Mfano mwingine ni zao la chai, Tanzania tunazalisha kilo milioni 37, Malawi wanazalisha kilo milioni 48, hivi hata ukiangalia kwenye ramani ukichukua tu Njombe na Iringa hata kwa kuangalia hali ya kijiografia unaona nini hapo? Na ilani yetu ya chama inasema tufike kilo milioni 60 ifikapo mwaka 2025. Hapo Rwanda wanazalisha kilo 25 milioni na growth ni asilimia kumi kwa mwaka, maana kwamba wanakua na wanaweza kutupika. Uganda wanazalisha kilo milioni 77 na Kenya wanazalisha kilo milioni 500 (hizo data ni subject to verification), na sasa angalia au chukulia hata ramani ya Kenya na sisi tungechukua ukanda wa milima ya Usambara na upande wa Tanga huku si tungeweza kuzalisha kama Kenya hata bila kuongeza maeneo ya Nyanda za Juu Kusini. Kuna fursa kubwa ambayo hatujaitumia na sasa tumeifungua, na tulichojifunza kwenye pamba tunahamishia kwenye chai. Ukienda pale Iringa, pale Kilolo tuna hekta 3,600 za chai zilioteshwa, lakini hamna uvunaji kwa sababu hamna kiwanda. Michai imekuwa mirefuu, tulienda kule tukapiga picha na ni kama tulikuwa porini kabisa.
“Tungechukua ukanda wa milima ya Usambara na upande wa Tanga huku si tungeweza kuzalisha kama Kenya hata bila kuongeza maeneo ya Nyanda za Juu Kusini”
Huwezi kuchuma ile chai ikiwa juu kiasi kile, lazima chai iwe fupi. Wanasema unaweza kui-prune na ikachipua upya. Chai unaweza kuendelea kuvuna kwa miaka hata 50, wewe kazi yako ni kuvuna kila siku. Pale Kilolo wanachohitaji ni kiwanda tu, na ukiweka kiwanda hata wananchi wa jirani wanataka kulima chai. Nilipopata taarifa ya Kilolo kabla sijaenda nilikuwa Njombe, niliongea na Unliver kwamba nakwenda kutembelea kiwanda chao, lakini nataka wajenge kiwanda kingine pale Kilolo. Wakaniambia wewe njoo kiwandani na tutakwambia kwa nini hatuendi Kilolo.Nilipofika pale, wakaniambia uwezo wa kiwanda unatumika kwa asilimia 20 na ikizidi sana ni asilimia 30 sababu ni kwamba hawana chai ya kutosha.
Wakanionyesha mashamba ya chai kwa upeo wa macho yangu wakisema hawawezi kuchuma chai na kuifikisha kiwandani kwa sababu ya ubovu wa barabara. Ukienda Lupembe kilometa 50 kutoka pale, watu wana chai, lakini wanavuna wanatupa. Hawana cha kufanya kiwanda cha pale kinafanya ovyo. Barabara ile inahitaji uwekezaji kidogo ili waweze kufikisha chai kiwandani. Halafu pia kuna watu wamejiunga ukiongea nao wanasema vijana hawapendi sana kuvuna chai kwa sababu ni kazi kubwa kuchuma yale majani kwa udogo wake. Wanawake ndiyo wanafanya kazi. Lakini kuna mashine ambayo ni kama bodaboda, kama vijana wanaendesha bodaboda basi wanaweza kuendesha mashine na wakavuna. Tukifanikiwa tutaongeza uwezo wa kiwanda mara tatu zaidi. Kile kiwanda kiko sehemu inaitwa Kabambe, nimewapeleka TIB wafanye, nimechukua mradi wa agro-connect, waliweka barabara na nimeagiza barabara ijengwe kuunganisha Kabambe na Lupembe, halfu kuunganisha yale mashamba mengine niliyoonyeshwa pale. Hawa jamaa (Uniliver) wakileta kiwanda pale Kilolo kwa hali ilivyo sasa hivi tutaweza kuzalisha kilo milioni 14.5. Sasa kg milioni 37 jumlisha 14 tutakuwa tumefika kilo milioni 50 na kitu. Najaribu kuwaonyesha kwamba kuna mambo madogo ambayo tukiyatatua mambo yatakwenda. Sasa ukiangalia bajeti ya Kenya ni mara mbili ya bajeti ya Tanzania kwamba ukisikia Waziri wa Fedha wa Kenya anasoma bajeti yake, ni mara mbili ya kwetu. Sisi ni trilioni thelathini na ngapi…wao ni sabini na kitu. Kwa nini? Ni kwa sababu tu kilimo chao cha chai kinatuzidi mara ngapi. Chukua kg. milioni 500 gawanya kwa kg milioni 37.
