kudhihirisha kwamba TARI Kibaha haifanyi tafiti na kuziweka kwenye makabati,” anasema Mauya.
Anasema TARI Kituo cha Kibaha ina dhamira thabiti ya kuboresha uzalishaji wa mbegu za miwa hasa ikizingatiwa kwamba kumekuwa na wateja wengi ambao wamekuwa wakifika kituoni na kutaka kujifunza masuala mbalimbali ya uzalishaji wa zao la miwa nchini.
“Zao la miwa limekuwa na mvuto kwa watu wengi hapa nchini na hii inatokana na ukweli kwamba mahitaji ya viwanda katika matumizi ya miwa yanazidi kuongezeka ndio maana tumekuwa tukipokea makundi ya watu kutoka kanda mbalimbali kutaka kujifunza kuhusu uzalishaji wa miwa” anaongeza Mauya.
Miwa ni moja ya mazao ambayo mbegu zake zitazalishwa kwa kuzingatia viwango vya ubora vilivyowekwa na Wizara ya Kilimo kupitia Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji wa malighafi hiyo inayotumika kuzaliwa sukari nchini.
Mipango ya Wizara
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe katika hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa Fedha 2022/2023 aliweka bayana kuwepo kwa mahitaji makubwa ya mbegu za miwa kutokana na upanuzi wa mashamba na uzalishaji katika viwanda vya sukari vya Kilombero na Mtibwa mkoani Morogoro, pamoja na TPC cha mkoani Kilimanjaro.
Kadhalika Waziri Bashe alieleza kuwapo kwa mipango ya miradi mipya iliyo katika hatua za awali za kumilikishwa ardhi ya uwekezaji wa viwanda vya sukari ni ya kampuni ya Rai Group iliyopo Kasulu (Kigoma) na mradi wa Rufiji (Pwani) wa Kampuni ya Lake Agro Ltd.
Kwa mujibu wa mipango hiyo, uzalishaji wa miwa ya wakulima wadogo wanaozunguka Kiwanda cha Kilombeto unatarajiwa kuongezeka kutoka tani 800,000 hadi 1,700,000, wakati katika Kiwanda cha Kagera, eneo lenye ukubwa wa hekta 13,000 linatarajiwa kulimwa na kupandwa na tayari hekta 5,300 zimelimwa katika shamba jipya la Kitengule.
Kwa upande wa Kiwanda cha Mtibwa, mpango wa kuongeza uzalishaji wa sukari utakwenda sambamba na ulimaji wa shamba la hekta 30,000 katika eneo la Dakawa na tayari hekta 3,500 zimelimwa.
Kwa kuzingatia hatua hizo, ni dhahiri TARI Kibaha inao wajibu wa kuhakikisha inazalisha mbegu za kutosheleza utekelezaji wa mikakati hiyo ambayo kwa ujumla wake inalenga kuongeza uzalishaji wa sukari nchini.
Akizungumzia umuhimu wa uzalishaji wa mbegu bora za miwa kwa wakulima, Mratibu wa zao la Miwa kitaifa, Minza Masunga anasema kipaumbele kikubwa kwa sasa ni kuhakikisha mbegu zinazalishwa na kuwafikia wadau ambao ni wakulima katika maeneo yao, hatua itakayosaidia kuboresha kilimo cha miwa hatimaye kuongeza uzalishaji wa sukari ambao itachangia kupunguza uhaba wa sukari nchini.
Masunga anasema Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, kituo cha Kibaha pamoja na kuanzisha mashamba ya mbegu mapya, pia wataendelea kuyaimarisha mashamba ya zamani ili yawe chachu ya kuzalisha mbegu za kutosha na hivyo kuchochea uzalishaji wa sukari hapa nchini.
“Tuna mashamba ya uzalishaji mbegu na mashamba darasa katika maeneo ya Kilombero, Mtibwa na Kilosa. Katika mwaka huu wa fedha lengo letu ni kuendelea kufanya kazi kwa karibu na wakulima wa miwa katika maeneo hayo ili mbegu zinazozalishwa ziweze kuwafikia hatua ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa wakulima kutumia mbegu bora,” anasema Masunga.
Itaendelea…