27.2 C
Dar es Salaam
HomeMahojianoMaajabu ya nyuki: Mdudu mdogo anayezalisha mazao manane ..(ii-3)

Maajabu ya nyuki: Mdudu mdogo anayezalisha mazao manane ..(ii-3)

Shughuli za wafugaji nyuki zilikuwa haziheshimiki sana na ndiyo maana kupitia Kijiji cha Nyuki tutawafungua Watanzania wengine waweze kuona thamani ya ardhi. Na hata mamlaka ya hapa Singida imelitenga hili eneo kwamba ni la hifadhi ya nyuki ya mtu binafsi, sasa mimi nimeendelea na zile hatua kwamba sasa hata wizara wanaweza kuiga jinsi Manispaa ya Singida ilivyofanya kwenye hiki Kijiji cha Nyuki na baadaye hizo sehemu nyingine zikiweza kufanya hivyo, tutakuwa na vijiji vingi vya nyuki. Mlienda kwa Mzee Pinda (Mizengo, Waziri Mkuu Mstaafu) pale, mmeona vitu alivyovifanya, alivyounganisha ufugaji wa nyuki pamoja na mazao mengine, pamoja na kilimo cha mazao ya aina tofauti. Hivi niwaambie, pangekuwa na watu kama wale milioni kumi (10,000,000) ambao wametengeneza establishment za aina hiyo, tungeiita hii Jamhuri ya Muungano Royal State ya Tanzania kama ile ya Emirates, kwa sababu watu wengi watakuwa wakiishi maisha kama ya aina hiyo.

“wizara wanaweza kuiga jinsi Manispaa ya Singida ilivyofanya kwenye hiki Kijiji cha Nyuki.”

Kwa hiyo mimi naona katika masuala ya ardhi hakuna tatizo kubwa, hamna upungufu mkubwa wa ardhi, ni jinsi ya kutumia. Lakini pia kwenye masuala ya watu ni kuendelea kupewa elimu, watu wote. Mimi sasa hivi naazisha kozi, tarehe 16 (Agosti) nitakuwa na kozi Dodoma ya wafanyakazi wa Serikali. Nafundisha mpaka tarehe 11 mwezi Septemba (2021). Mwezi mzima, nitawafundisha wafanyakazi na watumishi wa serikali habari hii-hii kwasababu hata wao wanataka kuja kuwekeza humu (kwenye ufugaji nyuki). Sasa wanawekeza, halafu hawajajua fursa ilivyo. Nataka niwatangazie fursa ilivyo. Mimi nataka nisiwe na roho mbaya katika hili jambo. Watu wajue na halafu wao wanavyojua wao wafanikiwe huko na sitaki malipo.

SWALI: Umezungumzia mafunzo kwa wafanyakazi wa serikali, vipi kwa watu ambao hawako serikalini?

 

JIBU: Sekta binafsi itafuata, ila nimeanza na watu wa serikalini kwa sababu wao wakiweza kulifanya hili, wakiweza kuliona hili sekta binafsi huwa hawana shida. Unajua sekta binafsi huwa ni washambulizi, wale huwa wanashambulia. Lakini fursa ikibanwa sana maanake hawashambulii maana watakamatwa. Ukiwa na ndoo mbili (za asali) unakamatwa njiani, mara lipia kibali, sasa hayo yote yanafanywa kwa sababu aliyekabidhiwa kusimamia hili labda ni askari. Polisi yeye hajui mambo ya misitu, aliyeachiwa lindo naye ndo hivyo hafahamu haya mambo, sasa hayo yote hayo yanaonyesha kutokuelewa.

Bado kuna migongano ndiyo maana juzi katika mapendekezo yetu tulikuwa tunafikiri hata hii sekta ndogo ya nyuki ihame iende Wizara ya Kilimo au iende Mifugo.

Sasa mpaka baadaye unakaa, unawaelewesha kwamba jamani mimi ni mtu nina TIN number kwa hiyo hii ni biashara, siyo maliasili. Kwa jinsi ilivyo, mtu ukibeba asali inaonekana kama umebema nyara za serikali, wakati ni mfugaji na sisi tunafuga nyuki, kama mtu anavyobeba kuku. Bado kuna migongano ndiyo maana juzi katika mapendekezo yetu tulikuwa tunafikiri hata hii sekta ndogo ya nyuki ihame iende Wizara ya Kilimo au iende Mifugo. Kwenye Wizara ya Maliasi (na Utalii) inakaa na wahifadhi.

Inaonekana ni nyara za serikali na katika mazingira hayo haiwezi kukua maana mara geti mara nini asali inakuwa kama madini. Mimi naomba ufugaji wa nyuki ifahamike kwamba ni binadamu ndiye anafuga nyuki. Binadamu anaweka jitihada. Ndiyo maana nimeanza mafunzo haya, watu wakishaelewa tutajadiliana. Nimefanya mafunzo haya siyo kuwaelimisha sana ila kwa sababu wao wenyewe ni wawekezaji. Mfanyakazi wa serikali siyo kwamba yeye siyo mwananchi, yeye pia ana-save income yake. Na mimi wateja wengi niliowapata kwa miaka mitatu iliyopita wanaowekeza ni watu wa serikalini. Wana-save mitaji yao, wanawekeza.

