23.2 C
Dar es Salaam
HomeKilimo BiasharaSoko la Zabibu Dodoma: Kutoka anguko la DOWICO hadi fursa ya uwekezaji

Soko la Zabibu Dodoma: Kutoka anguko la DOWICO hadi fursa ya uwekezaji

Na Elizabeth Tanzania, Dodoma

Jua kali la Dodoma linapochomoza juu ya mashamba ya Hombolo, Mpunguzi na maeneo mengine yanayozalisha zabibu, kijani cha mizabibu kinatoa taswira ya sekta inayojaribu kuandika upya historia yake.

Kwa miongo kadhaa, zabibu imekuwa zaidi ya zao la biashara; imekuwa sehemu ya utambulisho wa kiuchumi wa Dodoma.

Lakini nyuma ya mashamba hayo ya kijani kuna hadithi yenye sura mbili: upande mmoja ni ongezeko la uzalishaji na fursa za uwekezaji, na upande mwingine ni gharama kubwa za uzalishaji, udhaifu wa mifumo ya soko, ucheleweshaji wa malipo na changamoto za tija zinazoweza kumfanya mkulima asione faida inayolingana na jasho lake.

Historia ya zao hili inarudi nyuma hadi miaka ya 1950–1980, wakati kilimo cha zabibu kilipoanza kuimarika Dodoma. Zao hilo lilianza miaka ya 1950 baada ya wamisionari kuleta miche kutoka Ufaransa kwa ajili ya uzalishaji wa divai ya ibada.

Baadaye, katika miaka ya 1970, Serikali iliamua kulikuza zaidi zao hilo kwa kujenga kiwanda cha serikali cha Dodoma Wine Company (DOWICO), kilichokuwa na uwezo wa kusindika hadi lita 31,280 za mvinyo kwa mwaka.

Hata hivyo, mdororo wa kiuchumi na changamoto za viwanda uliifanya DOWICO ishindwe kuendelea na shughuli zake na hatimaye kufilisika mwaka 1993. Anguko hilo liliathiri pia uzalishaji wa zabibu, ulioshuka hadi kufikia tani 1,060 kuelekea miaka ya 2000.

Katibu Tawala Msaidizi (Sekta ya Viwanda), Dodoma, Aziza Rajabu Mumba, anaeleza kuwa kuyumba kwa uchumi baada ya vita vya Tanzania na Uganda vya mwaka 1979 kulidhoofisha viwanda vya ndani na kuchangia anguko la sekta hiyo.

Kwa wakulima, anguko hilo halikuwa suala la kiwanda pekee. Liliacha athari kwenye mnyororo mzima wa thamani, kiasi kwamba baadhi yao walikata tamaa na kung’oa mizabibu yao.

Leo, hata hivyo, taswira inaanza kubadilika. Kwa mujibu wa takwimu za Halmashauri ya Jiji la Dodoma, kuna wastani wa wakulima 1,640 waliopo kwenye kanzidata ya Jiji, wanaolima jumla ya ekari 2,500 na kuzalisha wastani wa tani 15,000 kwa mwaka katika misimu yote miwili.

Mtafiti Mwandamizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Makutupora, Felister Joseph Mpole, anasema eneo la kilimo cha zabibu linaendelea kupanuka na kufikia karibu hekta 5,000 mwaka 2026.

“Wakulima wengi huko nyuma walikuwa wakitegemea mvua lakini sasa hivi wengi wameanza kutumia kilimo cha umwagiliaji, ambalo limeongeza mavuno kutoka tani mbili hadi tatu kwa ekari hadi kufikia tani nne hadi sita kwa ekari kwa yule aliyefuata kanuni bora,” anasema Mpole.

Ushahidi huu unathibitishwa na Agnes Woiso, Afisa Kilimo na Mratibu wa zao la Zabibu Jiji la Dodoma, ambaye anasema kuwa mkoa wa Dodoma pekee ndio unaolima zao la zabibu nchini Tanzania, ambalo linazalisha misimu miwili kwa mwaka, fursa ya kipekee ambayo haipatikani popote duniani.

Katika bajeti yake ya mwaka huu wa fedha 2026/2027, Serikali inasema umwagiliaji ni miongoni mwa nguzo muhimu za kuongeza tija. Wizara ya Kilimo imepanga kuendeleza miradi mikubwa ya umwagiliaji, ikiwamo Gridi ya Taifa ya Umwagiliaji inayohusisha pia Dodoma na Singida.

