NAFASI ya kilimo katika taifa la Tanzania ni adhimu. Kwa mujibu wa ripoti ya sampuli ya sensa ya kilimo nchini ya mwaka 2019/20 iliyotolewa na Mamlaka ya Takwimu nchini (NBS), sekta hii inakadiriwa kubeba takribani kaya 7,837,405 zikikadiriwa kuwa na watu wapatao 40,754,506. Idadi hii ni wastani wa asilimia 70 ya idadi ya watu wote wa Tanzania. Kilimo kinatupa ajira, chakula, mali ghafi kwa ajili ya uzalishaji viwandani na kuingizia taifa fedha za kigeni ambazo aghalabu ni muhimu sana kwa ajili kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi.
“Ttutakuwa daraja la kuibua fikra mpya kuhusu kilimo ili walau kwa kiasi tutoe mchango wetu katika kubadilisha mitazamo hasi.”
Kwa maana hiyo kilimo siyo kitu cha kubezwa hata kidogo. Ni kazi adhimu ambayo inatufanya tuishi. Bila chakula hayupo atakayesimama. Ni kwa kutambua nafasi ya kilimo katika ustawi wa taifa letu Jarida la FAMA limeamua kuelekeza nguvu zake zote kuandika habari za kilimo. Ni azma yetu kuwa tutakuwa daraja la kuibua fikra mpya kuhusu kilimo ili walau kwa kiasi tutoe mchango wetu katika kubadilisha mitazamo hasi (negative mind set) za watu wa taifa letu kuhusu kilimo.
Kwa miaka mingi sasa, taifa letu limekuwa na sera, mikakati na kauli mbiu mbalimbali katika kujaribu kusukuma mbele sekta ya kilimo. Mengi yamefanywa. Hata hivyo, kwa matokeo ya muda mfupi na mrefu ambayo taifa hili limeshuhudia tangu uhuru, hakika hatuwezi kujivuna sana kwamba tumefanikiwa vya kutosha katika eneo la kilimo.
Changamoto pia ziko kwenye matumizi ya huduma za ugani, upatikanaji wa mikopo.
Kwa mfano takwimu za NBS zinaonyesha kuwa kaya 7,677,291 nchini kote zinajishughulisha na kilimo. Idadi hiyo kwa vigezo vyovyote vile ni kubwa, lakini jambo la kusikitisha ni kwamba zana kuu inayowawezesha kuendesha kilimo ni jembe la mkono. Yaani asilimia 95 ya kaya hizo ambazo shughuli yao kuu ni kilimo wanawezeshwa kwa kutumia jembe la mkono. Ni dhahiri hawawezi kuongeza sana tija katika kilimo chao. Na kwa kipingamizi hicho tu, hatua zao kuyafikia maendeleo ya maana hazitakuwa kubwa.
Changamoto pia ziko kwenye matumizi ya huduma za ugani, upatikanaji wa mikopo inayoelezwa kwamba ni wakulima 294,618 tu walipata mikopo kwa ajili ya kilimo kutoka vyanzo tofauti mwaka 2020. Idadi hii yaionyeshi kuwa inaweza kusukuma mbele kilimo kwa kasi kubwa licha ya ukweli kwamba mchango wake kwenye pato la taifa unatajwa kuwa ni takribani asilimia 27.
Hali pia siyo ya kutia moyo kwenye eneo la matumizi bora ya mbolea. Takwimu za NBS zinaonyesha kuwa ni ekari milioni 2.5 sawa asilimia 21.4 ya eneo lote lililolimwa ndilo lilitumia mbolea. Kilimo cha umwagiliaji nacho ni cha kijungujiko kwani hadi sasa ni asilimia 2.3 tu ya eneo lote linalolimwa nchini ndilo lipo katika mfumo wa umwagiliaji, hali hii inafanya asilimia 97.7 ya kilimo cha taifa letu kutegemea mvua. Matumizi ya mbegu bora nayo ni changamoto kubwa. Ni asilimia 22 tu ya eneo lote lililolimwa mwaka jana ndilo lilitumia mbegu bora, asilimia 75.7 lilipandwa mbegu za kienyeji.
FAMA inatambua kuwa hizi ni baadhi tu ya changamoto za kilimo nchini. Inaelewa kwa mapana yake kwamba ili nchi hii ipate maendeleo ya kweli ambayo kwa hakika yatawagusa watu wake wengi, hakuna mbadala wa sekta ya kilimo. Ni lazima rasilimali fedha, watu, mipango na mikakati mingi zaidi ielekezwe kwenye kilimo kama kweli taifa hili linataka kubadili hali ya umasikini wa watu wake.
Kwa bahati nzuri, juhudi zote ambazo zimetoa matokeo chanya kama vile taifa kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 100, zinatokana na nguvu na kujituma kwa wakulima wadogo. Ni wakulima wadogo wadogo kwa ujumla wao wanazalisha chakula ambacho kingi kinaliwa hapa hapa nchini, lakini pia kupata ziada ya kuuza nje.
Tutakuwa wajuzi wa kubisha hodi katika ofisi za serikali, mashirika ya umma, watu binafsi, vituo vya utafiri, kutembelea waliofanikiwa katika kupiga hatua chanya katika kilimo ili kuueleza umma.
Tumejipa wajibu wa kijamii na kiutu kuwa wadau wa kweli katika kuhamasisha kilimo. Kutoa nguvu zetu kwa njia mbalimbali kuhabarisha umma, hususan wakulima juu ya mbinu gani zinafaa kwa ajili ya kupiga hatua zaidi. Ni njia zipi zinafaa kwa ajili ya kusaidia kuachana na mbinu duni za kilimo ili kupata matunda mengi na bora zaidi ya kazi na jasho la kila mmoja.
Tunaahidi kuwa tutawaunganisha wakulima wa taifa hili na taarifa za kitafiti, masoko, ujuzi wa kijasiriamali ili kuwa washirika wa kuhamasisha mabadiliko makubwa ya kilimo nchini. Tutakuwa wajuzi wa kubisha hodi katika ofisi za serikali, mashirika ya umma, watu binafsi, vituo vya utafiri, kutembelea waliofanikiwa katika kupiga hatua chanya katika kilimo ili kuueleza umma juu ya maarifa mapya ya kilimo, mbinu mpya za kilimo, ziliko rasilimali za kusaidia wakulima na taarifa mpya za maamuzi ya kisera na kisheria yaliyofikiwa kwa ajili ya kilimo nchini.
Ni rai yetu kwamba wadau wote wa kilimo watatuunga mkono.
Ni imani yetu, FAMA tutakuwa mdau wa kweli wa kuhamasisha kilimo katika taifa letu. Ni rai yetu kwamba wadau wote wa kilimo, kutoka ofisi za umma, mashirika ya umma, mashirika ya kimataifa, sekta binafsi na mkulima mmoja mmoja katika sekta yote mtambuka kwa maana ya kilimo, ufugaji, uvuvi na misitu, watatuunga mkono ili kwa Pamoja tufanikishe dhima hii tuliyoamua kuibeba mabegani mwetu kwa moyo wa dhati kabisa.