Kijiji cha Nyuki ni habari inayovuma nchini kwa kishindo. Ni mahali ambapo nyuki wamethibitisha kuwa chanzo cha utajiri wa kutupa. Soma mahojiano haya kati ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kijiji cha Nyuki,
***** na Waandishi wetu, Neville Meena na Jesse Kwayu, ujue nyuki ni Habari nyingine.
SWALI: Tumezunguka na kuona sehemu ufugaji wa nyuki na uzalishaji wa asali, unaweza kutueleza umefikafikaje hapa, kwamba nini kilichokusukuma mpaka ukafika hapa ulipo leo?
“Ilipofika kwangu mimi niliwambia mimi nataka katika maisha yangu nifuge nyuki.”
JIBU: Mimi niseme tu kwamba hili wazo la ufugaji wa nyuki, kwangu mimi lilianza kama ndogo, ndoto kabisa ile nightmare nikiwa kama na miaka kumi hivi, niliona kwamba katika mto ambao uko hapa ndani (nadhani mmeuona), mimi niliuota kwamba badala ya kupitisha maji, unatiririsha asali. Ilikuwa ni ndoto ya kawaida na kwa kuwa ilikuwa ni ndoto nilipoamka nikapotozea.
Lakini kila nilipokuwa nakua, ndoto hiyo ikawa inanirejea mara kwa mara kichwani mwangu. Wakati fulani nikiwa nasoma masomo ya Biology Chemistry na Physics (PCB) kule Moshi, Kilimanjaro tukiwa tumekaa nje na wenzagu, wakaanza kusema kwamba ‘mimi ndoto yangu ni kwenda kumsaidia baba yangu labda udaktari’ na kila mtu alisema vitu vyake, ilipofika kwangu mimi niliwambia mimi nataka katika maisha yangu nifuge nyuki.
Walicheka sana, wote walicheka sasa mimi nikajiuliza kwamba wapo waliosema baba zao ni madaktari ni matajiri na nini, sasa mimi baba yangu alikuwa mfugaji wa nyuki, lakini mizinga michache kwa ajili ya mahitaji ya nyumbani tu. Kwa hiyo maana yake hapo ndipo nilipoanza kuona kwamba ule ukawa umaarufu wa shuleni nikiwa kidato cha tano wakiniita wewe jamaa wa nyuki.
Sasa nikiangalia baba alinipa pocket money (fedha za matumizi) Shilingi 40,000, halafu mimi nimepata laki mbili na kitu, nikashtuka na kung’amua kwamba kumbe hii ni business!
Sasa nikawa nikija likizo nachukua kama kilo tano (lita kama tano) nakuwa nazo katika sehemu yangu ya kuishi pale shuleni. Sasa ikawa watu wakichukua uji, maana shuleni tulikuwa tunakunywa uji wakwa wanakuja kuomba wanasema aisee asali kidogo, asali kidogo….sasa ikawa ma-dormitory (mabweni) yote tulikuwa nayo kama 54 kwenye shule ya Old Moshi (Moshi Sekondari) mtu akichukua uji ananyosha moja kwa moja kwenye locker (kabati la kutunzia vifaa) langu kuja kuomba asali.
Kwa hiyo kipindi kilichofuata cha likizo nyingine wakaniagiza kabisa kule majumbani maana walikwenda wakawasimulia wazazi wao kwamba kuna mwanafunzi mwenzetu huwa anatulisha asali kule shule. Ikawa kipindi nilipokuwa nakwenda kuanza form six baada ya kumaliza likizo ya form five, nilikwenda na kilo tanotano, zile galoni za lita tanotano zaidi ya kumi na tano (15); nyingine niliziacha Arusha na nyingine niliziacha Moshi kwenye nyumba za wale wazazi wa wanafunzi niliokuwa nasoma nao. Nikapata takriban Shilingi 210,000 hivi maana nilikuwa nikiuza galoni kwa Shilingi 25,000.