SWALI: Katika moja ya majawabu yako umesema ufugaji wa nyuki unahitaji mtaji mdogo, nini maana yake?

 

JIBU: Ni rahisi sana kufuga nyuki. Ardhi inapatikana tena kwa bei ndogo sana. Kwa mfano hapa kuna baadhi ya maeneo Singida ekari moja inauzwa Shilingi 50,000. Sasa unapata ekari moja kwa Shilingi 50,000 ni uwekezaji mdogo, maana kiwanja mjini kwa ajili ya kujenga hoteli ni kiasi cha 300,000,000 – 400,000,000. Lakini hapa kwa sababu tunafugia nje ya mji, gharama ya ardh inakuwa ndogo. Hiyo ni moja, la pili ni mizinga.

Unanunua mzinga wa kibiashara kwa Shilingi 200,000. Ule mzinga wa laki mbili utavuna kwa miaka hamsini, bila palizi, bila nini yaani wenyewe upo kwa ajili ya biashara. Sasa chukua kwamba kila mwaka mzinga unakupa laki mbili kwa kuvuna asali tu achana na hayo mazao mengine, kwa hiyo ni laki mbili mara hiyo miaka 40 mpaka 50, hauoni kwamba hiyo ni faida kubwa? Mahindi yenyewe wanawekeza kwa nununua mbegu kila mwaka, au kila msimu. Pia hapo kuna kulima, kuna palizi, mbolea.

Mimi nimeanza kufikiri kwamba pengine kuna watu wanapenda kuteseka, kwa sababu unamuonyesha mtu kwamba njia hii unapata hela nyingi, unapata mahitaji yako haraka, yeye bado anang’ang’ania njia ileile ambayo anatumia laki tatu anapata laki moja, kwa kulima mahindi!. Ni kweli, tumefanya majaribio pale kwenye njia ya kwenda Iguguno kuna mtu alikuwa amelima ekari mbili za mahidi, tumemwekea mizinga ya nyuki 50, mizinga imempa zaidi ya Shilingi Milioni mbili, mahindi amepata magunia manne na gunia moja ameuza Shilingi 30,000, ambazo mara nne ni sawa na laki moja na ishirini.

Leo tunazungumza katika mazingira ambayo watu wanaingiza kwenye akaunti milioni 30, milioni 40 kwa wiki, kwa mwezi tena kijijini, eneo ni lile lile.

Palepale alipolima mahindi amepata Sh.2,000,000. Nawashauri hata wakulima wa mahindi, parachichi, wakulima wa miti, ikiwa mtu unaweza kusubiri miti kule Iringa miaka 16, anashindwaje kusubiri asali. Anashindwaje kuwekeza kwenye nyuki ambako anapata kila baada ya mwaka? Na nyuki naye anadumu kwa miaka hiyo…na baadaye atakuja kukata ule mti na kuuza tu. Mimi nafikiri na siyo kwamba napinga biashara ya miti..lakini imefika mahali vijana pamoja na wawekezaji wengine katika nchi ya Tanzania, tuanze kuwa na reasoning capacity.

Tuanze ku-reason baadhi ya vitu kwamba kwa nini tunaishi namna hii, kwa nini tunafanya hiki. Mimi nilikuwa najiuliza hapa kwa nini sisi ni maskini? Actually, mimi nimezaliwa katika familia ambayo hata mia tano kupatikana ilikuwa siyo rahisi. Leo tunazungumza katika mazingira ambayo watu wanaingiza kwenye akaunti milioni 30, milioni 40 kwa wiki, kwa mwezi tena kijijini, eneo ni lile lile. Sijabadilisha uwanja wa mapambano. Uwanja bado ni ule ule. Kilichobadilika ni mawazo tu, jinsi ninavyofikiri. Kama mnavyoona, nyumba yangu (ya kushi) ile pale. Ofisi yangu hii hapa. Viwanda hivi hapa. Duka hili hapa.

Kwanza unajua ukiwa barabarani miaka 50, kila siku uko barabarani hata ajali za barabarani unazishuhudia kila wakati na kila ukipita.

Mimi naamka pale kwangu, nafika hapa (ofisini), situmii hata usafiri, hakuna haja ya gari, hakuna risk (hatari) nyingi. Kwanza unajua ukiwa barabarani miaka 50, kila siku uko barabarani hata ajali za barabarani unazishuhudia kila wakati na kila ukipita. Lakini ukikaa hapa, unatoka labda ukienda kusali Jumamosi au Jumapili na weekend unatoka kwenda kufanya shopping labda sehemu. Lakini pia huku unaweza kuanzisha bustani ndogo ndogo, na ufugaji mdogo wa mbuzi, mayai nini..na ukapata huduma huku huku. Hata katika hili janga la COVID-19 ambalo halitaki watu kukutana mara kwa mara, mimi nikiamua kukaa hapa nafanya vitu vya humu ndani, maana yake naweza kukaa muda mrefu nikiwa safe kwa sababu sina mwingiliano na watu wengi. Niseme tu kwa ujumla kwamba hiyo ndiyo story ya Kijiji cha Nyuki.

spot_img

latest articles

explore more

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here