kuna mambo madogo ambayo tukiyatatua mambo yatakwenda.
SWALI:
Unafikiri mfumo wetu wa kutegemea mazao kama kahawa, pamba, tumbaku (traditional cash crops) kama vyanzo vikuu vya kuingiza fedha za kigeni utaivusha nchi hii? Unafikiri mazao mbadala kama mbogamboga na maua yakipewa msukumo yana nafasi gani kuwa chanzo kikuu cha fedha za kigeni nchini?
PROF. MKENDA: Mtu akiwa na kahawa yake akiamua kung’oa ili alime kitu kingine huna uwezo wa kumsukuma kumzuia kwa sababu shamba ni la kwake, soko litaamua. Kwa hiyo kazi yetu sisi kwanza ni kusaidia kuongeza tija, kwenye kahawa watu wanang’oa kwa sababu tija ndogo. Ukiangalia tija ya arabica tunapata nadhani gramu 0.5 au tunaweza kwenda mpaka kilo 1.5 kwa mti kwa mwaka. Kwa hiyo tija inapozidi kuwa ndogo, watu wanaona kwamba zao halilipi. Kwa ndizi ni suala la kufanya kisasa, isipokuwa tutakuwa na changamoto ya mifumo ya kimiundombinu kwa maeneo ya mbali kama Mbeya na Kagera. Kwa sababu hata hawa watu niliowaambia tuandike mradi wa banana nataka waanzie Kagera, sasa wanasema kwamba SGR ikifika huko itakuwa ni rahisi. Tunataka zile ndizi zikitoka tu shambani, zinasafirishwa haraka. Kwa hiyo hata kama ni Kilimanjaro bandari inakuwa ni Mombasa kwa sababu ya mifumo (logistics). Mombasa kila wiki kuna meli inatoka inachukua mazao ya mbogamboga. Narudi tena kwa suala la tija ndiyo changamoto kubwa.
Asilia tulikuwa na mazao mangapi ambayo tuliyachukulia kama ya biashara. Tulikuwa na chai, tumbaku, pamba, kahawa na korosho na mkonge. Hatutayaacha haya mazao, tunaweka kazi kubwa sana kuongeza tija ili mazao yaendelee. Hatuamini kwenda kwenye mbogamboga na mazao ya bustani kwa maana ya kuacha haya mengine. Haya bado tunaweza kuongeza tija na tuna kazi kubwa ya kuongeza tija. Kwa hakika nilivyokuwa Morocco, kwa mfano wafanyabiashara niliokutana nao waliniambia duniani mkonge bora unatoka Tanzania. Wana picha wanakuonyesha wanasema nyuzi zake kwa sababu ya joto, jua kwa sababu tuko karibu na Ikweta. Wanasema mkonge wetu ni bora zaidi, siyo Mexico, siyo Brazil wala Msumbiji. Lakini kuna mfanyabiashara alikuwa ananimbia yeye ananunua mkonge Spain ambao unakuwa umetoka Tanzania.
