26.2 C
Dar es Salaam
HomeKilimo BiasharaMapengo yanayolikabili soko la zabibu Dodoma

Mapengo yanayolikabili soko la zabibu Dodoma

Na Elizabeth Tanzania, Dodoma

Kwa mkulima wa zabibu mkoani Dodoma, msimu wa mavuno hauashiria mwisho wa kazi ya shambani katika msimu husika wa kilimo, lakini wakati huohuo huwa ndiyo mwanzo wa safari yenye maswali mengi kuhusu bei, mnunuzi, ubora wa zao, usafirishaji, upatikanaji wa taarifa za soko na muda ambao malipo kufanyika.

Tafiti za kitaalamu zinabainisha kuwa zabibu zinapokomaa kwa wakati mmoja, mkulima anakuwa na uchaguzi mdogo; akiamua kusubiri bei ipande, anaweza kukabiliwa na hatari ya zao kuharibika na akiamua kuuza haraka, anaweza kupata bei ambayo haikidhi gharama alizotumia kuzalisha.

Utafiti wa kitaaluma wa Felix Frank Mlay wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) unaonyesha kwamba wadau wengi wa zabibu wanakabiliwa na changamoto za taarifa za soko, mikopo, upotevu baada ya mavuno, usafirishaji, ubora wa zao, gharama za miamala na uhusiano dhaifu kati ya wazalishaji na masoko.

Utafiti huo wa mwaka unaoitwa ‘Understanding Marketing Challenges along Grapes Value Chain in Central Areas of Tanzania’ unaohusu changamoto za masoko katika mnyororo wa thamani wa zabibu unaweka bayana kuwa zao hilo huharibika haraka (high perishability).

“Kukosekana kwa maghala na makofu ya kuhifadhi ubaridi (cold storage), wakulima hulazimika kuuza zabibu kwa bei ya chini wakati wa msimu wa mavuno (kati ya TZS 500 hadi 1,200 kwa kilo moja) ili kuepuka hasara,” insomeka sehemu ya repoti ya utafiti huo wa mwaka 2021.

Hoja hiyo inathibitishwa na Batilda Kinyenje ambaye ni mkulima wa zabibu wa Dodoma, ambaye anasema ziko nyakati ambazo wakulima hulazimika kusubiri muda mrefu huku zabibu zikiendelea kupungua ubora.

“Zabibu ikishakomaa haina uvumilivu. Ukichelewa kuiuza inaanza kunyauka, inapungua uzito na wakati mwingine ndege wanaharibu,” anasema Kinyenje, akisisitiza umuhimu wa kuwa na maghala yenye mazingira ya baridi na vituo vya kisasa vya ukusanyaji.

Bei ya zabibu

Utafiti wa Mlay unaonyesha kuwa mkulima wa zabibu Dodoma anaweza kupata bei nzuri wakati fulani, na bei ya chini msimu mwingine na kwamba kuyumba kwa bei ni moja ya changamoto kubwa katika soko la zabibu katika mfumo mzima wa uzalishaji.

Utafiti mwingine uliofanywa kwa pamoja na wataalam kutoka taasisi tatu; Taasisi ya Elimu Endelevu (ICE) ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Taasisi ya Mafunzo ya Serikali za Mitaa (Hombolo, Dodoma) na Taasisi ya Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Dodoma unaonyesha kuwa wastani wa bei ya zabibu ulikuwa Sh964 kwa kilo, lakini bei ilitofautiana miongoni mwa wakulima.

Wataalamu katika matokeo ya utafiti wao uiochapishwa kwenye Jarida la Uchumi wa Kilimo na Maendeleo, Juzuu ya 10(1), kurasa 001–010, Aprili 2021 (http://academeresearchjournals.org/journal/jaed) walihusisha tofauti hizo za bei na muundo uliogawanyika wa soko, maeneo ya wakulima na umbali kutoka kwenye masoko, hasa viwanda vya kuchakata.

Tatizo la bei ya zabibu pia linaonekana kupitia wakulima ambao wanawalalamikia wanunuzi kutumia vipimo vivipo visivyo halisi ambavyo huwapunja. Musa Malogo ambaye ni mkulima wa zabibu Dodoma, anasema baadhi ya wanunuzi hutumia kreti au makasha  yakielezwa kuwana na uwezo wa kilo 20, lakini mara kadhaa mzigo husika hujazwa zaidi ya kiwango hicho.

Kwa maelezo yake, mkulima anaweza kupeleka mzigo unaodhaniwa kuwa wa kilo 20 lakini ukawa na kilo 23 hadi 25 au zaidi bila tofauti hiyo kulipwa kwa uwazi. “Wanakuja na boksi lao wanasema ni kilo 20, lakini ukipima unakuta lina kilo 23, 24 au 25. Hizo kilo zinazidi zinabebwa na mkulima,” anasema Malogo.