Sasa nikiangalia baba alinipa pocket money (fedha za matumizi) Shilingi 40,000, halafu mimi nimepata laki mbili na kitu, nikashtuka na kung’amua kwamba kumbe hii ni business! Sasa pale ndipo ukawa mwanzo kabisa wa kuona kwamba sasa hii ni biashara. Kwa kuwa nilikuwa nasoma masomo yenye uelekeo wa udaktari awali niliwaza kwamba baada ya kuhitimu nikasome masomo ya udaktari na nilikuwa napenda madaktari, lakini nilipofika kidato cha sita nikaamua kuua ile ndoto ya udaktari na kuingia kwenye ufugaji wa nyuki.
Niliporejea nyumbani hapa kwenye Kijiji cha Nyuki sikuwa na eneo nilimuomba baba ekari moja hivyo akanipa. Nikahamisha misinga yake ya asili na kuileta kwenye eneo langu, kwa hiyo passion ya nyuki ikawa imeniingia na hata matokeo yangu ya kuingia chuo kikuu nilichaguliwa kuingia Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA). Actually hata sikusoma hata ile kozi niliyopangiwa, nilikuwa busy na nyuki. Yaani nilikuwa nasoma kozi ambayo haihusiani na nyuki, lakini ukunikuta maktaba nilikuwa nasoma nyuki tu. Watu waliosoma na mimi wanajua kwamba mimi nilikuwa nikienda maktaba na-search mambo ya nyuki tu.
Kutoka pale nilikuwa naamini kwamba hata nikihitimu sitaajiriwa na serikali wala sitaajiriwa na mtu yeyote.
Mimi nilikuwa nasoma Food Science, lakini nilikwenda Forestry nikakutana na mhadhiri alikuwa anaitwa Profesa Temu, akanipa notice za forest, mwaka wa kwanza wiki ya kwanza vile nilivyoingia, ile kozi niliyopangiwa..maana mimi niliomba forest, lakini sikupata kwa sababu ya mipangilio ya TCU (Tume ya Vyuo Vikuu). Kutoka pale nilikuwa naamini kwamba hata nikihitimu sitaajiriwa na serikali wala sitaajiriwa na mtu yeyote. Nikaamua kuwekeza zaidi kwenye nyuki na nikawambia watu kwamba mimi kusoma ni kama part time (kitu cha muda) maana mimi nataka nifanye biashara.
Wakati wanafunzi wenzangu wanasoma ili waje wafanye kazi, mimi nilikuwa nawaona wao ni wateja wa mazao yangu, na hata walimu wa SUA nilikuwa nawaona ni wateja kwa sababu nilianza ku-pack asali nikiwa kule na kuwagawia kwenye nyumba zao.
Hao maprofesa, madaktari, wakawa wateja wangu na mpaka leo ni wateja wangu na wanafunzi ambao walikuwa wanaweza kupata hiyo asali kutoka kwangu. Ilinilazimu nihame kutoka kwenye hosteli za chuo nikaenda kupanga nyumba nje kwa ajili ya kufanya biashara za asali.
Ni kweli ni kama yeye haikumwingia akilini kidogo, akaniambia nenda ukaone jinsi ya kufanya.
Baada ya hapo nikaanza kufanya hiyo biashara na nikakutana na Mzee Pinda (Mizengo, Waziri Mkuu Mstaafu), nikiwa mwaka wa pili hapo chuo kikuu, kwa sababu tu ya passion maana naye alikuwa anasema nyuki sana na mimi nikajaribu kuonana naye. Akani-support mizinga 100 ya kuanzia baada ya kuona nimekuwa vibrant katika hii sekta. Lakini alifuatilia sana maendeleo yangu.
Tulikuwa tunafanya mawasiliano na wakati nahitimu alikuwa ni mtu ambaye ningeweza kumwambia kwamba anisaidie kupata ajira, lakini mimi nilimjulisha kwamba nakwenda kijijini kwetu kwa ajili ya kwenda kuanza kufuga nyuki kibiashara. Ni kweli ni kama yeye haikumwingia akilini kidogo, akaniambia nenda ukaone jinsi ya kufanya. Nilipofanya hivyo nikapata fursa ya kwenda Israel kwenye Chuo Kikuu cha Kilimo cha Jerusalem ambako niliamua kusomea commercial beekeeping.