Kwa hiyo hatuyaachi haya, lakini na haya mengine tunayaendeleza vilevile na si kuayapunguzia msisitizo maana maeneo ya kulima mbogamboga nayo yapo ya kutosha. Sasa kwenye mazao ya bustani kitu kikubwa ni mifumo ya miundombinu (logistics) kwa kweli ambayo tunaifanyia kazi. Ukivuna yale yanaharibika haraka (perishable), hivyo iabidi haraka sana yafike sokoni tena katika hali nzuri. Tumekaa na TAHA na wameniletea mapendekezo yao kuna vitu wanapendekeza kwa ajili ya kuboresha logistics. Wameniambia kwa mfano Mombasa kinachosababisha baadhi ya maparachichi yanakwenda Kenya ni kwa sababu pale kuna meli inaondoka kila wiki. Siku inayoondoka inafahamika na kama una shehena unapeleka wanakupigia simu kukwambia bwana, unajua kesho tunaondoka..umefika wapi?…wahi tupakie kwenye meli. Kwa hiyo tunahitaji kitu kama hicho ambacho kitatusaidia katika bandari zetu hapa ni lazima kuwe na meli ambayo itakuwa inakuja kupeleka mazao hao. Vinginevyo bei itakuwa ndogo maana bidhaa itakaa muda mrefu na gharama ya kutunza kwenye cold rooms itakuwa kubwa. Tunahitaji mfumo uliounganishwa. Na mashamba yapo kwa sababu tulitembelea juzi hapa mashamba Arusha yaliyokuwa ya maua, mengi yameachwa ni mapori. Tunazungumza sasa ili yarudi ili wawekezaji waweze kuwekeza na kuzalisha.
Sasa tumekwisha kuanza taratibu za kuongeza maofisa ugani, lakini hata kabla ya kuongeza hawa waliopo lazima tuwawezeshe wafanye kazi vizuri.
SWALI:
Maafisa Ugani vijijini wamekuwa ni adimu sana. Hata pale wanapokuwapo vitendea kazi vimekuwa ni changamoto kubwa sana. Ni upi mkakati wa serikali kutatua shida hii ambayo inaathiri tija katika kilimo na hivyo kuzidi kuwanyong’onyeza wakulima?
PROF. MKENDA: Tuna upungufu mkubwa wa maofisa ugani na siyo hivyo tu, baadhi ya maneno au maeneo mengine maofisa ugani wamepewa kazi za utendaji. Hafanyi kazi ambazo wanapaswa kuzifanya. Hawana vifaa vya kazi, lakini baadaye anaambiwa kwamba wewe ndo utakuwa ukikusanya ushuru. Sasa tumekwisha kuanza taratibu za kuongeza maofisa ugani, lakini hata kabla ya kuongeza hawa waliopo lazima tuwawezeshe wafanye kazi vizuri.
Sasa bwana shamba anakuja kunishauri mimi na sasa mimi ndiyo namshauri yeye. Lakini mimi silaumu maana kama hatuwafanyii mafunzo rejea.
Tuwafanyie na mafunzo rejea, maofisa ugani wote. Wewe katika eneo lako hapa watu wanalima ndizi na ulimaliza chuo sijui miaka 25 na pengine hujakaa chini na kuongeza maarifa mapya kama aina mpya ya ndizi nk, ina faida gani na inahitaji nini? Maarifa mpaya ambayo yameibuka katika kulima vizuri na ni ya namna gani. Kuna wakati mwingine unasikia mkulima anakwambia mimi nilimwita yeye hapa, lakini mimi ndiye nilikuwa nikimfundisha huyo bwana shamba wako.
Mmoja aliniambia kwamba nilimwita hapa kuna mmea (sitautaja) bwana shamba akawa anauliza, hili ni zao gani hili. Sasa bwana shamba anakuja kunishauri mimi na sasa mimi ndiyo namshauri yeye. Lakini mimi silaumu maana kama hatuwafanyii mafunzo rejea, unaona semina zinafanyika kwa hiyo inabidi mabwana shamba wawepo waambiwe kuna hiki kitu kipya kimekuja, kinafanywa hivyo. Kuna maarifa mapya yamekuja, tumegundua hiki, wenzetu wamefanya utafiti huko. Kwa mfano huyu mkuu wetu wa TARI hapa ndiyo Mwenyekiti wa Bodi ya utafiti barani Afrika au Afrika Mashariki, kwa hiyo na yeye lazima na yeye awe anafikia na kujua kwamba utafiti kama ulifanyika Kenya nao ukoje, Uganda ukoje na sisi tuchukue na kujaribu huku kwetu na kuangalia jinsi ya kuupeleka kwa wakulima.