Anasema katika mazingira ambayo mkulima huwa na zabibu ambazo ziko tayari kuvunwa na zikiachwa muda mrefu zinaweza kuharibika, huwa hakuna njia nyingine zaidi ya kuuza kwa bei hata ikiwa ni ndogo kwani wakati huo kunakuwa hakuna muda wa kusubiri mnunuzi mwingine.

Utatuzi wa kimfumo

Biashara ya zabibu haipaswi kuangaliwa kama shughuli isiyokuwa na sheria au mamlaka ya usimamizi kwani nchini Tanzania zao hilo liko chini ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko nchini Tanzania (COPRA).

Zabibu ziliingzwa rasmi katika mfumo wa udhibiti wa COPRA kupitia tangazo la Serikali la mwaka 2024 likilitaja zao hilo kwa jina la kisayansi Vitis vinifera, katika kundi la mazao ya bustani yanayodhibitiwa chini ya mfumo huo.

Mkuu wa Sehemu ya Mazao ya Bustani na Pareto wa COPRA, Lilian Mpinga anasema taasisi hiyo inao wajibu wa kutoa bei ya msingi inayolenga kumlinda mkulima kwa mazao yaliyoko chini ya uangalizi wake na kwamba hufanya hivyo baada ya kufanya tathinini ya kitaalamu kwa mazao husika.

Mpinga anasema tathmini hiyo huzingatia mambo mbalimbali, ikiwemo bei ya soko na gharama za uzalishaji, kabla ya mapendekezo kuwasilishwa na kutangazwa kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa. “Kwa zabibu bado hatujawa na utaratibu huu wa kufanya assessment (tathimini) ya bei na kuweka base price (bei ya msingi),” anasema Mpinga, hali inayothibitisha kwamba mkulima wa zabibu hanufauki na uwepo wa COPRA.

Hata hivyo Mpinga anasema iwapo changamoto ya bei ya zabibu itaendelea kuwa kubwa, zao hilo linaweza kupewa kipaumbele katika mchakato wa kuanza kufanyiwa tathimini ili kutafuta bei yenye uwiano, mchakato mbao utafanywa kwa kuwashirikisha wakulima wenyewe, wanunuzi, halmashauri, wizara na COPRA wenyewe.

Kuhusu wizi kupitia lumbesa (kutumia mabox; mfumo usio rasmi wa vipimo unaowapunja wakulima), Mpinga anasema hauishii kuwa suala la uzito pekee bali pia uaminifu katika biashara.

COPRA inaeleza kuwa formalization (urasimishaji) ya biashara ya mazao inapaswa kwenda sambamba na ubora, vipimo na masharti yanayotambulika. Mpinga anasema pale mkataba unapoweka wazi kiwango cha ubora kinachotakiwa, bei na masharti mengine ya biashara, inakuwa rahisi zaidi kwa pande zote kudai haki zao.

“Kwa sasa mfumo huo bado haujawekwa vizuri kiasi kwamba unapotokea mkulima analalamika kwamba hajalipwa vizuri kwa sababu ya ubora, inakuwa vigumu kuthibitisha,” anasema.

Taarifa za soko na malipo

Wakulima wengi wamekuwa wakilalamikia kuwa nguvu uamuzi wa bei iko mikononi mwa wanunuzi, hasa wakati wa mavuno zabibu zinapokuwa nyingi, huku kukiwa na uhiyaji mkubwa wa soko.

 

Hata hivyo kwa mujibu wa utafiti wa Mlay mkulima asiyejua bei ya zabibu katika maeneo mengine anaweza kuuza kwa bei ya chini bila kujua kwamba mnunuzi mwingine angelipa zaidi.

Utafiti huo ulibaini kuwa takribani asilimia 72 ya wadau wa soko waliokuwa kwenye utafiti walipata aina fulani ya taarifa za masoko, lakini taarifa hizo hazikuwa zote za kuaminika.

Mbali na bei ya zabibu, changamoto nyingine ni muda wa kulipwa baada ya kuuza. Monica Ngolo, mkulima wa zabibu, anasema wakati mwingine mkulima anaweza kumaliza msimu wa kuuza lakini akakaa miezi kadhaa bila kujua atalipwa lini. “Habari ya kuuza unakaa hujui hela unalipwa lini… unaweza kukaa hata miezi mitatu hata minne,” anasema Ngolo.

Kuchelewa kwa malipo kuna athiri upatikanaji wa fedha za kuandaa msimu unaofuata, kununua dawa, mbolea, kulipia wafanyakazi, kumwagilia na kufanya shughuli nyingine za shamba, hivyo malipo yanapochelewa kwa miezi kadhaa, mzunguko mzima wa uzalishaji unaweza kuvurugika.