Tayari miradi 28 ya umwagiliaji imekamilishwa ikiwa na uwezo wa kumwagilia zaidi ya hekta 31,000 na kunufaisha wakulima 98,500. Mkoani Dodoma, ambako vipindi vya ukame vinaweza kuathiri uzalishaji, uwekezaji katika umwagiliaji unaweza kuwa msingi wa kuifanya zabibu kuwa zao la biashara linalozalishwa kwa uhakika zaidi.

Jedwali Na. 1: Takwimu za Uzalishaji wa Zabibu Mkoani Dodoma (2021-2025)

Mwaka Eneo (Ha) Uzalishaji (Tani) Eneo (Ha)Uzalishaji (Tani)
2021/20221,82010,1451,7549,283
2022/20232,36215,9202,22416,077
2023/20242,06613,3752,25314,802
2024/20252,25314,8022,78917,507

Gharama kubwa, faida ndogo?

Ingawa uzalishaji unaongezeka, wakulima wadogo wanakabiliwa na gharama kubwa za uendeshaji na pembejeo. Afisa kilimo na mratibu wa zao la zabibu jiji la Dodoma Agnes Woiso anabainisha kuwa pembejeo za zabibu ni ghali.

“Dawa pekee ili uweze kupata zabibu za kutosha lazima upulize si chini ya mara tano, na gharama zake hazipungui Shilingi 2 kwa ekari moja,” anasema Agnes.

Kauli hiyo inaungwa mkono na mkulima Batilda Kinyenje kutoka Mpunguzi ambaye pia anaseme:“Hapa dawa tu tulizopiga tumetumia karibu milioni moja na kitu… bado gharama za kulimia, mbolea, na uzoefu wa kupogoa”.

Mkulima mwingine Laban William Nyakapala anasema kuwa zabzibu inahitaji mbolea ya samadi ili matunda yasijae ‘sambalu’ (matunda nyonge), lakini samadi hiyo sasa kuna wakati hupatikana maeneo ya mbali kutoka yalipo mashamba  kama Bahi na Chamwino kwa gharama kubwa za usafiri.

Utafiti wa kiuchumi uliofanywa na Aristides Abdallah Nalyoto (2023) kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) wenye kichwa ‘Economic Analysis of Grape Production in Tanzania: A Case Study of Dodoma Region’ unatoa picha halisi ya kihesabu kuhusu uwekezaji huu.

Utafiti huo uliowahusisha wakulima 118 katika vijiji vya Mpunguzi, Mpunguzi A, Mpunguzi B, na Matumbulu, ulibaini kuwa wastani wa gharama ya uzalishaji wa zabibu kwa kila ekari moja ni Shilingi 831,000.

Katika gharama hii, Shilingi 195,000 pekee ndizo zinazokwenda kwenye pembejeo zinazobadilika (variable inputs) kama mbolea na dawa, huku kiasi cha Shilingi 636,000 kikichukuliwa na gharama za nguvu kazi au vibarua (labor costs) kuanzia maandalizi ya shamba, upogoaji (pruning), palizi, kupiga dawa, hadi uvunaji.

Kwa wastani wa mavuno ya kilo 1,280.7 kwa ekari yanayouzwa kwa bei ya wastani ya Shilingi 1,170 kwa kilo, mkulima anapata jumla ya mapato (Total Revenue) ya Shilingi 1,498,419 na kubakiwa na faida ya pato la jumla (Gross Margin) ya Shilingi 667,419 kwa ekari moja kwa mwaka.

Katika uhalisia wa maisha ya shambani, gharama hizi zimezidi kupanda huku bei ya zabibu ikiwa na kasi ndogo ya mabadiliko. Charles Daniel, mkulima wa skimu ya umwagiliaji Hombolo mwenye shamba la ekari moja na nusu, anaeleza uzoefu wake;

“Madawa ya kupulizia yamepanda yamekuwa juu zaidi, na mbolea ya samadi sasa hivi tripu moja inauzwa kati ya Shilingi 120,000 hadi 130,000 kulingana na umbali inapochukuliwa. Lakini bei ya ununuzi haiongezeki kila mwaka, na inaamuliwa zaidi na wanunuzi wenyewe kuliko makubaliano na wakulima.”

