Na Mwandishi Wetu,Dodoma
Chama Kikuu cha Ushirika cha TAMKU kimeanza kutekeleza mkakati wa kupanua uwekezaji wake katika mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo, ikiwemo usafirishaji, uhifadhi na uchakataji wa korosho, hatua inayolenga kuongeza mapato ya wakulima na thamani ya mazao nchini.
Akizungumza katika Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo (Nanenane) yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Mjumbe wa Bodi ya TAMKU, Nurudini Rajabu Chikolo, amesema chama hicho kinatarajia kujenga kiwanda cha kuchakata korosho wilayani Tunduru, Mkoa wa Ruvuma, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa dira yake ya maendeleo ya mwaka 2050.
Amesema pamoja na kiwanda hicho, TAMKU imepanga kujenga jengo la utawala la ghorofa tano ambalo litakuwa na ukumbi wa kisasa wenye uwezo wa kuhudumia zaidi ya watu 700.
Kwa mujibu wake, maandalizi ya utekelezaji wa miradi hiyo yanaendelea baada ya kukamilisha hatua za awali za kupata vibali na kuandaa michoro ya uhandisi, huku ujenzi ukitarajiwa kuanza mara taratibu zote zitakapokamilika.
Chikolo amesema TAMKU pia imewekeza katika huduma za usafirishaji wa mazao kupitia mradi wa malori matano yanayotoa huduma za usafirishaji wa mizigo katika maeneo mbalimbali nchini, hatua inayolenga kupunguza gharama za usafirishaji na kurahisisha upatikanaji wa masoko kwa wakulima.
Aliongeza kuwa chama hicho kinaendelea kutoa huduma kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa mazao ya korosho, ufuta na mbaazi katika Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma na maeneo jirani, ikiwemo Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe.
Aidha, amesema kampuni tanzu ya chama hicho, TAMKU Group of Companies Limited, inasimamia shughuli za maghala ya kuhifadhi mazao, kupokea mazao ya wakulima pamoja na kusambaza pembejeo za ruzuku, hatua inayochangia kuongeza uzalishaji na kipato cha wakulima.
Chikolo aliwahimiza vijana kujiunga na vyama vya ushirika, akisema mfumo huo unatoa fursa za ushiriki katika shughuli za uzalishaji, biashara na uwekezaji, huku ukiwawezesha kujijengea kipato na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kutoa pembejeo za ruzuku kwa wakulima, akisema hatua hiyo imechangia kuongezeka kwa uzalishaji wa korosho unaosimamiwa na TAMKU kutoka tani 17 mwaka 2017 hadi kufikia tani 41,000 katika msimu uliopita, huku matarajio yakiwa ni kuongeza uzalishaji huo zaidi katika msimu ujao.