Wasindikaji

Stanslaus Sumezwaga, Mkurugenzi na mmiliki wa GCP Winery Investment, anasema baadhi ya viwanda vinakabiliwa na changamoto ya mtaji kwani tegemeo ni kupata mikopo kutoka benki kwa ajili ya kununua zabibu na kuendesha uzalishaji.

Anasema benki inapochelewesha fedha, uwezo wa kiwanda kuwalipa wakulima kwa wakati nao huathirika. Hii inaonyesha kuwa tatizo la malipo lina mizizi katika mfumo mzima wa thamani wa zao hilo, kuanzia mkulima hadi kiwandani.

Wasindikaji pia wanakabiliwa na gharama kubwa za uzalishaji. Daniel Molel, Meneja Uzalishaji na Mratibu wa Wakulima kutoka Central Tanzania Wine Company (CETAWICO), anasema kampuni hiyo inalazimika kuagiza kutoka nje baadhi ya vifaa na viambata vya kutengeneza mvinyo, vikiwamo chupa za kioo, vizibo vya koki, amira maalumu na kemikali.

“Vifaa vyote vya viwandani kuanzia teknolojia ya kisasa, chupa, vizibo na kemikali maalum lazima tuziagize kutoka nje kwa gharama kubwa,” anasema  Molel na kuongeza kuwa pia ushindani wa divai zinazoingia nchini kwa bei ya chini unaleta shinikizo kwa viwanda vya ndani.

Wakati huo huo, wazalishaji wa ndani wanakabiliwa na ushindani wa bidhaa za mvinyo kutoka nchi kama Afrika Kusini ambazo huingia sokoni kwa bei zinazoweza kuwa chini zaidi.

Kadhalika changamoto za ubora nazo zimeibuka katika mnyororo wa uzalishaji kwani wadau wa sekta wanasema baadhi ya viwanda vidogo hununua zabibu ambazo sukari yake hakifikii kiwango kinachohitajika kwa uzalishaji bora wa mvinyo.

Hali hiyo inaweza kuathiri ubora wa bidhaa inayozalishwa na hatimaye taswira ya mvinyo wa Dodoma katika soko la ndani na la kimataifa, hivyo baadhi ya wasindikaji wanapendekeza kuundwa kwa bodi maalumu ya zabibu itakayoweza kuratibu masuala ya bei, ubora, uzalishaji na masoko.

Wakati mjadala wa bodi ukiendelea, COPRA tayari inaeleza kuwa ina jukumu la kurasimisha biashara na kusaidia mazao yaliyo chini yake kufikia masoko. Mpinga anasema mamlaka hiyo haiishii kwenye bei na mikataba pekee, bali pia inataka kuona ubora wa mazao ukiimarika ili uwe rahisi kuingia katika masoko yenye thamani zaidi.

Kwa zao linaloharibika haraka kama zabibu, Mpinga anaona njia mbili muhimu za kulifanya soko liwe na uhakika zaidi: mikataba ya kilimo inayoweka soko kabla ya mavuno na uwekezaji katika vituo vya ukusanyaji, cold rooms na pack houses. Anaongeza kuwa usindikaji wa zabibu kuwa juisi au bidhaa nyingine pia unaweza kupunguza utegemezi wa kuuza zabibu mbichi wakati wote wa mavuno.

Kuna dalili kwamba zao hili linaanza kupewa nafasi kubwa zaidi katika ajenda ya masoko ya kimataifa kwani kwa mujibu wa COPRA, katika mwaka wa fedha 2026/27, moja ya hatua zinazotarajiwa ni kuwezesha mchakato wa kupata certification (ithibati) ya mvinyo unaotokana na zabibu ili bidhaa hiyo iweze kufikia soko la Ulaya.

“Kwa mwaka huu wa fedha 2026/27, tupo kwenye shughuli ya kuwezesha uthibitishaji (certification) wa mvinyo (wine) unaotokana na zabibu ili kupata fursa ya kuingia kwenye soko la Ulaya, hilo ndilo jambo kubwa ambalo tunalifanya sasa hivi kwenye upande wa zabibu” anasema Mpinga.

Godfrey Mathias Makenza kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) anasema mamlaka hiyo hushirikiana na COPRA katika utoaji wa vyeti vya afya ya mimea (Phyto-certification), hatua ambayo anasema ni muhimu kwa sababu zabibu zinazolengwa kwa masoko ya nje lazima zikidhi masharti ya afya ya mimea ya nchi inayoagiza.

spot_img

latest articles

explore more

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here