Kilio kikubwa zaidi cha wakulima ni juu ya ukosefu wa soko la ushindani na mifumo isiyo na usawa ya upangaji bei. Mkulima Isack Jumbe anasema;“Viwanda vinapanga bei vyenyewe bila kutushirikisha wakulima wadogo, hawaji kukaa nasi kujadili changamoto tulizopata shambani”.

Anasema mawakala/madalali mara nyingi hutumwa kununua zabibu bila mikataba rasmi na kujipangia bei zao bila majadiliano. Musa Malogo kutoka Matumbulu anaeleza unyonyaji kupitia mfumo wa “Rumbesa” (ununuzi usio rasmi)

 “Zabibu inatakiwa kupimwa kwa kilo lakini asilimia kubwa wanakadilia wanaweka kwenye mabox hawapimi kwa uzani halisi bali Boksi linalodaiwa kuwa la kilo 20 mara nyingi linakuwa na uzito wa kilo 23 hadi 25, jambo linalotuumiza sana”.

Hali hii ya unyonge wa upangaji bei pia inashuhudiwa na mkulima wa zabibu, Ezekiel Nadoa wa Hombolo na Mgaya Mkombozi (Katibu wa Chama cha Wakulima Hombolo). Nadoa anasema, “Zabibu ikishaiva haina uvumilivu shambani, tuna haraka ya kuiuza ili isioze, kwa hiyo inatubidi tu kubeba na kuuza kwa bei yoyote ile inayopangwa na viwanda”.

Naye Mgaya Mkombozi anaonya kuwa soko bado linatawaliwa na wamiliki wachache wa viwanda ambao wanajipangia bei zao wenyewe bila makubaliano ya pamoja na wakulima.

Hatua za Serikali

Jibu la kwanza linaonekana katika mipango ya Serikali ya kuongeza uzalishaji wa miche. Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo ya 2026/27 inasema mwaka 2025/2026, Serikali ilizalisha na kusambaza miche ya zabibu 342,000 kwa wakulima chini ya mpango wa ruzuku.

Waziri wa Kilimo Daniel Chongolo anasema kwa mwaka huu wa fedha 2026/27, Serikali imepanga kuongeza miche ya zabibu hadi 700,000 kwa kushirikiana na sekta binafsi, likiwa ni ongezeko la takribani asilimia 105 ndani ya mwaka mmoja.

Hata hivyo, ongezeko la miche linahitaji kuambatana na maji, teknolojia, ujuzi, mitaji na uhakika wa soko. Bila hivyo, miche mingi inaweza kuongeza uzalishaji bila kuongeza kipato cha mkulima.

Serikali imeunganisha zao la zabibu na utafiti na teknolojia. Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) imeshiriki kutoa mafunzo kuhusu kilimo bora na uongezaji thamani wa zabibu, huku katika mwaka 2025/2026 wakulima na maafisa ugani wakipewa mafunzo katika maeneo ya uzalishaji.

Tatizo kubwa: soko

Hata kama uzalishaji utaongezeka, tatizo la soko linaweza kuwa kikwazo kikubwa kwa uwekezaji.

Mkulima Isack Jumbe anasema viwanda mara nyingi hupanga bei bila kuwashirikisha wakulima wadogo. Mawakala na madalali nao, kwa mujibu wa wakulima, hununua zabibu bila mikataba rasmi na wakati mwingine huamua bei zao.

Musa Malogo kutoka Matumbulu anaeleza changamoto ya mfumo wa “Rumbesa”, ambapo zabibu huwekwa kwenye maboksi bila kupimwa kwa uzani halisi.

Kwa sababu zabibu ikishakomaa haiwezi kukaa muda mrefu shambani bila kuharibika, mkulima huwa katika nafasi dhaifu ya kujadiliana bei. Nadoa wa Hombolo anasema hali hiyo huwalazimisha wakulima kuuza hata kwa bei wasiyoiona kuwa ya haki.

Hapa ndipo uwekezaji wa kweli unapopaswa kuingia: si kujenga mashamba pekee, bali kujenga mfumo wa biashara unaowaunganisha wakulima, viwanda, wasindikaji, wafanyabiashara na masoko.

spot_img

latest articles

explore more

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here